‘Mafisadi’ waziteka kampeni za Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Zakhia Meghji

KAMPUNI iliyopewa kazi ya kukusanya fedha za kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Push Mobile Media Limited – inahusishwa na watuhumiwa wa ufisadi nchini, MwanaHALISI limegundua.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo katika ofisi ya Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA), mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo ni Peter Noni.

Hivi sasa Noni ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Raslimali ya Taifa (TIB); nafasi aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete yapata mwaka mmoja sasa.

Kabla ya uteuzi wake, Noni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Mikakati na Utendaji katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amekuwa akisakamwa kwa tuhuma za ufisadi ndani ya benki hiyo.

Kwanza, mlipuko wa ufisadi ndani ya BoT ulitokea Noni akiwa mtu wa madaraka makubwa na wa karibu na Gavana Daudi Balali aliyebebeshwa mzigo wote wa wizi wa aina yake nchini.

Pili, kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Timu ya Rais Kikwete aliyoiunda kuchunguza wizi BoT, karibu watuhumiwa wote wa ufisadi waliofikishwa mahakamani walimtaja Noni kuwa mshirika mkuu katika kufanikisha wizi huo.

Leo hii, moja ya makampuni mawili yanayounda Push Mobile Media Limited, iliyopewa kazi na CCM, inamilikiwa na Peter Noni.

Kampuni hiyo ambamo Noni ni mkurugenzi inaitwa Six Telecoms Company Limited (STC) iliyosajiliwa Dar es Salaam kwa hati Na. 50940.

Mkuu huyo wa TIB ana hisa 700 kati ya hisa 1,000 za STC. Hisa zilizosalia zinamilikiwa na wenzake wawili, Dk. R. W. Tenga na Hafidh M. Shamte.

Ni Noni aliyekuwa bosi wa Esther Komu, Imani Mwakosya na Bosco Kimela ambao ni miongoni mwa wafanyakazi wa BoT waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi.

Watumishi hao wa benki wamekuwa wakidai kuwa Noni ndiye alikuwa mwidhinishaji wa malipo yote ya fedha zilizokombwa na wanashangaa kwa nini hayuko kizimbani.

Rais Kikwete alimteua Noni kuwa bosi wa TIB katikati ya tuhuma hizo.

Kana kwamba rais hasikii tuhuma hizo, akasema fedha zote zinazokusanywa kutoka kwa mafisadi waliokiri na hivyo kuepushwa kupelekwa mahakamani, zitapelekwa TIB ambako zitasimamiwa na Noni.

Hadi sasa Noni hajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zozote zile za ufisadi na malalamiko ya wafanyakazi wenzake hayajafanyiwa kazi.

Kwa hiyo Noni wa BoT ndiye yuleyule wa TIB anayeshughulikia fedha zilizoibwa BoT; na kampuni yake ndiyo inashughulikia ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kampeni za CCM mwaka huu.

Kampuni nyingine inayounda Push Mobile Media Limited ni Opera Telecoms. Kila kampuni inamiliki asilimia 50 ya hisa za Push Mobile.

Wiki mbili zilizopita, CCM ilizindua mpango wa kutafuta fedha za kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu, ambapo imepanga kukusanya zaidi ya Sh. 40 bilioni zikiwamo zile za kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms).

Taarifa kutoka BRELA zinaonyesha kuwa kampuni ya Push Mobile ilisajiliwa 28 Februari 2006 na kupata hati ya usajili Na. 56155.

Six Telecoms ina ofisi katika jengo la Barclays, mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam. Inatumia anwani ya S.L.P 11133, Dar es Salaam.

Anuani ya kampuni ya Opera Telecoms ni 3 Brindley Place, Birmingham -1 2JB nchini Uingereza.

Kuwapo kwa Noni katika umiliki wa Push Mobile, kunajenga uwezekano mkubwa wa kuwapo ubia au ushirikiano na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Noni na Rostam ni wabia katika biashara – kwa pamoja wanamiliki hisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Noni na Rostam walikuwa wanamiliki asilimia 35 ya hisa katika kampuni ya hiyo.

Noni alikuwa anamiliki hisa zake kupitia kampuni ya Planetel Communications Limited, huku Rostam akimiliki kupitia kampuni ya Caspian Construction Limited.

Hivi sasa hisa hizo 35 zinamilikiwa na kampuni ya Mirambo Limited ambayo taarifa za mtandao hazionyeshi iwapo zinamilikiwa kwa pamoja au na Rostam peke yake.

Miaka miwili iliyopita wamiliki wa Mirambo walipeleka maombi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutaka kuuza hiza zao katika Vodacom kwa wawekezaji wa nje; lakini imeripotiwa serikali iliwakatalia.

Rostam anamiliki makampuni mengi nchini, lakini hakuna hata moja ambako jina lake linaonekana wazi isipokuwa katika hisa za Vodacom.

Hata katika kampuni ya uchapishaji magazeti ya New Habari Corporation Limited, ambayo amekiri hadharani kuimiliki, jina lake halionekani.

Naye Noni, katika ushahidi wake mahakamani, katika moja ya kesi za watuhumiwa wa ufisadi BoT, alisema kila kitu katika kashfa kilitendwa kwa maelekezo ya aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali.

MwanaHALISI lilimtafuta Rostam kutaka kujua iwapo yumo katika Push Mobile inayokusanya fedha za CCM.

Akijibu kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, Rostam alisema, “Asante kwa ujumbe wako. Naomba uninukuu kwa ukamilifu kama ifuatavyo.

“Nawashangaa kwamba kwa mara ya kwanza mmeona haja ya kuniuliza na kutaka maoni yangu juu ya uzushi ambao mmekuwa mkiuandika dhidi yangu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, huku mkijua hauna ukweli wowote,” alieleza.

Alisema gazeti limekuwa likitimiza malengo ya “kuwatumikia wale wanaojaribu kunichafua bila mafanikio.”

Bali alisema, “…na huu (uzushi) mlioamua kuniuliza leo, ni uzushi mwingine ambao sielewi unatoka wapi; lakini endeleeni nao tu…”

Rostam amekuwa akituhumiwa katika ukwapuaji mabilioni ya shilingi kutoka BoT na hasa kwa kutumia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited. Hajakamatwa.

Naye Zakia Meghji alipoulizwa iwapo anajua kuwa mmoja wa wamiliki wa Push Mobile ni Peter Noni, alisema, “Sisi tuna-deal (tunashughulika) moja kwa moja na makampuni ya simu ya tiGO, Zain na Vodacom.”

Alikiri kujua kuwa Noni ndiye mmiliki wa Push Mobile. Meghji ni mwenyekiti wa kamati ya kukusanya na kutumia fedha za CCM wakati wa uchaguzi.

Dk. R.W. Tenga anayetajwa kuwa mkurugenzi wa Six Telecoms, sasa ndiye mwanasheria wa BoT.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: