‘Njama za mauaji’ zafichuka


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
NAIBU Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS), Jack Zoka

NAIBU Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS), Jack Zoka ametajwa kuwa miongoni mwa wanaopanga mkakati wa kuangamiza wanaodaiwa kuikosoa serikali, MwanaHALISI limeelezwa.

Aidha, ametajwa kuwa mmoja wa waliounda mpango wa kutekwa na kuteswa kwa Dk. Steven Ulimboka ambaye hivi sasa anaendelea na matibabu Afrika Kusini.

Taarifa zilizofikia gazeti hili kutoka vyanzo mbalimbali zinasema, Zoka ni mtuhumiwa Na. 1 katika utekelezaji wa mpango wa siri wa mauaji, utekaji na utesaji ambao umeandaliwa mahususi na kwa watu maalum.

Miongoni mwa wanaotajwa kutaka kuangamizwa, ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibord Slaa, mbunge wa Ubungo kupitia chama hicho, John Mnyika na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), wachapishaji wa MwanaHALISI, Saed Kubenea.

Bali Zoka hakupatikana juzi Jumatatu kutoa kauli yake juu ya tuhuma hizi.

Mwandishi alimwita Zoka tangu saa nane mchana hadi saa 12.55; lakini simu yake iliita bila kupokelewa na wakati mwingine ilijibu kuwa mwenye namba hiyo hapatikani.

Hatimaye mwandishi alipeleka ujumbe kwa Zoka uliosema: “Natumai umzima wa afya. Mimi mhariri wa MwanaHALISI nataka uzungumzie tuhuma za viongozi wakuu wa CHADEMA, kuwa TISS na wewe binafsi, mmepanga kuua baadhi yao. Unasemaje?”

Zoka aliombwa pia kutoa kauli juu ya taarifa katika mitandao, zinazomtaja yeye binafsi kuwa nyuma ya mpango uliofanikisha kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka.

Dk. Ulimboka alipelekwa Afrika Kusini 30 Juni, kwa michango ya madaktari wenzake, watu mbalimbali na kile kilichoelezwa kuwa “msaada mkubwa wa mfanyabiashara mashuhuri nchini, Dk. Reginald Mengi.”

Kwa mujibu wa mawasiliano ya imeili yaliyotumwa na mmoja wa watoa taarifa wa ndani wa Dk. Slaa na Mnyika, mpango wa kuwateketeza watu hao umeandaliwa mahususi ili “kuwatisha katika harakati za kutetea wananchi wanyonge.”

Mtoa taarifa huyo kutoka ndani ya idara ya usalama ameeleza, katika mawasiliano yake ya 27 Juni 2012, kuwa kuna mpango wa kuteketeza maisha ya Dk. Slaa na Mnyika; na kwamba mpango huo unaratibiwa moja kwa moja na Zoka.

“…the information I'm giving you is authentic (taarifa ninazokupa ni sahihi na makini). Tayari kuna timu imetumwa kwenda Dodoma kufuatilia mienendo ya Mnyika kwa maana ya mahali alipofikia, mahali anapopendelea kutembea na kula chakula na marafiki anaokuwa nao mara kwa mara, hasa wanawake kama wapo,” anaeleza mtoa taarifa.

Anasema, “Hii timu inafanya kazi moja kwa moja kwa maelekezo ya Zoka na wamepewa kazi ya kutathmini njia bora ya kumdhuru Mnyika bila kuacha trace (unyayo) yoyote. Katika options (njia za kutumia), kuna kuweka sumu kwenye maji, chakula au (kumpiga) sindano. Kuna matumizi ya ajali au ujambazi.”

Andishi hilo linasema, “Katika ajali, timu hiyo imeelekezwa kuangalia mbinu kama waliyowahi kuijaribu kwa Mwakyembe (Dk. Harrison Mwakyembe mbunge wa Kyela CCM). Hapa kuna vijana wamefundishwa kikamilifu njia hii. Mafunzo yao yaliandaliwa (jina la nchi tunalo) mwishoni mwa mwaka jana.”

Anasema, “Katika sumu wamejiandaa kwa sumu inayoua taratibu. Kama mtakumbuka, katika bunge lililopita, Sitta (Samwel Sitta) aliwahi kudokeza juu ya sumu ya aina hiyo kuingia nchini. Wakati ule sumu ililetwa na kambi ya kina (majina tunayo) na wakati intelligence yetu ilipochunguza na kuijua, wakaona ni silaha nzuri sana kumaliza wapinzani. Sumu hii inapatikana India na baadhi ya nchi zilizokuwa za Kisovieti…”

“Kwenye ujambazi zimeandaliwa approach (njia) mbili; moja ni ya matumizi ya tindikali kama ile aliyofanyiwa Kubenea; na nyingine ni ya matumizi ya ujambazi kama ule aliofanyiwa Dk. Ulimboka.”

Tarehe 5 Januari 2008, Kubenea na mshauri wa habari na mawasiliano, Ndimara Tegambwage walishambuliwa na watu waliotumwa mahususi. Kubenea alimwagiwa tikindikali machoni na Tegambwage alijeruhiwa kwa panga. Hadi sasa, bado Kubenea analazimika kwenda nje ya nchi mara kwa mara kwa matibabu.

Mtoa taarifa anasema, “Hivyo nimethibitishiwa kwamba hii ya Ulimboka iliandaliwa na usalama na si polisi kama baadhi wanavyohisi. Kijana aliyekuwa akisimamia zoezi hili anafahamika kwa jina la Rama ambaye yuko kwenye kurugenzi ya bwana Zoka.”

Rama ambaye mtoa taarifa hakutoa jina lake la pili, ndiye anatajwa kushiriki kumtesa Ulimboka katika moja ya majumba ya kificho na hatimaye kutelekezwa kwenye msitu wa Mabwepande, Bunju, nje ya jiji la Dar es Salaam.

“Wakati wakimtesa Ulimboka, ni Rama aliyekuwa akisisitiza kuelezwa kama Ulimboka ametumwa na CHADEMA na kwamba ni nani hasa katika CHADEMA anayemtumia. Wazo lililopo kwenye usalama ni kuwa Ulimboka anatumiwa na Mnyika pamoja na Dk. Slaa,” anaeleza kigogo huyo wa taarifa za kina.

Gazeti hili halijaweza kupata jina la pili la Rama na kazi anazozifanya TISS.

Zoka ni naibu mkurugenzi wa TISS anayeshughulikia siasa. Huyu ni kiongozi wa idara hiyo anayehudhuria vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC).

Vikao hivi ndivyo hufuatilia kwa karibu, utendaji na shughuli nyingine za chama na mipango yake; na kuagiza jinsi ya kukabiliana na mazingira kinzani kwa chama. Gazeti hili lina nyaraka kadhaa zinazotuhumu baadhi ya watu, likiwamo gazeti hili, kuwa mstari wa mbele “kuanika siri za serikali.”

Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema katika kikao cha CC kilichofanyika Butiama mwaka 2008, “MwanaHALISI limekuwa likiandika kwa ufasaha mazungumzo ya viongozi wakuu wa serikali na CCM.” Akaonya juu ya viongozi kuvujisha taarifa za chama chake.

Kuhusu mpango wa kuangamiza viongozi wa CHADEMA, Dk. Slaa amesema baada ya kupata taarifa hizo alituma wanausalama wake kufuatilia.

“Baada ya uchunguzi ulioshirikisha watu mbalimbali, tulijiridhisha kuwa kuna mpango huo. Tukaamua kuitisha mkutano wa waandishi wa habari jana (Jumapili iliyopita), kueleza umma juu ya jambo hili,” ameeleza Dk. Slaa katika mahojiano yake na gazeti hili juzi Jumatatu.

Awali taarifa zinasema mpango wa kumteka Ulimboka ulilenga kuwatisha madaktari, na kwamba tayari uliandaliwa mkakati wa kutumia baadhi ya magazeti kufanya propaganda kuwa utekeaji huo umeandaliwa na raia walioathirika na mgomo wa madaktari.

Tayari gazeti la Rai linalomilikiwa na Rostam Aziz, swahiba mkuu wa Rais Kikwete, limechapisha makala kwenye ukurasa wa nne ya toleo Na. 980 la Julai 5 - 12 inayolenga kuaminisha umma kuwa Dk. Ulimboka ametekwa na watu walioathirika na mgomo wa madaktari.

Makala hiyo imeandikwa na mwanasiasa na mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Prince Mahinja Bagenda.

Mwanasiasa huyu ambaye sasa ameibukia kwenye uandishi wa habari, ndiye mwandishi wa kitabu kilichopewa jina la “Jakaya Mrisho Kikwete, tumaini lililorejea.” Kitabu hiki kilichapishwa na kusambazwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

MwanaHALISI linaweza kuthibitisha kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa serikali na jeshi la polisi, wameaminishwa kuwa mkakati wa kumteka Dk. Ulimboka ulipangwa na CHADEMA.

Ujumbe wa simu ya kiganjani (sms) ya kiongozi mmoja serikalini, uliotumwa kwa mwananchi mmoja (majina yote tunayo) unasema, “… hii ni hatari sana. Sasa tunaanza kujua kuwa hii ni kazi ya opposition (upinzani) wamejipanga kwa ufundi mkubwa kuiweka serikali na jeshi la polisi pabaya...”

Haikuweza kufahamika mara moja kilichomsukuma mserikali kuihusisha CHADEMA na kilichotokea. Haikujulikana pia iwapo amesukumwa na taarifa zinazodaiwa kupangwa na usalama wa taifa.

Ujumbe ambao mserikali alikuwa akijibu ulikuwa unasema, “Kamanda Msangi aliyemkamata na kumtesa Dk. Ulimboka yupo katika jopo la kuchunguza nini kimemtokezea Dk. Ulimboka. Alipofika kumhoji, Dk. Ulimboka alimwambia ‘nirudishie simu na waleti yangu.’ Kamanda Msangi taratibu akatoka wodini kichwa chini…”

Taarifa zinasema kuwa mkakati wa kutaka kusingizia watu walioathirika na mgomo huo ulipata upinzani mkali kutoka miongoni mwa wapanga mkakati kutokana na baadhi yao kutaka kuihusisha CHADEMA na tukio hilo.

Aidha, mahojiano ya Dk. Ulimboka yanayopatikana kwenye mtandao wa kijamii wa You Tube yaliyofanyika kabla ya kupelekwa Afrika Kusini, 30 Juni 2012, yanaonyesha watekaji wa Dk. Ulimboka ni “watu kutoka serikalini.”

Akiongea kwa shida, Dk. Ulimboka ananukuliwa akisema anamfahamu mtu ambaye alimuita kwenye kikao ambapo muda mfupi baadaye alitekwa; waliwahi kukutana kwenye mgogoro wa madaktari mwanzo na ni mfanyakazi wa ikulu.

“…kwa muda kama siku tatu mfululizo, huyu bwana alikuwa anajaribu kuwasiliana na mimi lakini kwa bahati mbaya ratiba yangu ilikuwa haiwezekani kumwona. Nilishawahi kumwona zamani, kwenye mgogoro ule mwingine, lakini this time of course (mara hii) alikuwa serious (makini) akinitafuta… Huyu bwana anafanya kazi ikulu.

Anasema, “…kwa sababu namfahamu kutokana na incidence (matukio) za kwanza, sikuwa na muda. Lakina jana aka-insist (akang’ang’ania) sana na akakaa Hugo (hoteli) pale muda mrefu sana, sisi tulikuwa tumekaa Leaders Club.”

“Baadaye nikamwambia Deo (Dk. Deogratias Michael) kuna jamaa mmoja, ambaye yeye Deo anamkumbuka sana kwa sababu mara zote huwa tunakwenda naye, anataka kutuona. Basi tukawaacha wenzetu wanafanya kazi nyingine, tukaondoka mimi na Deo around (kama) saa tano na robo (5.15),” anaeleza Dk. Ulimboka katika kanda hiyo iliyosambazwa katika nchi mbalimbali duniani.

Naye akatuarifu kuwa pale Hugo alipokuwa amekaa wanafunga, akawa ameenda kule juu sehemu inaitwa Stereo, akanambia yupo pale. Mimi nikawasha gari hadi pale, nikaangalia meza ya kwanza pale sikumuona. Tulipoingia pale hatukumwona. Nikazunguka sikumwona, nikampigia simu akaniambia nakuja hapo sasa hivi.

“It took like twenty, thirty minutes (ilichukua kama dakila 20 au 30 hivi) tangu aliposema anakuja. Tukaamua kuwasha gari ili kurudi pale Leaders…tukaishia pale Tunisia Road; kuna kontena, tukakaa pale, sasa akawa anapiga simu akisema anakuja kuna vitu anamalizia; tukawa tunawaza ni vitu gani?”

Dk. Ulimboka anasimulia “mtu wa ikulu” alivyoingia kwa gari na kumuuliza iwapo alikuwa na Deo na kwamba walianza majadiliano yaliyohusu hali ya mgomo na jinsi wao walivyokuwa wakiona unaweza kutatuliwa.

“Sisi tukasema mambo yote yanafahamika. Tukaongea naye kwa muda mfupi tu; akawa anaandika… kwa hiyo pia alikuwa very busy communicating, (akionekana kujishughulisha zaidi na mawasiliano ya simu). Unaona?

Taarifa tulizozipata wakati tunakwenda mitamboni zinasema kuwa jeshi la polisi limeelekezwa kuwakamata viongozi wakuu wa CHADEMA kwa kile kilichoelezwa kuwa madai yao ya kutaka kuuawa yanazusha mtafaruku kati ya nchi na wahisani.

Mpango huo ulipangwa kutekelezwa wakati wowote kuanzia jana Jumanne.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)