‘Nibebe nibembeleze JK nibebe’


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

MAMBO mazito. Sasa serikali ya Rais Jakaya Kikwete inakesha ikiimba kibao cha Nibebe kilichotungwa na msanii wa muziki wa injili, Rose Muhando.

Atakayeacha kuimba, katika nchi hiyo inayonyambuka kama tambara bovu, atajikuta benchi. Serikali inarudia sana kibwagizo cha Nibebe, nibebe, nibembeleze nibebe; nibebe, nibebe mikononi mwako niwe salama.

Rose alitunga na kuimba kibao hicho kuonyesha alihitaji neema tu ya Mwenyezi Mungu aweze kuokoka vinginevyo hatafika alipo Yesu Kristo.

Iko wazi, mtu yeyote anayeomba kubebwa, hata kazini tu ina maana hana uwezo au hana sifa – hapo anatumia undugu, rushwa, uswahiba na kulialia – ili apate fadhila ambayo kimsingi hakustahili.

Wee, hata kama umeokoka, ukiacha kuomba tu inakula kwako. Eti hata kama siku zote umeishi ukimtegemea Mungu, ukiasi njia zake siku moja tu, inabidi ukeshe kuomba maghufira.

Serikali ya JK inajua vema hili. Lakini inafurahi kwamba Rose Muhando amerahisishia kazi ya kuomba, kulialia na kutegemea mbeleko. Swali, mbeleko ya nani?

Wakati JK anaimba nibebe mikononi mwako niwe salama yaani mikononi mwa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili aifikishe nchi salama mwaka 2015, mawaziri wake wanaimba nibebe mikononi mwako niwe salama. Ni mikononi mwa JK.

Jamii; asasi za kiraia na vyama vya upinzani wameibua kashfa nyingi za wizi, rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, lakini JK akiona mambo mazito anakimbilia kuita wana-CCM kuomba abebwe.

Bila ya mshikamano huo wa kutetea uhalifu kwa wana-CCM, kashfa ya Richmond ingeivunja serikali ya JK mwaka 2008. Bila ya fungamano la uhalifu, kashfa aliyoiibua aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Lucas Seleli, kwamba serikali ilianza kutumia Bajeti ya mwaka 2009/2010 kabla ya kupitishwa bungeni, ingeiondoa serikali.

CCM walioiingiza serikali hii kwa mtaji wa rushwa sasa hawaoni na hawasikii ndiyo maana wanalinda serikali isiangushwe kwa sababu ya ufisadi uliokubuhu.

Serikali adilifu inawezaje kukaa na wezi kujadiliana nao warejeshe walichoiba? Serikali adilifu inawezaje kuzuia wezi kupitia Kagoda au Meremeta wasishtakiwe? Au chama adilifu kinawezaje kuruhusu waliotoa rushwa kupitishwa kugombea uongozi? Pamoja na uhalifu wote, CCM wameibeba serikali huku wakilia pembeni.

Baada ya kutambua hilo, mawaziri wameona njia pekee ya kujiokoa wakisakamwa ni kujikabidhi mikononi mwa JK – nibebe mikononi mwako JK tuwe salama.

Rose alipoomba kubebwa na Yesu amfikishe mbinguni kwa Baba yake ni kwa vile yeye binafsi ama kashindwa au kakosa au kaishiwa uwezo na nguvu – kapungukiwa imani. Hata mawaziri wa JK wako hivyo.

Wanaimba bwana bila kuchoka. Kama hawaimbi kwa sauti watakuwa wanaimba kwa ala za mdomo au kwa kupiga mluzi tena kwa msisitizo ssnibebe mikononi mwako JK niwe salama.

Kama si kuwabeba Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na naibu wake, Dk. Lucy Nkya, wangepona vipi? Madaktari wenzao wa Muhimbili, Mbeya, Bugando, KCMC, Ilala, Temeke, Kinondoni hawawataki, sasa Mponda na Nkya watafanyaje kazi?

Hatari ya kubebwa ni kwamba mara zote anayebebwa kutokana na uwezo mdogo analazimika kusubiri mbeleko.

Wanaonufaika kwa kuimba nibebe si Mponda na Nkya tu, bali wengine kibao. Inaanzia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Waziri William Ngeleja waliolikoroga katika sakata la kuchangisha na kugawana fedha. Wapo wengi hawa.

0658 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: