‘Polisi wa Tulawaka watatumaliza’


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version

POLISI wa kituo cha Mavota kilichopo ndani ya eneo la kijiji cha Mavota, wilayani  Biharamulo, katika mkoa wa Kagera, wanakabiliwa na tuhuma nzito.

Wananchi wanatuhumu polisi kupiga, kunyang’anya fedha na mali na kuua raia katika eneo hili la kijiji ambako pia ndiko kwenye mgodi wa dhahabu wa Tulawaka.

Viongozi wa kijiji, kata ya Kaniha na wananchi wanaoshi na kufanya shughuli zao katika eneo hilo, wanalalamikia polisi kwa ukatili badala ya kutimiza jukumu lao la kulinda mali na usalama wa raia.

Anayelalamikiwa zaidi ni mkuu wa kituo hicho. Gazeti hili lilikutana na mkuu huyo kutaka maelezo juu ya tuhuma hizo.

Sajenti Respicius Eneri ndiye mkuu wa kituo cha Mavota. Aliulizwa iwapo askari wake wanashiriki ukatili na mauaji naye alijibu kwa ufupi:

Kwanza, ndio anafikisha mwezi wa pili tangu afike kituoni pale. Pili, bado anajifunza mazingira. Tatu, “mimi siyo msemaji wa jeshi la polisi,” ameeleza.

Diwani wa kata ya Kaniha (CCM), Edward Mashauri, ambaye ndani ya kata yake ndiko kunafanyika unyang’anyi, anadai polisi wa kituo cha Mavota wamekithiri kwa ukatili kwa wananchi.

Anasema wengi wanaoteswa na kuuawa, ama ni wachimbaji wadogo, wafugaji katika eneo hilo au waendesha pikipiki za kubeba abiria, maarufu kwa jina la “bodaboda.”

Kijiji cha Mavota ni sehemu ya msitu wa hifadhi. Kituo cha polisi kipo kati ya makao makuu ya kijiji na mgodi wa Tulawaka unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Gold Corporation (Barrick).

Ni kilomita tano (5) kutoka makao makuu ya kijiji hadi mgodi wa Barrick – ukipitia mbuga yenye miti na nyasi ndefu.

Mpaka kati ya mgodi wa Tulawaka na kijiji ni wa seng’enge. Uchimbaji dhahabu katika mgodi huu siyo kama ule wa migodi mingine wa kwenda chini sana. Wananchi wanaeleza kuwa hiyo “inatokana na dhahabu kuwa juujuu.”

Lakini dhahabu pia haziko kwenye shimo moja. Eneo lote ndani na nje ya seng’enge linasemekana kuwa na madini haya ya thamani.

Mwaka 1998, wakati Barrick wakifanya utafiti wa madini, waliamuru wanakijiji katika eneo linalopakana na mgodi wa sasa kuwa wasichimbe vyoo zaidi ya futi sita kwenda chini.

“Hii ni kwa kuwa dhahabu ya hapa iko juujuu tu; lakini amri hiyo iliondolewa mwaka 2002,” anaeleza mwenyekiti wa kijiji Daud Donasian.

Katika mazingira haya wananchi wanapata dhahabu ama kwa kuchimba wenyewe katika eneo kati ya kijiji na mgodi, au kwa kuchenjua kutoka mawe yaliyotupwa na mgodi; au kwa uhusiano na waliomo ndani ya ngodi.

Ni wenye dhahabu nje ya mgodi – wanaouza, wanaununua au walioibeba tu – ambao wanadaiwa kukamatwa na polisi, kunyang’anywa mawe yao ya dhahabu, kupigwa na wanaokaidi kuuawa kwa kupigwa risasi.

Diwani Mashauri anaeleza kuwa katika eneo lote la kijiji na hadi kwenye mpaka wa mgodi, “hakuna sehemu iliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hii ni kero ya kwanza kubwa.”

“Hapa kuna tatizo kubwa,” anasema diwani na kuongeza, “Hata kama wananchi wamefanya makosa, hukumu yake haistahili kuwa kifo, tena cha kikatili na kilichoamuliwa na mtu mwingine asiye  mahakama.”

Mashauri anasema ameshapokea taarifa nyingi za wachimbaji wadogo, wafugaji na waendesha pikipiki wakilalamikia vitendo vya polisi wa kituo cha Mavota.

Ukatili mwingine anaotaja Mashauri ni polisi kuwakamata wanaochunga mifugo pembezoni mwa hifadhi, “kuwabambikizia kosa” la kuingiza mifugo kwenye hifadhi na kuwatoza faini ya Sh. 50,000 kwa kila ng’ombe.

“Wafugaji wanakamatwa, wanapigwa, wanatozwa faini na wakishalipa hawapewi hata risiti ya faini waliyotozwa,” anaeleza diwani Mashauri huku akitikisa kichwa kuonyesha masikitiko.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na mwandishi wamekiri kuruhusiwa na polisi kwenda maeneo karibu na mgodi lakini wanaporudi, wanatishiwa, wanapigwa na kunyany’anywa walichonacho.

Mchimbaji mdogo nje ya mgodi aliyejitambulisha kwa jina moja la Pascal, amesema anashangaa serikali kuruhusu kampuni ya nje na kutelekeza mwananchi. “Mbona wachimbaji wadogo na wakubwa sote tunafanya shughuli moja?” anauliza.

Kiongozi wa kijiji ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema “kiongozi wa wilaya” alifanya mkutano kijijini Mavota na kuwaambia polisi kuwa “atakayeua mchimbaji mdogo, atapandishwa cheo au atapelekwa Dar es Salaam kuangalia televisheni.”

“Tangazo hilo alilitolea pale… kwenye mwembe ule pale na kila mtu alisikia. Majibu yake tuliyapata baada ya wiki moja. Hii ni baada ya polisi wawili kufanya mauaji ya watu watatu na kabla hata ya wiki kwisha wakahamishwa wote,” anaeleza mtoa taarifa mbele ya wanakijiji wenzake.

MwanaHALISI lina jina la kiongozi huyo wa wilaya na majina ya askari wawili waliotoa roho za wachimbaji wadogo.

Imeelezwa kuwa kabla ya mauaji hayo, mwaka 2009, polisi waliwanyang’anya vijana hao mawe yao ya dhahabu na walipokwenda kuyadai walipigwa risasi; wawili walikufa palepale na mmoja akafia hospitali.

Mtoa taarifa anasema pamoja na wananchi kushuhudia mauaji hayo, mpelelezi wa kesi hiyo (jina tunalo), alidai kuwa “marehemu walitaka kuchoma moto kituo cha polisi.”

Inaelezwa kuwa, robo tatu ya wafungwa katika gereza la Biharamulo ni wachimbaji wadogo maeneo ya mgodi wa Tulawaka ambao wanatoka kijiji cha Mavota, vijiji jirani na maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa kitongoji na diwani wa Mavota wameeleza kuwa kituo cha polisi cha Mavota kilijengwa na Barrick mwaka 2001.

Kituo kilitarajiwa kuwa kizibo kwa njia ziendazo mgodini na hivyo kuwa msaada mkubwa kwa wachimba dhahabu kutoka Canada.

Baada ya masimulizi mengi ya viongozi na wanakijiji, gazeti lilirudi kwa mkuu wa kituo, Sajenti Respicius Eneri, lakini alishikilia msimamo wake kuwa siyo msemaji na bado anajifunza mazingira,

Alipong’ang’anizwa kuwa hata viongozi wa kijiji wameshafika kituoni kuwalalamikia polisi wake, alijibu kwa mkato kwa kusema, “Unajua, wao ni wanasiasa; sisi tunatekeleza sheria na taratibu za nchi.” Akakata simu.

Kituo cha polisi cha Mavota kina jumla ya askari saba akiwemo mkuu wa kituo.

Afisa uhusiano wa mgodi wa Tulawaka, Bahati Mwambene, anakiri mgodi kupata taarifa za unyanyasaji unaofanywa na polisi.

“Sisi hatukubaliani na harassment (usumbufu); tumeshawaambia waache kuwatesa wananchi, badala yake wafuate taratibu za kisheria,” anaeleza Mwambene kwa sauti ya upole.

Mwendesha pikipiki aliyembeba mwandishi kutoka Runzewe hadi kwenye mgodi – umbali wa kilomita 14 hivi – alistuka pale alipogundua kuwa amebeba mwandishi.

“Sikujua kama wewe ni mwandishi wa habari. Nisingekubali kukuleta huku. Unajua polisi wakitukamata, na kujua kuwa wewe ni mwandishi anayefuatilia mambo yao, tutaangamia,” alieleza.

Tuhuma kubwa tunazotwishwa na polisi ni kwamba sisi wenye pikipiki “…tunabeba majambazi. Lakini wanatuonea, kwani nani atakubali kubeba jambazi kama anamjua?” anauliza kwa mshangao.

Mzee wa miaka 62 anayeishi Runzewe, wilayani Bukombe, analinganisha polisi wa Tulawaka na kokoro.

Anasema, “Wakikukamata hawakubakishii kitu mfukoni. Kila mwendesha pikipiki lazima awe na fedha mfukoni za kuwapa. Hiyo ni kama ada waliyojiwekea.”

Haya ndiyo Sajenti Respicius Eneri anasema hawezi kutolea maelezo kwa kuwa siyo msemaji wa polisi.

<p> 0784 447077 unclejay_jongo@yahoo.com</p>
0
No votes yet