‘Hatutaki mgombea asiyekigawa chama’


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Kinyang'anyiro cha Urais 2015

WANASIASA wanaamini kuwa mwisho wa uchaguzi ni mwanzo wa uchaguzi unaofuata, hata kama uko mbali kiasi gani.

Bali hali ya taifa letu kwa sasa si ya “kawaida” na kwa hiyo uchaguzi wa mwaka 2015 unatazamwa kama lulu itakayotatua matatizo yanayolisumbua taifa.

Hata ndani ya chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – hali ni mbaya. Viongozi wa juu wa chama na serikali wameshindwa kuelewa hoja na mkakati wa kutolalamika kwa vile chama chao ndicho kipo madarakani. Uzalendo umewashinda.

Sasa wameanza kutamka waziwazi kuwa hali ni mbaya na uongozi wa sasa umeshindwa kulikwamua taifa katika tope zito.

Gumzo la ni nani atakuwa mrithi wa Kikwete mwaka 2015 ni kali zaidi ndani ya CCM kuliko lilivyo ndani ya vyama vya upinzani. Siku za karibuni mikutano ya jumuia ya vijana (UV-CCM) mkoani Pwani na Dodoma, imetamka kuwa wapinzani wa ndani – wakosoaji wa CCM –  wanafanya hivyo kwa sababu ya ajenda ya urais wa 2015.

Orodha ya wanaotajwa kutaka kumrithi Kikwete ni ndefu na inaongezeka kila uchao. Wanaotajwa na wengine kujitaja ni pamoja na Bernard Membe, Profesa Mark Mwandosya, Vuai Shamsi Nahodha, Samwel Sitta, Fredrick Sumaye, Dk. Mohammed Gharib Bilali, Edward Lowassa, Hussein Mwinyi, Emmanuel Nchimbi, John Magufuli, Dk. Harrison Mwakyembe na Asha Rose Migiro.

Kwa hali ilivyo ndani ya CCM, mgombea kwa uchaguzi mkuu wa chama mwaka 2012 na hata uchaguzi mkuu wa 2015, anahitajika kuwa na sifa moja ya ziada ambayo huko nyuma haikuwa ikutumika.

Sifa hiyo ni uwezo wa mgombea kukigawa chama; yaani mgombea ambaye sifa zake na uwezo wake vinasababisha chama kugawanyika ili kukisaidia kubainisha wana-CCM wa kweli na wale ambao si waumini wa miiko, maadili na historia yake.

Hii ina maana kwamba, kama mgombea anakubalika kwa wanachama wote au wengi, basi hafai kukiongoza chama na taifa. Nitaeleza.

Nikiwa njiani kwenda Dodoma kushuhudia minyukano ndani ya UV-CCM, nimepata bahati ya kuongea na mzee mwenye hekima katika CCM. Mzee huyu amenipa wazo ambalo sikuwahi kuwa nalo.

Anasema CCM ya sasa ni kokoro lililokusanya wanachama wa aina mbalimbali; wasiofaa kukaa katika chama kimoja na kukifanya kiheshimike.

“Chama chetu kimekusanya mafisadi, wauza unga, magaidi, majasusi, wahaini, wahamiaji haramu, madalali wa raslimali za taifa, makuwadi wa ukoloni mambo leo, na mamluki wanaotalii kutoka chama hadi kingine,” ameeleza.

Kimuundo CCM kimekuwa chama cha wafanyabiashara wanaokitumia kulinda mali na biashara zao. Wakulima na wafanyakazi wamebaki kuwa nembo ya chama, lakini hawana sauti wala mamlaka.

Watu maskini na wanyonge hawaitegemei tena CCM kuwatetea; badala yake wanatetewa na vyama vya upinzani, wanaharakati na asasi mbalimbali za kiraia.

Haya ni mabadiliko makubwa katika maisha ya siasa za Tanzania, kwa sababu CCM na wazazi wake Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP) walikuwa vyama vinavyotetea haki na maslahi ya wanyonge ndani na nje ya taifa.

Kutokana na hali hiyo, mgombea wa CCM anayehitajika ili kukiokoa chama hiki na wavamizi na malimbukeni, ni yule ambaye akiteuliwa kupeperusha bendera yake wakati wa uchaguzi, wale wasiokubaliana na misimamo yake, wawe tayari kuondoka kwenye chama.

Mathalani, akiteuliwa Lowassa kupeperusha bendera ya chama, wale wanachama wasiokubaliana na misimamo yake ya kutetea, kuafikiana au kunyamazia ufisadi, waondoke katika chama kwa sababu hawawezi kutetea haki na maadili kisha wakakubali kuongozwa na mtu wanayemtuhumu ufisadi.

Akiteuliwa Sitta kugombea kwa niaba ya CCM, iwe wazi kuwa Lowassa na kundi lake wataondoka kwa sababu hawawezi kuongozwa na mtu ambaye wanadaiana fitina na wivu dhidi ya maendeleo binafsi ya wanachama wenzake.

Akiteuliwa Membe, akina Lowassa na wenzake wawe tayari kuondoka kwenye chama ili kulinda msimamo wao wa siasa za kiliberali katika uchumi. Hoja ya msingi hapa ni kuwa, hali halisi ndani ya CCM inahitaji mgombea anayegawa wanachama badala ya kuwaunganisha. 

Ni vigumu kuunganisha wanaoitwa “mafisadi” na wale wanaopinga ufisadi ndani ya chama kimoja. Naelewa wazi, hoja hii haikubaliki kwa wanafalsafa na wana sayansi ya siasa ambao hudai kuwa kutofautiana katika misimamo ya kiitikadi ni jambo la kawaida ndani ya chama.

Ndani ya CCM hali hiyo ya kukubaliana kutokubaliana haiwezi kufanya kazi kwa sababu ndiyo imekifikisha chama katika hali hii ya kuonekana kinasimamia kila kitu na kinajumuisha kila mtu.

Chama cha namna hiyo hakifai kuwa chama kwa sababu, hatimaye kinaweza pia kusimamia hata uzandiki kwa kuwa kinamkubali kila mtu na kila kitu. Kimsingi huo wala si umoja unaotakiwa na CCM, bali ni kusanyiko la watu wasio na makusudi maalum.

Tangu Baba wa Taifa aondoke madarakani, CCM ilibadilika na kuvunjilia mbali misingi na kanuni zake, kiasi kwamba wasiosafi walitumia mwanya huo kujiunga na chama, kukiteka na kukitumia kwa manufaa yao.

Kwa kuwa kila mtu anatafuta kwa manufaa yake mwenyewe, ni vigumu pia kwa watu hawa waliokiteka chama kukubaliana katika utekaji wao, na ndiyo maana napendekeza kuwa mgombea safi wa CCM awe ni yule anayeweza kukigawa zaidi chama, ili wale wanaokubaliana katika misingi ya aina fulani wabaki peke yao.

Kwa upande wa Rais Kikwete, inasemekana anamtaka rais mrithi wake atayemhakikishia usalama wake binafsi dhidi ya tuhuma za kushiriki hujuma za uchumi na raslimali za taifa.

Kutokana na majuto makubwa waliyonayo wana-CCM na Watanzania walio wengi, mgombea atakayeungwa mkono na Kikwete anaweza kuwa na wakati mgumu na asikubalike kwa wapigakura.

Hii ni kwa sababu, Rais Kikwete katika uongozi wake, amefanikiwa kujiongezea maadui wa kimaslahi bila kutengeneza marafiki wa maana wanaoweza kumsaidia katika masuala ya msingi.

Tabia ya Kikwete ya kukosa msimamo uliowazi na kuchelewesha maamuzi, mara nyingi kumeongeza nyufa ndani ya chama na kuleta hali tete katika taifa wakati wote wa uongozi wake.

Tetesi zinazosikika kuwa chaguo lake linaweza kuwa ama Asha Rose Migiro au Hussein Mwinyi, ni jitihada za kutaka kutumia ajenda ya jinsia au kuimarisha Muungano.

Kwa watu waliochoshwa na uongozi usio uongozi, hoja nyepesi kama za jinsia au muungano hazitaweza kununulika kirahisi.

Badala yake, hoja hizo zaweza kusaidia wananchi kuipumzisha CCM, ili ipate nafasi ya kujitengeneza; ili chama kingine kipate nafasi ya kuleta utawala mbadala.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: