‘Koti la muungano linawabana Zanzibar’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliotimiza miaka 48, umejaa kero ambazo kila upande, hasa Zanzibar, unaona zimekuwa karaha. Muungano huu na kero zimekuwa ni vitu vinavyokwenda pamoja – huwezi kuuzungumzia bila ya kuanza kutaja upungufu wake. Katika mada hii, SALUM TOUFIQ anapendekeza namna ya kutatua kero hizi.

MWALIMU Nyerere, akihojiwa na gazeti la Observer la Uingereza tarehe 18 Aprili 1968, alisema:

Kama ni Rais wa Tanzania, ni jukumu langu kulinda kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano.

Lakini iwapo umma wa Wazanzibari, bila ya kutumiwa na wageni, wakiwa na sababu zao binafsi, wakaona kuwa Muungano hauna maslahi kwao, sitoweza kuwalazimisha kubaki katika Muungano.

Pale upande mmoja ukiondoa ridhaa yake, muungano utakuwa tayari umesita. (Tafsiri ni yangu).

Hapa, ninasimamia nukuu hiyo. Katika harakati za kupitishwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Wazanzibari wameonesha wazi kuchoshwa na Muungano uliopo sasa. Wazanzibari walio wengi pamoja na viongozi wao, wakiwemo mawaziri na viongozi wa dini, wamesema waziwazi muungano huu wa miaka 48 hauna maslahi kwao.

Na “Baba wa Taifa” alishaota ndoto hiyo; leo kero za muungano zinaonekana zaidi kwa ndugu mdogo kuliko kwa kaka mkubwa.

Wapo Watanganyika wanaodai Tanganyika yao, ingawa ni wachache. Waliowengi, kuwepo au kutokuwepo kwa Zanzibar katika muungano hakuwaathiri chochote.

Hawa wanaona ukubwa wa ardhi, idadi ya watu na raslimali nyingi walonazo zinaitoa Zanzibar kama mshiriki mwenza katika Muungano. Hili likichanganyika na “kero ya Wazanzibari” kila siku kufanya kelele linawafanya waone Muungano hauna maana tena kwa Tanzania.

Wapo wanaoona Zanzibar “haina shukrani” kwa kuwa ati inategemea Bara kwa kila kitu – chakula, nguvu kazi na hata fedha za kuendesha nchi. Hawa ndio wengi wanaosema muungano unawanufaisha zaidi Wazanzibari na itakuwa ni kujitia kitanzi ikijitoa.

Tabaan. Kwa wote hawa basi na warudi kwa Mwalimu Nyerere. Sasa Zanzibar na Wazanzibari wesharidhika kuuchoka muungano. Kuna haja gani ya kuunda Tume ya Katiba kukusanya maoni ya wananchi?

Agenda kubwa kwa Wazanzibari ambayo ni suala la kuwepo au kutokuwepo kwa muungano si miongoni mwa hadidu rejea za Tume.

Wakati wajumbe wakiapishwa Ikulu, Dar es Salaam, 13 Aprili 2012, Rais Kikwete alisema wazi wanaohubiri kuvunjika kwa Muungano hawatasikilizwa!

Mtu atajiuliza: nini sasa faida ya kukusanya maoni kama hutaki kiini cha matatizo kijadiliwe?

Katika kulijadili hili naomba tukisome tena kitabu cha Baraza la Katiba, Zanzibar: Katiba Tuitakayo – Sheria ya Kuandika Katiba Mpya ya Tanzania na Suala la Muungano kwa Zanzibar, hususan Sura ya Nne (Uk.22 – 29).

Maana yake ni kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Tume, hata kama asilimia 100 ya Wazanzibari wakisema wameuchoka muungano, hawatasikilizwa.

Hapa ndipo ninapouona udhaifu mkubwa wa Sheria ya Tume hii. Nini hasa faida ya kuunda Tume na kutumia zaidi ya Sh. 40 bilioni ambayo matokeo yake si kupunguza kero za muungano?

Naliunganisha hili la kuundwa kwa Tume ya Katiba na kupitishwa kwa Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar (Sheria Nam. 9/2010). Marekebisho haya yameingiza vifungu vingi ambavyo kwa maumbile yake vinaonekana vikisisitiza Utaifa wa Zanzibar. Kifungu cha 1 kinasema:

Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka, na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Kifungu cha 2A nacho kimetoa mamlaka kwa Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo. Pia viko vifungu vyengine vinavyoonesha dhahir kujibu kejeli ya kaka wakubwa kwamba Zanzibar ni mkoa tu wa Jamhuri.

Tunafahamu jinsi mara kadhaa wanasiasa wa Bara na hata mahakama ya juu Tanzania (Mahakama ya Rufaa) walivyosisitiza Zanzibar si nchi.

Kwa maana hiyo hata ukifanya njama ya kutaka kumuondoa Rais wa Zanzibar madarakani kwa mtutu wa bunduki, haitakuwa uhaini.

Ni sawasawa na kujaribu kuiondoa Halmashauri ya Mji wa Chake Chake, si jambo la kushtua!

Ninaamini kitendo cha Baraza la Wawakilishi kupitisha marekebisho hayo kimekuja wakati muwafaka. Pale mwenzako asipofahamu lugha unayoitumia, muhimu utafute lugha atakayoifahamu.

Kubadilisha Katiba imekuwa lugha muwafaka kuwafanya wenzetu waone nini tunataka. Marekebisho ya Katiba yameibua lawama tele kutoka kwa wanasiasa na hata miongoni mwa wanasheria mahiri Bara.

Wengine wamesema Muungano wa Tanzania haupo tena baada ya Zanzibar kujitangaza ni nchi! Naziona hizi zote ni kelele za mlango tu.

Kwa upande mwengine naamini Marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya 2010 pamoja na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ndiko kulikosukuma kaka zetu wakubwa kuleta kiinimacho cha Tume ya Katiba.

Kama kweli lengo la Tume ni kushughulikia kero za muungano na kuuimarisha basi hilo lilipaswa kufanywa zamani, pale kelele za Wazanzibari na hata za makundi kama G55 ya Bara yalipoibuka kudai Serikali ya Tanganyika.

Lakini, hali iliwachwa tete. Waliokosoa Muungano wakaitwa wasaliti wasioitakia mema nchi. Kuunda Tume ya Katiba sasa ni sawa na kujaribu kuyazuia maji ya bahari yasifike ufukweni wakati wa bamvua.

Kuwepo au kutukuwepo muungano ndio suala la msingi hata kabla ya kuunda Tume. Zanzibar ipo Sheria ya Kura ya Maoni, 2010. Bara hawana, lakini hilo haliathiri chochote. Kama alivyonukuliwa Mwalimu hapo mwanzoni; Muungano hauwezi kuwepo endapo upande mmoja utaukutaa.

Cha msingi ni kulipeleka suala hili kwa wananchi wenyewe walitolee uamuzi. Viongozi wanahofu nini? Isije ikatufika hadithi ya Abunuwasi ya kuwekwa uchi halafu tukaamini hatuonekani!

Ninaamini muungano ni ridhaa ya nchi mbili zilizoungana. Muungano wa Serikali mbili au viongozi wawili bila ya baraka za watu wenyewe hauna maana. Hivyo iwapo upande mmoja utasita kuridhia kubaki katika muungano, huo unakuwa si muungano tena.

Sasa leo ya nini kuunda Tume na kupoteza mabilioni ya shilingi kujaribu kuutengeneza upya muungano ambao tayari viashiria vyote vinaonesha ushapitwa na wakati?

Si ingetosha tu kuuliza Watanzania kama wanautaka au hawautaki? Kungekuwa na haja gani ya kutaka uwe madhubuti kama wengi hawautaki?

Wazanzibari wakisema hawautaki, dawa iliyobaki ni moja tu: kumaliza taratibu mambo ya muungano. Udugu wa watu wetu na mahusiano ya kidiplomasia vitandelea.

Marehemu Karume aliunasibisha muungano na koti: likikubana utalivua tu. Nadhani koti la Muungano limekuwa linawabana sana Wazanzibari na lililobaki ni kulivua tu. Tukingoja sana itabidi tulichane; litashindwa kuvuka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: