‘Ngonjera’ za Sumatra na usalama baharini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

SIKUONA wala kuonyeshwa nani anakagua vyombo vya usafiri majini ambavyo vinatumiwa na wasafiri wengi kuliko hata wanaosafiri kwa meli.

Kuna mitumbwi iliyofungwa injini na isiyo na injini. Kuna mashua ziendazo kwa nguvu za upepo usukumao tanga. Nani anakagua vyombo hivi na lini?

Selemani Juma Feruzi (60), mvuvi aliyekutwa ufukweni Tanga anasema, “Hatuna vifaa vya kusaidia endapo tutapata tatizo tukiwa baharini. Wakati wa kuvua ndio kama unavyotuona; tunabadili nguo kwa kuingia kazini si kuwa na kifaa maalumu.”

Feruzi anasema hali ya kutokuwa na vifaa kwa ajili ya usalama wao haiko kwake na wenzake pake yao, bali hata katika wilaya zingine mkoani Tanga.

“Kule kuna wavuvi kama sisi. Hawana vifaa vya usalama. Hawana taarifa juu ya hali ya hewa. Hawana maarifa zaidi ya uzoefu wao wa miaka yote baharini. Hawana mbinu mpya za kujikinga,” anaeleza Feruzi.

Mvuvi mwingine, Alawi Said anasema, “Hapa wanakuja watu wa kuchukua ushuru tu baada ya sisi kurudi mwambao, lakini siyo kutupa somo la hali ya hewa au vifaa mbalimbali vya kutusaidia. Sijaona kitu hicho.”

Mkoa wa Tanga una wilaya nane. Mwandishi alitembelea wilaya nne na kujikita mwambao kwenye vyombo vya usafiri wa majini ambavyo hubeba mamia kwa mamia ya wasafiri au wavuvi waendao kazini.

Kwa mfano, wilaya ya Mkinga ina zaidi ya vyombo 100 katika vituo vikuu vya uvuvi vya Monga, Kwale, Vyale, Mchalikani na Mowa. Vyombo wanavyotumiwa ni mitumbwi na mashua.

Wilaya ya Pangani ina vituo vikuu vya uvuvi vya Ushongo, Kipumbwi, Mkwaja na Buyuni. Katika vituo hivi kuna zaidi ya vyombo 150 vya usafiri ambavyo pia ni mashua na mitumbwi.

Tanga Mjini kuna vituo vya wavuvi kama Sahale. Hapa kuna vyombo vipatavyo 200 ambavyo ni mashua na mitumbwi; Mwarongo vipo 50, Deep Sea kuna 50.

Katika wilaya ya Muheza kuna vituo vingi vidogo lakini kikuu ni Kigombe ambako kuna mitumbwi na mashua za uvuvi zipatazo 50.

Maofisa wa Sumatra mkoani Tanga wamemwambia mwandishi huyu kuwa hawajui “mambo mengi” kuhusu usafiri wa mitumbwi na mashua.

Mwandishi alipata taarifa nyingi juu ya vituo na vyombo vya majini kutoka kwa wamiliki wa vyombo, wavuvi na abiria.

Kwa mfano, ofisa wa Sumatra Kapteni Katama, mkoani Tanga anasema, yeye siyo msemaji wa mamlaka, labda nijaribu makao makuu kwa David Mziray (Maneja Mawasiliano, Sumatra).

Nilipofika kwa Mziray, makao makuu ya Sumatra jijini Dar es Salaam, aliniambia kuwa hana idadi ya vyombo vya usafiri majini kwa mkoa wa Tanga.

Alisema anachojua ni taarifa zipi amepeleka mikoani juu ya usalama wa baharini kwa wavuvi na abiria.

Ayub Simbuki, mvuvi wa kituo cha Deep Sea, mjini Tanga anasema kwa sauti ya uchungu na msononeko, “Binti, nakwambia tutaendelea kufa. Tutaendelea kufa kwa kuwa lazima tuingie majini ili tuishi, ingawa hatuna elimu, taarifa wala kinga.”

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)