‘Naapa CCM haitamjadili Mansour sasa’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAKATI huu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapokabiliwa na mtihani mgumu wa kurejesha imani kwa wananchi kupitia kaulimbiu yake ya “kujivua gamba,” siamini kama kina nafasi ya kumjadili Mansour Yussuf Himid.

Mansour ni waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoendeshwa kwa ushirika kati ya chama hicho na Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa hasimu wake mkubwa kisiasa.

Ni mwanasiasa kijana huyu ambaye amekuwa akiimarisha rekodi yake ya utendaji wa moyo wa kizalendo juu ya Zanzibar, nchi mama yake.

Tangu alipokuwa chini ya Amani Abeid Karume (2000-2010), Mansour alionyesha kupenda sana nchi yake. Aliitetea kila palipohitajika.

Alijitahidi kujieleza kwa hisia kila alipohojiwa kwa jambo hili au lile lililokuwa mamlakani mwake tangu akiwa Waziri wa Nchi, Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira chini ya Burhan Haji Saadat 2000-2005.

Alipopandishwa hadhi kuwa waziri kamili baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, Mansour siyo tu aliongeza kasi ya utendaji kazi kizalendo, bali pia alitumia fursa zilizoibuka na alizojitengenezea kujijenga kiuchumi.

Ni hapa alianza kulamba asali hata kuthubutu kuagiza ununuaji wa mitambo anavyoona yeye hata kama ilikuwa ni maono tofauti na yale ya wataalamu.

Zilipoingia zama za mwisho kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, Mansour alisimama kama mtaimbo kutekeleza dhamira ya rais.

Itakumbukwa hiki kilikuwa ni kipindi cha Karume kutafuta hatima yake ili apate maisha tulivu ya kustaafu baada ya kuitumikia nchi kwa miaka kumi mfululizo.

Ilikuwa ni muhimu kufuta dhambi za kiuongozi zilizoanzia mauaji ya raia kadhaa ya Januari 26-27, 2001.

Mansour akawa bega kwa bega kumsaidia kutimiza kila alichokipanga. Ni kijana huyu aliyeficha siri ya mipango ya Karume ambaye ni shemegi yake mara mbili – amemuoza dada yake, Shadya, naye kuoa kwao Karume – ya kutafuta maridhiano na Maalim Seif Shariff Hamad.

Hiki kilikuwa kitendawili kikubwa isivyo kawaida kwa Wazanzibari. Hakuna aliyegundua haraka mipango ile. Hata pale ilipotangazwa rasmi kuwa Karume alikutana na Maalim Seif Novemba 5, 2009 Ikulu kuu ya Zanzibar, watu bado walijiuliza nini hasa kinachopangwa.

Mansour alijua kila kitu. Najua alijua kila kitu. Niliwahi kusimuliwa kauli zake wakati akisimamia maagizo ya rais kuhusu mipango ya maridhiano. Alikuwa jasiri hasa na namsifu kwa hili la kuhifadhi siri ile mpaka ilipolazimu kuanikwa.

Hatua zile zilienda sambamba na mipango ya kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi asilimia inachomolewa kutoka mambo ya kusimamiwa kimuungano.

Ni Mansour aliyeongoza kampeni ndani ya serikali na Baraza la Wawakilishi. Yeye ndiye alikuwa waziri mhusika wa wizara inayohusu nishati.

Alikuwa kinara wa kuliambia Baraza kuwa serikali inataka kuweka mazingira ya kisiasa na kisheria kuwezesha kusimamia yenyewe utafiti na uvunaji wa raslimali hiyo ili Zanzibar inufaike moja kwa moja na raslimali hiyo iliyothibitishwa kuwepo katika ardhi ya Zanzibar.

Aliibeba dhamira hiyo hadi barazani. Alitoa hoja za serikali na akaahidi kuhakikisha utekelezaji wa yaliyoazimiwa na Baraza.

Ni Mansour aliyeahidi wananchi wa Zanzibar kupitia baraza lao kwamba kwa kuwa serikali imeshaamua na baraza limeidhinisha kwa kutoa azimio, hakuna kurudi nyuma.

Wakati akisimamia hili, alikuwa akitoa kauli nzito kwa Serikali ya Muungano bali pia akiashiria kutohofia chochote kwa chama – CCM.

Akapita vizuri na kukamilisha yale yaliyowezekana kabla ya uchaguzi. Akashinda tena uwakilishi Kiembesamaki; akabahatika kurudi waziri.

Mansour sasa ni waziri anayehusika na Kilimo na Maliasili ambako pamoja na kuwa suala la nishati haliko moja kwa moja kwenye utawala wake, anajivunia kuweza kulizungumzia kwa kuwa nayo ni maliasili ya nchi.

Si hivyo tu; katika nafasi yake ya uwakilishi jimboni, ana haki ya kutoa maoni yake (yakichukuliwa ni maoni ya wanajimbo), kunapokuwa na mjadala unaolenga maliasili za nchi.

Kwa hivyo basi, kwa muda wote huo Mansour akiwa serikalini – hapo kabla alikuwa katika sekta binafsi - amekuwa muwazi kusema kile anachokiamini.

Na katika kutumia haki yake hiyo ya kikatiba na kama kiongozi, anatoa kauli zenye sauti bila ya kujali kama kuna watu watakasirika. Kumbuka nilitangulia kusema huyu ni jasiri – haogopi mtu yeyote.

Ni Mansour aliyechagiza muswada wa marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ufutwe maana Zanzibar haijashirikishwa katika kuandaliwa kwa muswada.

Kwanza alisema kitendo cha kamati kuwaita wananchi kutoa maoni kuhusu muswada, ni sawa na kuwadanganya, halafu akaapa kuwa “Wazanzibari tutapinga muswada iwe katika Baraza la Mapinduzi, hadharani au katika kikao cha faragha.”

Ni kauli zile nzito zikiwemo za mawaziri wenzake kadhaa, zilizolazimisha uongozi wa serikali Bara kutia kwapani muswada na hatimaye kuuondoa katika mjadala bungeni.

Leo muswada unarudishwa huku Zanzibar ikibainishiwa mamlaka yake kamili kama mshirika mkuu wa muungano na Tanganyika.

Mansour ameibuka tena. Akichangia hoja ya makadirio ya matumizi ya wizara ya Ardhi, Maji, Makazi na Nishati, aliponda mfumo wa serikali mbili na kupendelea wa serikali tatu – sera ya CUF.

Katika kauli iliyochangamsha baraza na kujikuta akishangiliwa na wajumbe wa CUF, Mansour alisema: “Hapa mpango wa serikali moja hatutaki kuusikia. Mfumo huu butu wa serikali mbili, sasa basi, (busara) twende kwa jambo ambalo kila mmoja wetu analizungumza la serikali tatu na mengineyo.”

Sasa anaonekana msaliti wa sera za chama chake. Wanaojitambulisha kama makada wanampangia zengwe. Utaratibu uleule wa kishetani wa kutunga vipeperushi umekuja kumsakama.

Makada hao wanamwambia: “Wewe ni Mjumbe wa NEC-CCM; Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar; Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC Zanzibar ukiongoza Idara ya Uchumi na Fedha, kwanini hukusema hayo katika vikao halali vya chama?” Wanamtuhumu kwa msimamo wake huo dhidi ya serikali mbili kwamba “anataka kuvuruga tena wana-CCM na kuzorotesha umoja wa kitaifa uliopo tangu kuasisiwa kwa Muungano mwaka 1964.”

Hakuna historia ya Polisi kushughulikia vipeperushi vya namna hii maana viliwahi kuwa vingi kuchapishwa na kuenezwa sehemu za mikusanyiko ya watu katika mji wa Zanzibar.

Hivi vilieneza siasa za chuki dhidi ya wanasiasa wa CCM wenyewe na kwa upande mwingine vikilenga kuchafua CUF na viongozi wake, hasahasa Maalim Seif.

Ninaamini Polisi ambao hawakufanya chochote juzi na jana kuhusu vipeperushi, hawathubutu kuchunguza leo wakati CCM na CUF wanapanga na kutekeleza mipango mimoja chini ya “siasa za maridhiano.”

Ni hapo pananishawishi kuamini katu CCM haina nafasi ya kumhangaikia Mansour maana ikifanya hivyo, itazidi kutanua wigo wa mazonge yaliyokijaa na ambayo yanahatarisha kubaki kwake madarakani.

Najua, Mansour hana hofu; ametulia. Huyu jasiri bwana!

0
No votes yet