‘Sasa Kikwete atavunja taifa’


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete aliahidi ataongoza vikao vya CCM ili kujivua gamba. Alimaanisha kuondokana na viongozi na wanachama wanaoonekana kuwa mzigo kwa chama. Alionya awali kuwa “tusilaumiane” mbele ya safari.

Wiki iliyopita Kikwete ameongoza vikao vya chama mjini Dodoma, na msamiati ulioongoza vichwa vya habari, siyo kujivua gamba wala kufanya mageuzi ya ndani ya chama (reforms), bali “kuvunja” sekretarieti na kamati kuu ya chama.

Kwa mara nyingine, Rais Kikwete ameweka rekodi ya kuvunja. Alivunja serikali katika kipindi chake cha kwanza, na sasa amevunja Kamati Kuu ya chama anachokiongoza. Haijulikani atavunja nini baada ya hapa, lakini wenye hekima wanadhani atavunja nchi na dalili zipo. Nitaeleza baadaye.

Kuna tofauti ya kufanya mabadiliko (reforms) na kuvunja Kamati Kuu. Kufanya mabadiliko ni zaidi ya kuboresha. Ni kushughulikia suala kwa maudhui na sura yake.

Kilichofanyika ni kubadili sura katika uongozi wa chama huku akijitahidi kutoudhi pande zinazohasimiana lakini safari hii ameshindwa maana amewagusa tuliodhani hawagusiki.

Kuvunja Kamati Kuu ni tendo kubwa. Linahitaji maelezo, kama ndani ya CCM kungekuwa na demokrasia. Lakini kwa kuwa Mwenyekiti wa chama chetu ni karibu sana na “mungu mtu”, haiwezekani hili likapata maelezo ya kutosha.

Walioondolewa katika uongozi wa chama na vyombo vya maamuzi, walifanya kazi chini ya Rais Kikwete na wengine ndio waliomuingiza madarakani. Haiwezekani hawa wakakiharibu chama bila kumshirikisha au bila yeye kuchukua hatua za mapema kunusuru mpasuko.

Demokrasia ndani ya CCM haitoshi ndiyo maana hili limepita na hakuna aliyehoji vya kutosha.

Ni kweli sekretarieti iliyopita ilishindwa kumsaidia mwenyekiti ambaye ni rais. Hili lilionekana mapema na watu walipiga kelele wakaambiwa wana fitna.

Alipovunja serikali mwaka 2008, sekretarieti hiyo ilitakiwa kuwa imemwambia mapema, na kwa kuwa haikumwambia alitakiwa kuiondoa wakati huo.

Katika hali ya kawaida, rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala, anapovunja serikali, alitakiwa kuvunja hata sekretarieti ya chama hicho maana ubovu wa serikali huanzia katika chama kinachoongoza serikali.

Hata baada ya kuvunja serikali, haikutegemewa watu waliosababisha serikali ivunjwe wabaki sehemu ya serikali hiyo, bunge na chama kinachotawala. Ubovu wa kiongozi wa chama aliyeko serikalini au bungeni ni wazi unaathiri hata nafasi yake serikalini na kwenye shughuli za bunge.

Ni tatizo kwa sekretarieti na Kamati Kuu kushindwa kumsaidia mwenyekiti, lakini ni tatizo zaidi kwa mwenyekiti kutoona wala kusikia kuwa sekretarieti haimsaidii. Kuivunja sekretarieti na Kamati Kuu bila kukiri udhaifu wa mwenyekiti, ni kuahirisha matanga yatakayokuja karibuni.

Mtikisiko wa kuvunja serikali wakati ule ulizaa mtikisiko mkubwa ndani ya chama. Uhasama ulishamiri ndani ya chama na ndani ya serikali. Rais alikiri hadharani kuwa imefikia wakati watu hawasalimiani na hawawezi kuacha glasi za maji mezani bila kuhofia kuwekewa sumu.

Mtikisiko katika taasisi baada ya kufanya mabadiliko huwa mkubwa kutegemea kiongozi anayeongoza mabadiliko hayo. Imemchukua rais na mwenyekiti wetu, karibu miaka mitatu kuvunja chama, baada ya kuwa amevunja serikali.

Mtikisiko wa kuvunja serikali mwaka 2008, ndio umeendelea mpaka kuvunja chama (Kamati Kuu na Sekretarieti). Ni wazi kuwa mtikisiko huu wa sasa unaweza kuvunja nchi; dalili zipo.

Mjadala wa sasa kuhusu katiba ni dalili za awali. Ni wazi kuwa walioandaa muswada huu, iwe kwa kujitolea au kuagizwa na rais mwenyewe, wamemuhujumu rais kwa kujua au kutojua.

Sehemu moja ya Muungano imetengwa na muswada huu mbovu ambao Mzanzibari na muasisi wa Muungano amediriki kuuita “utumbo”.

Muswada huu unaua muungano na kuendeleza udikiteta wa taasisi ya urais ambayo, kama muswada huu utapitishwa, taasisi hiyo itaitwa ni “ufalme”.

Muswada unaopendekezwa na Rais Kikwete unavunja nchi chini ya utawala wa Rais Kikwete mwenyewe. Na kwa kuwa chama tawala ni legelege kwa sasa, hakuna njia nyingine ya kuepusha kuvunjika kwa nchi, kwa sababu hakuna bima ya kuzuia hilo, ikiwa chama kimeachwa hoi na ufisadi pamoja na uongozi legelege.

Dalili za kuvunja nchi katika utawala wa Kikwete zilianza pale Wazanzibari walipomweka kiti moto Waziri Mkuu Pinda kuhusu hadhi ya Zanzibar katika Muungano.

Tangu hapo mambo yalienda kasi mpaka Zanzibar ilipofanya marekebisho ya 10 ya katiba yanayotamka wazi kuwa Zanzibar ni dola kamili yenye alama zote za dola.

Marekebisho hayo ya katiba ya Zanzibar yamemuweka Rais Kikwete mahali pagumu. Hivi punde atalazimika kukubali kupigiwa mizinga 21 atakapotembelea Zanzibar; na Rais Ali Mohammed Shein atakagua gwaride la Muungano hapa Tanzania Bara.

Haya yote ni kuvunja nchi, lakini kwa bahati mbaya hayawaamshi Watanganyika kuunda nchi yao iliyomezwa.

Dalili nyingine za kuvunja nchi ziko hadharani – zikiwa na rangi ya dini –  tangu dini fulani kudaiwa kupendelewa na nyingine kuonewa, hadi serikali kutenga fungu la dharula la kuhudumia “dini mpya ya Babu wa Loliondo.”

Kama serikali yetu ilikataa kuwa haina dini, kwa sasa haiwezi kufanya hivyo maana Babu Mwasapile atawaumbua wote, tangu rais, waziri mkuu, jamaa zao, majaji na hata viongozi wa majeshi.

Kwa kuwa sasa ni wazi Rais Kikwete anajua kuvunjavunja vitu, kama Rais Mkapa alivyokuwa fundi wa kuuzauza vitu, tutarajie nini kubwa kutoka kwa rais anayevunjavunja.

Hatuliombei, lakini laja.Taifa letu litavunjwa vipandevipande.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: