‘Mafisadi’ wanakumbatiwa, watetezi wanadhihakiwa!


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Rais Kikwete na Rostam Aziz

NIMEPITIA kitabu cha Zaburi nikakutana na maneno: “Kama misingi ikiharibika, mwenye haki atafanya nini?” Hicho ndicho tunachokishuhudi leo nchini. Misingi ya taifa inabomolewa kwa kasi, huku waadilifu, wazalendo, na wanaolitakia mema taifa wanaulizwa, “Mtafanya nini?”

Miaka michache iliyopita alitokea kiongozi wa chombo cha dola ambaye aliwatangazia wananchi kuwa “nchi imetekwa nyara” na hakuitwa mchochezi. Akatokea kiongozi mwingine mkubwa akasema, “mafisadi wakikamatwa nchi itawaka moto.” Naye hakuitwa mchochezi.

Akaja mwingine akaficha mamilioni ya shilingi nje ya nchi. Ni Andrew Chenge. Wananchi walipomuuliza akasema vilikuwa ni ‘vijisenti” na kusababisha hasira kali kwa wananchi dhidi ya serikali iliyoshindwa kutoa maelezo ya jinsi gani mtumishi huyo wa umma aliweza kuwa na mamilioni hayo ya shilingi bila kuyatolea taarifa.

Huyu hakuitwa mchochezi. Tena alipewa kazi ya kusimamia maadili ndani ya chama chake na licha ya kuhusishwa na vifo vya watu wawili kutokana na uzembe wake na kufoji bima, bado chama chake kimeshindwa hata kumpa onyo. Akahusishwa na kashfa ya Tangold hakuna aliyemuuliza.

Lilikuwepo genge la wajanja wa biashara na kisiasa ambao waliamua kuliingiza taifa kwenye mkataba mbovu wa Richmond na baadaye wa Dowans huku wakitoa taarifa mbalimbali za ulaghai.

Wakawezesha kampuni ya Richmond kupewa mkataba na TANESCO wakati haina uwezo na baadaye wakatuletea kampuni ya rafiki yao wakituambia inatokea Costa Rica kumbe inatokea Falme za Kiarabu.

Kinara wao ambaye ni mbunge maarufu wa CCM, Rostam Aziz mwanzoni akikana kuhusika, lakini baada ya kuona mabilioni yanakaribia mlangoni, akajitokeza na kusema pasipo shaka kuwa kweli yeye ni mhusika. Wote hawa hawakuitwa wachochezi!

Tena Rostam siyo tu anatajwa kwenye kashfa hii! Anatajwa katika kashfa nyingi ikiwamo wizi wa fedha za EPA kupitia kampuni yake ya Kagoda.

Mtu ambaye angeweza kuisaidia TANESCO toka mwanzo kwa kuwapa taarifa sahihi ili wasije kuingizwa mjini akiwa na wajibu wa mtu mwenye hadhi ya Bunge na mtu wa karibu na Ikulu.

Pamoja na Rostam kutajwa na yeye kukiri kuhusika na Dowans Holdings S.A kampuni hewa ya Costa Rica (Falme za Kiarabu na Oman), hakuna chombo chochote “cha dola” ambacho kimewahi kuwa na ubavu hata wa kutaka “kauli rasmi” kutoka kwake.

Wananchi wamekerwa na hilo. Wanahoji: Hivi mtu mmoja anaweza kulipigisha taifa zima kwata kiasi cha jarida moja maarufu duniani kumuita kuwa ndiye “king maker” wa Tanzania! Hadi sasa, siyo usalama wa taifa wala polisi waliomuweza Rostam. Anaonekana ana nguvu kwelikweli.

Yaani hadi rais wa nchi analazimika kusimama hadharani na kuliambia taifa kuwa “hawajui wamiliki wa Dowans” wakati swahiba wake mkuu Rostam ndiye aliyewaingiza nchini! Hatujamsikia yeyote kikisema, huyu analeta uchochezi na anatishia amani!” 

Kwamba ukimsikiliza John Chiligati, mafisadi siyo wachochezi wa chuki dhidi ya serikali na chama tawala.

Ndugu zangu, misingi imebomolewa; wenye haki watafanya nini?

Qurani Tukufu nayo inatudokeza juu ya suala hili la kuhakikisha misingi haivunjwi na kuwa haki inatendekea. Mwenyezi Mungu ameweka Mizani ili msidhulumu katika vipimo vyenu” (Surat 55:7-9). 

Lakini wenzetu wamegeuza kipimo; wameamua kubadili mawe ya mizani na kutaka kudhulumu Watanzania kwa kuwanyima ukweli. Badala ya kuwang’ang’ania mafisadi katika serikali yao na kuwatimua kutoka chama chao ambao ndio hasa wachochezi kwa misingi ya sheria zilizopo, wao wamegeuka na kuwatuhumu watetezi wa wanyonge.

Swali kubwa ambalo kila mwananchi mwenye akili timamu anatakiwa kujiuliza sasa ni hili: Je, tuko tayari kuukubali uongo kuwa ukweli? Tuko tayari kuiita pombe maziwa na kuwapatia watoto wetu wanywe; tuko tayari kuona mafisadi wanatukuzwa na watetezi wanapuuzwa?

Hivyo, ndugu zangu tunachogombania sasa hivi kinyume na wana CCM wanavyofikiria siyo madaraka yao kututawala wapendavyo, bali madaraka yetu juu yao! Tunachogombania siyo utajiri wa wanachama wao, bali utajiri wa taifa letu!

Tunachogombania siyo ardhi iliyo mikononi mwao bali kuiondoa mikono yao toka kwenye ardhi yetu. Huu ni ugomvi wa kifikra, na ushindani wa hoja zenye kutulazimisha tuupatie udhuru ufisadi na hoja zinazotufungua macho kuukataa ufisadi.

Kinachofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika maandamano na mikutano yao siyo uchochezi. Wanapotuambia kuwa mafisadi wameling’ang’ania taifa na kuwa kushindwa kwa serikali kuwadhibiti na kuwatia pingu kutalifikisha taifa kwenye hali ya Misri, Tunisia, Algeria na Libya, kwamba serikali iliyoko madarakani na vyombo vyake imeshindwa kutetea maslahi ya wananchi, huu siyo uchochezi.

Kila anayetakia kheri anatambua hali halisi iliyopo nchini. Haitaji CHADEMA kumuambia kuwa kuna mfumuko wa bei, hahitaji Mbowe au Dk. Slaa kumueleza tatizo la nishati ya umeme nchini linatokana na sera mbovu na usimamizi mbovu wa serikali iliyoko madarakani!

Hahitaji kuambiwa na Dk. Slaa kuwa mfumo wetu wa uchaguzi, sheria na utawala unahitaji mabadiliko makubwa! Kima mmoja anayajua hayo na anayefikiria hivyo, atakuwa anawadharau wananchi.

Ni kwa sababu hiyo basi uchaguzi uko mbele yetu. Mstari uliochorwa ardhini sasa umevukwa. Je, tuinamishe vichwa vyetu kwa woga mbele zao? Je, tukubali kuwaimbia nyimbo za sifa na shangwe huku nasi tumevaa magwanda ya njano na kijani huku wametushikia mijeredi ya miiba migongoni mwetu? 

Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu (Surat Ar-rum 30:41)

Wasio haki hutembea pande zote, Ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu (Zab. 12:8)

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: