‘Katiba ya watu’ itapatikana kwa mapambano


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

MWANZO mwema huashiria mwisho mwema. Mara nyingi walioanza vibaya walimaliza vibaya. Mchakato wa katiba mpya tumeuanza vibaya tutegemee mwisho wa aina gani?

Hii inathibitishwa na malumbano yaliyopo kuanzia Bungeni hadi katika makundi ya wananchi na katika hotuba ya Rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete.

Tukiendelea kwa mwendo huu tusitarajie mwisho mwema. Wote wanaobishana ni waelewa wazuri, lakini hawaelewani. Kuna nini hapa?

Rais Kikwete alitangaza hadharani dhamira yake ya kutaka nchi ipate katiba mpya ndani ya maadhimisho ya miaka 50 ya taifa la Tanzania (siyo Tanganyika) hapo 2014. Aliamua hivyo, licha ya ukweli kwamba katika ilani ya uchaguzi mkuu ya CCM mwaka 2010, suala la katiba mpya halikuwemo.

Walioingiza suala hilo kwenye ilani ni CHADEMA na Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kilianza kuandaa rasimu. Hoja ya katiba mpya imekuwa ya vyama vya upinzani na CCM wameibaka.

Ushahidi kwamba CCM waliiteka nyara hoja, ni kauli za Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema. Wote hoja ilipokolea, walisema Tanzania ina katiba nzuri na hakuna sababu ya kuandika nyingine. Waziri Kombani alisema kwamba kwanza kuandaa katiba mpya ni gharama ambazo serikali haiwezi kukidhi.

Washauri hawa wa Rais ndio waliwatia hasira wananchi – wakaandamana. Februari Rais alitangaza haja ya kuwa na katiba mpya katika kipindi hiki cha kusherehekea miaka 50 ya uhuru. Msisitizo huo ndio ulibadili upepo wa majadala huku Kombani akidai ‘eti alikuwa anatikisa tu kiberiti’.

Hata aliyohutubia Rais, yanapaswa kuwa ni ushauri wao. Lini watu hawa walibadili msimamo “wa kutikisa kiberiti”, wakatawadha kupata udhu wa kushughulikia kile walichokitangaza kuwa ni haramu kuwapo?

Madhali wangali na msimamo wao wananchi wana haki ya kutilia shaka watakachokifinyanga na kukipeleka bungeni kikajadiliwe.

Katika serikali inayozingatia maadili washauri hawa wasingekuweko leo kwenye nafasi wanazoshika. Walishajipaka shombo nani atawaamini tena? Kiongozi akishapoteza imani kwa wananchi, anafanana na kikaragosi tu, hafai.

Kombani na Werema wangetaka kudhihirisha uadilifu wao katika uongozi, siku ileile Rais wa Jamhuri alipotangaza dhamira yake hadharani na kutofautiana nao wangeachia ngazi. Ndiyo ustaarabu wa viongozi wenye kuheshimu maadili.

Ili Rais asifanane nao alipaswa kuwatimua. Kuendelea kupokea ushauri wao kwa jambo lilelile walilotofautiana naye tena mbele ya wananchi, kunavunja heshima ya Rais, serikali anayoiongoza na kunaondoa ile “dhamira njema” aliyokuwa ameionyesha.

Rais anakuwa sawa na ndumilakuwili. Chombo kimoja cha habari kimehoji wananchi wa kawaida kujua mawazo yao kama wabunge wameutendea haki mchakato wa katiba mpya katika kuujadili bungeni.

Asilimia 92 wamesema hakukutendwa haki. Asilimia saba (7) tu wamesema ndiyo. Inahuzunisha Rais wa Jamhuri kuwa kati ya wale asilimia saba.

Wanaofurahia kupitishwa kwake wamekosa busara. Ole wao walioamua kushindana na wananchi katika hili. Hata mpuuzi anajua kuwa watashindana lakini hawatashinda.

Mchakato kupitishwa na wabunge wa vyama shirika vya CCM na CUF ni uhuni. Yampasa Rais atumie busara zake binafsi kabla hajausaini. Aelewe vizuri kuwa kuusaini ni kusaini machafuko. Aliyepewa dhamana ya nchi ni yeye. Siku ya hesabu kina Kombani hatawaona!

Siyo wahuni tu waliomo katika chama na serikali wanaoiporomosha haiba ya Rais, yeye mwenyewe hana uwezo wa kuisimamia? Sheria ya ulimwengu ipo wazi. Yanayotendwa na wateule wa Rais huvikwa juu ya mabega ya Rais wao kama nishani ivaliwavyo.

Mema humtukuza Rais wakati maovu na hadaa kama hizi humdhalilisha kiongozi mbele ya watu wake. Tunachobishania hapa ni kipi? Makubaliano yetu katiba mpya.

Mchakato wake lazima ujadiliwe na wananchi wote tangu mwanzo. Ni upuuzi kudhani kuwa katika umri wa miaka 50 tangu uhuru, bado Watanzania wanaweza kudhaniwa na baadhi ya wenzao, tena kikundi kidogo, kuwa bado ni watoto wadogo halafu wawekewe masharti na mipaka ya nini na nini cha kujadili.

Kwa sasa hilo haliwezekani. Aliweza Mwalimu Julius Nyerere enzi zile na sisi tukamwita Baba wa Taifa, hakuna mwingine! Naye angerudi leo na wazo kama hilo   wananchi wangempuuzia kwa mbali.

Kujadili hadidu za rejea kwa pamoja, kuna ubaya gani? Kuafikiana nani atakusanya maoni ya wananchi, nani atayachambua kuna ubaya gani? Haya lazima yajadiliwe na watu wote kabla ya kupelekwa bungeni kusomwa kwa mara ya pili.

Walichofanya wabunge wa CCM na CUF wakizingatia ushirika wa kuongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya mfumo Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hadaa. Ndiyo maana tuliwasikia wabunge wenye fikra finyu wakijadili watu badala ya hoja iliyokuwa mbele yao! Mbunge kumshukuru Rais katika jambo hili ni kujidhalilisha mwenyewe.

Walionesha udhalili wao! Wanaposema Rais amerundikiwa madaraka mengi yapunguzwe, haraka wakamfikiria Kikwete kama vile amelengwa yeye.

Na mbunge aliyesema katiba tuliyonayo lazima tuilinde na kuitetea kwa vile tumeapa kufanya hivyo alidhihirisha kuwa wakati anaapa alikuwa anaapa kama kasuku. Maskini mbunge huyu hajui kuwa Katiba yenyewe ina vipengele vinavyoruhusu kuibadili.

Ndiyo maana anadhani kujadili upatikanaji wa katiba mpya ni sawa na kufanya uhaini. Watu wa ovyo kutawala watu wazima kisanii haikubaliki.

Hofu yangu, sasa katiba mpya ya wananchi inaweza kupatikana kwa mapambano. Udhalimu utawasukuma wananchi katika mapambano! Wameshindwa kuelewa kuwa kati yao wote, hakuna hata mmoja mwenye ubavu wa kuwapeleka Watanzania wa leo puta kama alivyofanya Nyerere na waliomfuatia. Ole wao watu hawa!

0
No votes yet