‘Ndesa’: Nimeshinda kabla ya uchaguzi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), anasema yeye ni mbunge tayari kwa kipindi cha 2010 – 2015.

“Pale Moshi Mjini wananchi wamenieleza, ‘Mzee tulia, kazi imekwisha.’ Ni kwa sababu wameona kazi tuliyowafanyia,” anasema Ndesamburo.

“Sina mpinzani. Simuoni wa kuniangusha. Wote wanaotajwa kutaka kugombea Moshi Mjini, wanacheza ngoma wasiyoijua,” anasema Ndesamburo katika mahojiano na MwanaHALISI wiki hii.

Anasema wananchi wa Moshi Mjini wanajua jinsi alivyowatumikia. “Wanajua jinsi nilivyosimamia rasimali zao; nilivyopigania maendeleo yao na wanafahamu kazi iliyofanywa na wabunge wa chama chetu ndani na nje ya Bunge.”

Kauli ya Ndesamburo ilitokana na kile kinachoitwa na viongozi wa CCM “Mkakati wa kumng’oa Ndesamburo” Moshi Mjini.

Anasema hata kabla ya kampeni kuanza na uchaguzi kufanyika, tayari yeye anajihesabu kuwa ameshinda. Hata wapigakura wake wamemhakikishia hilo.

Anasema kujiamini kwake kuwa tayari ameshinda kiti hicho cha ubunge hata kabla ya uchaguzi kufanyika, kunatokana na alivyowatumikia wananchi na vitendo alivyoita vya “kihalifu” vinavyofanywa na CCM dhidi ya wananchi.

“CCM wameuza kila kitu. Wameuza viwanja vya michezo bila kujali mwongozo wa rais unaotaka kulinda viwanja vya michezo. Hivi sasa, Moshi haina hata viwanja vya kufanyia mazoezi,” anasema.

Mbali na kuuza viwanja vya michezo, Ndesamburo anatuhumu CCM kupora sehemu ya katikati ya mji iliyokuwa inatumiwa na wafanyabiashara wadogo, maarufu kama “machinga.”

“Bila kujali athari za uchumi, CCM wameuza eneo la Kibororoni na kuacha wafanyabiashara wote bila eneo la kufanyia shughuli zao,” anasema kwa sauti ya masikitiko.

Anasema uamuzi wa kuuza eneo hilo ambalo limekuwa na soko tangu miaka 50 iliyopita, umeleta umasikini kwa wananchi.

“Nataka wakazi wa Moshi wabadilishe Baraza la Madiwani kwa kuachana na madiwani wa CCM. Hiyo ndiyo njia pekee ya kujikomboa kutoka makucha ya CCM. Vinginevyo, chama hiki kitauza kila kitu na kuwaacha masikini,” anasisitiza.

“Hiki si chama cha siasa. Ni gulio la wahalifu lenye kazi ya kuuza na kubinafsisha. Viongozi wake hawajali hata maisha ya wananchi, bali kila kukicha utasikia, hapa pameuzwa au pamebinafsishwa,” anasema.

Mfano hai anaoutoa Ndesamburo, ni uamuzi wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi ambalo lina madiwani wengi wa CCM.

Kwa kutumia wingi wao, na bila kutumia busara na uzalendo, madiwani wa CCM wamekubali kuipa kampuni ya Tanzania Discovery Heritage (TDH), hati ya kumiliki ardhi ya wananchi iliyopo katika eneo la ardhi ya Uhuru Park.

Kampuni hiyo imepanga kuitumia hati hiyo kuiweka dhamana benki ili ipatiwe mkopo wa Sh. 1.5 bilioni kwa madai ya kuendeleza eneo hilo.

“Katika kikao cha Kamati ya Fedha nilikatalia jambo hili. Nilisema hatuwezi kutoa ardhi ya asili ya wananchi kwa kampuni binafsi,” anaeleza Ndesamburo.

Imeelezwa na baadhi ya madiwani kuwa mjadala ulikuwa mkali na hakuna muafaka wowowte uliofikiwa.

Baada ya madiwani wa CCM kuona suala hilo limeleta mvutano wakaamua kulipeleka katika Baraza la Madiwani ambako kwa wingi wao wangelipitisha.

Ndesamburo anasema baada ya mkutano wa Kamati ya Fedha kumalizika, aliita madiwani wenzake wa Chadema na kuwaeleza kilichotokea katika kikao cha Kamati ya Fedha, na kwamba kwa pamoja walikubaliana kupinga eneo hilo kuuzwa.

Anasema baada ya mkutano wake huo na madiwani wenzake wa Chadema, yeye akaondoka kuja Dar es Salaam kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Bila aibu, CCM wakatumia wingi wao katika baraza la madiwani kupitisha uamuzi huu haramu na usiokubalika. Ndiyo maana tunaposema CCM hawawezi kupambana na ufisadi, tunasema tukiwa na uhakika na hilo,” anaeleza mtunga sheria huyo.

“Ninaposema tayari nimeshinda ubunge, nina maana pana zaidi. Kwamba wananchi wanajua kuwa CCM haina ubavu wa kupambana na ufisadi. Hiki ni chama kinachokumbatia mafisadi,” amesema.

Kampuni ya TDH imeingia mkataba wa miaka kumi na Halmashauri ya Moshi kabla ya mkataba wa awali kumalizika, manispaa imeiongezea kampuni mkataba wa miaka 33.

Tayari uamuzi wa kumuongezea mwekezaji mkataba na kumpa hati ya umiliki ya Uhuru Park kwa ajili ya kuombea mkopo, umeibua zogo na umekumbana na upinzani kutoka kwa wananchi.

Hofu kubwa inatokana na maelezo kwamba iwapo kampuni ya TDH itashindwa kurejesha mkopo wake, italazimisha benki kuuuza ardhi hiyo.

Kuhusu mkakati wa chama chake katika uchaguzi ujao, Ndesamburo anasema yeye na chama chake wamejipanga kushinda, si katika jimbo la Moshi Mjini pekee, bali hadi majimbo mengine yaliyoko mkoa wa Kilimanjaro.

Anasema Chadema imepanga kushinda majimbo takribani saba kati ya tisa yaliyoko Kilimanjaro na kwamba tayari wamepatikana wagombea wenye sifa katika majimbo hayo.

Anasema, “Mbali na Moshi Mjini, ambako mimi tayari nimeshinda hata kabla ya uchaguzi kufanyika, tunataka kushinda Hai, Moshi Vijijini, Siha, Vunjo na Same Mashariki.”

Katika kuhakikisha Chadema inatimiza adhima hiyo, Ndesamburo anasema yeye amepewa jukumu la kusimamia kampeni za mkoa wa Kilimanjaro kwa kunadi wagombea na hata kutafuta wagombea wenye sifa.

“Mimi sitaenda popote. Nitabaki Kilimanjaro na nitatumia helkopta, magari, pikipiki na baiskeli. Katika kutekeleza adhima hii, nimejitolea kupita nyumba hadi nyumba,” anasema.

Tayari Ndesamburo amenunua helikopta mbili ambazo anasema atazitumia kwa ajili ya kampeni za chama chake kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Ndesamburo aliyeandika historia bungeni baada ya kujiondoa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyokuwa ikisikiliza shauri la mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi dhidi ya waziri Adam Malima kwa kile alichodai, “Bunge limehongwa.”

Ndesamburo alituhumu Bunge kushindwa kushughulikia madai yaliyohusisha wajumbe wa Kamati kupokea rushwa katika kesi hiyo.

Ndesamburo ambaye jimboni mwake wafuasi wake humwita “Ndesa-pesa,” kutokana na uwezo wake kifedha, tayari amekuwa bungeni kwa vipindi viwili mfululizo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: