‘Hatujakomaa’ kwa midahalo ya kisiasa


Lucas Kisasa's picture

Na Lucas Kisasa - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version

NIMESOMA makala ya Nkwazi Mhango (MwanaHALISI 15 – 21 Septemba 2010) iliyobeba kichwa cha habari kisemacho: “Midahalo ya wazi itaiumbua CCM.”

Mwandishi amejaribu “kuwateka wasomaji wake,” juu ya “kilichoikimbiza CCM” kwenye midahalo katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi.

Ni vema ikaeleweka kuwa suala la midahalo halimo katika sheria, taratibu wala kanuni za uchaguzi.

Kwa nchi kama Marekani, midahalo, hasa ile ya urais, ni utamaduni uliozoeleka ingawa hauko katika kanuni za uchaguzi au sheria zake.

Midahalo wakati wa uchaguzi ni muhimu kutokana na sababu kadhaa zifuatazo.

Wagombea kupata nafasi ya kuwaeleza wapigakura sera na maoni yao juu ya masuala mbalimbali; nini watawafanya pale watakapoingia madarakani na kueleza matarajio yao katika kuleta maendeleo.

Kwa ujumla, midahalo inatoa nafasi kwa wapigakura kumwelewa mgombea au chama, mipango yake na kama anafaa au hafai kwa kile anachopigania.

Kwa nchi kama Marekani, ambayo ni kubwa na ambako kuna televisheni karibu kila nyumba, midahalo ina maana kubwa mno kwa wagombea na vyama vyao.

Lakini kwa nchi masikini kama Tanzania ambako idadi kubwa ya wananchi huko vijijini hawapati magazeti huku pia kukiwa na idadi ndogo sana ya watu wenye televisheni na redio; ni vigumu kuelewa umuhimu wa kuwa na midahalo ya kisiasa kama njia ya kufikisha ujumbe kwa wapigakura.

Inawezekana basi, pengine kwa nchi kama hii, kampeni za kutumia mikutano ya kampeni au za “mtu kwa mtu” au hata “Kitanda kwa Kitanda,” kama wanavyosema baadhi ya wanasiasa, zikawa na maana zaidi kuliko kutumia midahalo.

Lakini jambo jingine ambalo hatuna budi kuliangalia kwa makini katika suala la midahalo, ni kuhusu oganaizesheni, mfumo na menejimenti ya midahalo hiyo.

Je, midahalo hiyo inasimamiwa na nani? Inaandaliwa vipi? Nani washiriki wa midahalo zaidi ya wagombea? Taratibu na kanuni zake ni zipi?

Kwingineko midahalo inachukuliwa kwa umakini mkubwa ambapo si waandaaji tu wa midahalo yenyewe, bali hata washiriki wake huwa na makubaliano maalum katika uendeshaji wake.

Kutokana na umuhimu mkubwa wa midahalo ya kisiasa katika jamii, ndiyo maana katika vyuo vikuu mbalimbali midahalo ina nafasi katika masomo yanayofundishwa na hasa kwa masomo ya Sayansi ya Siasa.

Pamoja na kwamba midahalo kinadharia ni jambo jema, lakini kwetu ni jambo geni na ambalo halijaeleweka barabara.

Wako baadhi ya watu wanaochukulia mdahalo kuwa ni mahali pa kuumbuana na kupakaziana. Makala ya MwanaHALISI niliyoitaja inaelekea huko.

Mwandishi ametaja mambo kadhaa, yakiwemo wizi, ufisadi, asasi binafsi ya mke wa rais (WAMA), kile alichoita “ulinzi wa majini katika karne ya 21 na ahadi za mwaka 2005 – kwamba CCM ingeumbuliwa kama ingeingia kwenye midahalo.

Ni maoni yangu kuwa kwa mtaji huu, lipo tatizo kubwa kuhusu uelewa wetu wa dhana nzima ya midahalo ya kisiasa nchini.

Haiwezekani kwenye midahalo hiyo tuanze kuulizana masuala ya majini – ambapo rais wetu hajawahi hata kuzungumzia masuala ya aina hiyo; au kwanini wewe rais mke wako anatumikia chama kimoja.

Nadhani ni hofu ya aina hii kwamba wako baadhi wasiofahamu maana ya mdahalo wa kisiasa na ambao wanataka kuutumia kuleta mambo yasiyo na tija katika nchi kwa kuwachafua wengine.

Midahalo siyo suala la papara na kukurupuka kwa watu kuamua haraka na kuwakusanya watu wazima na akili zao na kuwaambia “haya njooni tufanye mdahalo.”

Mdahalo ni lazima uandaliwe kisayansi na kwa umakini mkubwa ambapo vyama vya siasa na wagombea wake watashirikishwa katika makubaliano ya namna mdahalo utakavyoendeshwa.

Lazima wajadili mambo ya kuzingatia katika mdahalo; kanuni na taratibu zake; yapi yanakubaliwa na yapi yanakatazwa. Wajadili hata mfumo wa uendeshaji.

Watajadili kwa mfano, kama wagombea watatoa hotuba ya kufafanua sera zao; maswali yataulizwa na akina nani; nani washiriki wengine – waandishi wa habari au watu wengine kutoka makundi mbalimbali.

Ikiwa lengo la mdahalo litakuwa ni kukomoana kwa baadhi ya washiriki na kuugeuza kuwa sehemu ya kutolea hasira zao, ni wazi kuwa mdahalo wa aina hiyo hautufai na wala hatuna haja ya kuwa nao.

Ikiwa chama cha siasa au wagombea wataona kuwa mdahalo hauwezi kuwasaidia kisiasa kwa nini washiriki? Kwa mfano, mwandishi anasema masuala mengine yatakayoulizwa ni kama kashfa ya Richmond na EPA.

Ni kweli kwamba haya ni masuala ambayo kwa sasa yametawala mazungumzo nchini. Inawezekana pia katika haya kuna mapungufu.

Lakini hivi kweli wako ambao hadi sasa wanatilia shaka dhamira ya dhati ya rais Kikwete katika kukabiliana na matatizo ya rushwa na ufisadi nchini?

Watu wamefikishwa mahakamani kutokana na tuhuma mbalimbali za ufisadi. Mambo mengine kadhaa kuhusiana na tuhuma za ufisadi na rushwa bado yanaendelea kufanyiwa kazi na vyombo husika.

Je, tunataka rais aanze kukiuka misingi ya utawala bora na wa sheria kwa kuagiza watu wakamatwe ovyo kwa kuhisiwa tu kuwa ni mafisadi? Je, akifanya hivyo si haohao ambao leo wanamsakama watakujageuka na kusema rais ni dikteta na hazingatii utawala wa sheria?

Kuhusu ahadi za rais, hivi ni kweli rais hajatekeleza hata ahadi moja katika zile alizoahidi mwaka 2005?

Kuna Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa shule za sekondari za kata zilizoenea nchini.

Ilani ya CCM kwa uchaguzi wa mwaka huu imeorodhesha mambo mengi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na yale yatakayofanywa katika kipindi kijacho cha 2010- 2015.

Hivyo kusema kwamba hakuna ahadi hata moja iliyotekelezwa na serikali, hiyo ni dhihaka, mzaha na utani.

CCM inaweza kuwa na mapungufu yake. Lakini ni chama kipi ambacho hakina mapungufu? Ni kweli ndani ya CCM wamo baadhi ya viongozi mafisadi na wala rushwa. Sawa. Lakini ndani ya CHADEMA, CUF na vyama vingine, wamo pia baadhi ya viongozi mafisadi na wala rushwa.

Haiwezekani kuwa CCM iwe imefanya makosa tu na kusiwe na mazuri. Kuna mazuri mengi yaliyofanywa na chama hiki na serikali zake.

Kwamba sasa watu wanapata nafasi ya kukosoa serikali yao na hata utendaji wa rais kupitia vyombo vya habari ni sehemu ya mafanikio hayo katika uimarishaji wa demokrasia ikiwa ni pamoja na uhuru wa kutoa mawazo.

Hakuna mashaka kwamba CCM hakiwezi kuondoshwa kwa midahalo. Watu wenye mawazo hayo, watafute mbinu nyingine. Ushindi unakuja kwa mipango na mikakati mizuri. Si kwa zima moto.

Lucas Kisasa ni mwandishi wa habari na meneja utawala wa magazeti ya CCM – Uhuru na Mzalendo na kada wa chama hicho.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: