‘JK anavunja Katiba’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version

DK. Willibrod Slaa amemtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoapa kuilinda.

Akiongea na MwanaHALISI juzi Jumatatu, alisema vitendo vya rais havilingani na kauli anazotoa ambamo anadai kuongoza kwa misingi ya sheria na kuheshimu katiba.

Dk. Slaa amesema kitendo cha Rais Kikwete kusamehe walioiba mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni ushahidi kamili wa kuvunja katiba.

Miaka mitatu iliyopita Rais Kikwete alitangazia walioiba fedha za EPA kuwa iwapo watarejesha sehemu ya fedha walizoiba, basi serikali haitawapeleka mahakamani.

Rais aliunda kile alichoita “Timu Maalum” kuchunguza walioiba fedha za EPA. Timu iliongozwa na Mwanasheria Mkuu Jonston Mwanyika.

Wajumbe wengine walikuwa Inspeka Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah.

Baada ya uchunguzi huo, rais alitangaza kuwa tayari ana majina ya wote waliokwapua mabilioni ya EPA. Alisema baadhi ya wakwapuaji walikuwa tayari wameahidi kurejesha fedha hizo.

“Kauli ya rais iliondoa ukungu juu walioiba kutoka BoT. Wananchi walisubiri serikali itoe orodha ya wezi hao, lakini hadi leo haijawekwa hadharani,” anasema Dk. Slaa kwa sauti ya masikitiko.

“Rais anasema sana kwamba nchi inaendeshwa kwa sheria na kwamba anafuata katiba, hivyo serikali haiwezi kumhukumu mtu bila ya kuwa na ushahidi wa tuhuma zake,” anashangaa Dk. Slaa.

Anauliza, “Rais anataka ushahidi gani zaidi ya walioiba kukiri kuwa waliiba? Uko wapi ushahidi zaidi ya kurejesha ulichoiba? Tunachoona ni rais kutoa msamaha kwa wezi.”

“Rais aliwataka walioiba fedha za EPA wazirudishe na watakaoshindwa kuzirejesha watashitakiwa kisheria. Kweli, wapo walirejesha na mpaka leo hawajashitakiwa mahakamani.

“Huku ni kuvunja sheria mama, kwani mtuhumiwa yeyote sharti apelekwe mahakamani kwa kuwa huko ndiko sheria itaamua iwapo ana hatia,” amesema Dk. Slaa.

“Hakuna popote katika katiba ya nchi panapotoa mamlaka kwa rais kusamehe mtuhumiwa kabla ya kuwa ameshitakiwa na kuhukumiwa.

Akisisitiza, Dk. Slaa amesema, “Nimesoma katiba sijaona popote pale, kifungu kinachompa rais mamlaka haya ya kusamehe watuhumiwa ambao hawajafikishwa mahakamani.”

“Wala hakuna mahali popote ambako katiba inatoa mamlaka kwa rais kusamehe mwizi, tena aliyekiri waziwazi kuwa ameiba,” ameeleza Dk. Slaa.

Alipoulizwa sasa rais afanye nini, Dk. Slaa alisema, “Rais hajawaambia Watanzania ukweli wa jambo hili. Wapo watuhumiwa ambao bado hawajapelekwa mahakamani kushitakiwa kwa wizi wa fedha za umma.”

“Hili ni kosa zito kwa rais aliyeapa kulinda katiba. Kama anasamehe mtu ambaye hajapelekwa mahakamani kushitakiwa je, wale walioko magerezani watolewe kwa kuwa rais ana mamlaka ya kuwasamehe?” amehoji.

Amesema nchi ikifikishwa hapo, ina maana viongozi wake hawaamini tena utawala wa sheria na kuongeza, “…hatua hiyo itasababisha nchi isitawalike kwani kila mtu aliyeko karibu au anayeweza kumfikia rais atafanya atakavyo akijua hakuna atakayemgusa.”

Wiki iliyopitam Dk. Slaa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa Rais Kikwete hajawatendea haki Watanzania kwa kushindwa kuwashitaki watuhumiwa wa ufisadi.

Alikuwa akitoa tathmini ya yaliyojiri na utendaji wa serikali katika mwaka 2011.

Mapema Januari 2008, serikali ilitangaza orodha ya kampuni 22 zilizotajwa katika ripoti ya ukaguzi uliofanywa na maodita wa kimataifa kuwa zilichota zaidi ya Sh.130 bilioni kutoka BoT.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Dk. Slaa alitaja kampuni ambazo alisema zimerejesha Sh. 70.7 bilioni.

Akiongea kwa sauti ya uchungu, Dk. Slaa alisema licha ya serikali kukataa au kushindwa kutoa hadharani orodha ya waliorejesha fedha hizo, bado pia haijaeleza ni kampuzi zipi zimekataa kurejesha fedha za wizi.

Akizidi kushusha tuhuma, Dk. Slaa amesema bado serikali haijaeleza ukweli wa zilipohifadhiwa fedha zilizorejeshwa na waliokiri kuiba.

Ajabu ya jambo hili, anasema katibu mkuu wa CHADEMA, “…ni kwamba rais haoni kuwa anawajibika kulieleza bunge masuala haya. Hii inaonyesha alivyo mzito katika kushughulikia tatizo la ufisadi.”

“Tena hapa tunarudi nyuma kule ambako watendaji wake wa vyombo vya uchunguzi waliwahi kusema kuwa, kuwashitaki watuhumiwa wa ufisadi wote waliokutwa wameiba kunaweza kuvuruga usalama wa nchi,” alisema.

Kauli hiyo ilikaririwa na mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah, IGP Said Mwema na Rais Mstaafu awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Wakati kiza kinaendelea kufunika ukusanyaji wa fedha na matumizi yake, Rais Kikwete amelihakikishia Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kuwa atasimamia misingi ya utawala bora wa fedha.

Katika barua yake kwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa IMF Christine Lagarde, rais amesema kumekuwepo changamoto katika mahusiano kati ya Tanzania na shirika hilo.

Amesema, hata hivyo, serikali yake itajitahidi kuweka nidhamu katika menejimenti ya fedha. Barua ya rais iliwasilishwa kwa Lagarde na Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkulo mwezi uliopita mjini Washington.

Wachunguzi wa mambo ya siasa na uchumi wanasema, “…kama rais hawezi kuwa muwazi kwa Watanzania, atawezaje kuwa muwazi kwa IMF?”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: