‘Serikali inasubiri tufe, wachukue fedha zetu’


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
  • Ushahidi wa adha katikati ya utajiri wa dhahabu
  • Mapunjo ya fidia yafichwa kwa mkuu wa wilaya

HAMIS Charles amechanganyikiwa. Anaongea peke yake barabarani. Hata akimuona asiyemjua, anaomba amnunulie chakula.

Kuna masimulizi marefu katika kijiji cha Nyamalembo, kitongoji cha Mine (mgodi) Mpya, wilayani Geita mkoani Mwanza kuhusu Charles (47).

Faustin Barnabas anasema, kama wengine kijijini wanavyosema, kuwa “…amerukwa na akili.” Kwa nini? Maelezo ni kuwa aliporwa shamba na nyumba.

Kwa muda wa miaka mitatu na nusu sasa Charles na wenzake 85 wanaishi kwenye mahema baada ya kuswagwa na wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mines (GGM) – kwa msaada wa serikali – kutoka makazi yao ya asili katika kijiji cha Nyamalembo ili kupisha uchimbaji madini.

Mwili wa Charles umenyauka. Analala chini katika hema. Hapati mlo wa kumshibisha wala kumpa kinga ya mwili; kwa muda mrefu sasa amekuwa akilala chini katika hema. Analaani GGM na serikali.

Ni maisha haya yaliyopelekea kudhoofika mwili na akili. Mkewe, Teddy Maganga (35) na watoto wake watatu, wamekimbilia kusikojulikana. Charles anathibitisha hilo.

Nilipokutana na Charles wiki iliyopita mjini Geita, akiwa anabembelezwa kutoka barabarani, alikokuwa amekaa, ili asigongwe na magari alinieleza haraka, “Mimi ninashangaa kwanini sifi.”

Mwandishi: Kwanini unakaa barabarani?

Charles: (Kimya)

Super Jonaa Said (aliyekuwa anambembeleza atoke barabarani): Huyu bwana amechanganyikiwa. Hata haelewi anachokifanya.

Charles: Acha uwongo! Mimi sijachanganyikiwa. Nimemwambia sijala toka juzi, akaninunulie chipsi lakini hataki; na mimi sitaki kutoka barabarani. Bora nife! Na wewe (akimwangalia mwandishi), kwakuwa umenisemesha utaninunulia chipsi?

Kabla mwandishi hajajibu, alitoa kamera kwenye mkoba. Akampiga picha.

Charles: Unanipiga picha? Dau limeongezeka. Lazima uninunulie chipsi na soda.

Mwandishi: Toka barabarani basi twende nikununulie hizo chipsi.

Charles: Hapo sawa (anatoka barabarani).

Charles, Said na mwandishi wakaongozana hadi banda ambako walikuwa wakiuza chipsi;  sehemu maarufu inayoitwa Lunguya, pembeni mwa MS Hotel. Mwandishi alinunua chipsi.

Wakati Charles anakula, Said alinieleza kuwa Charles ni miongoni mwa wananchi 86 walioswagwa kwa mabavu kutoka makazi yao ya asili ili “kupisha wenye fedha na nguvu.”
 
“Huyu bwana amechanganyikiwa siku za hivi karibuni kutokana na maisha magumu katika mahema na kupotea kwa matarajio yake,” alieleza Saidi.

Mara Charles alidakia, “Usituite wananchi, sisi sio wananchi, sisi ni wakimbizi. Walio katika nchi yao hawawezi kuishi kwenye mahema kwa zaidi ya miaka mitatu hata kama kwa majanga ya asili kama mafuriko.”

Huku akimtolea macho Said, alisema “Hebu mpeleke pale tunapoishi kwenye mahema akajionee tunavyoteseka; kipindi cha mvua tunaoga kila siku. Maisha ya kwenye mahema yamefanya mke wangu na watoto wanikimbie,” anasema Charles huku akiinama.

Mwandishi: Nimesikia wakisema mkeo na watoto wamekukimbia?

Charles: Usinikumbushe machungu. Unafikiri mwanamke kijana anaweza kuishi kwenye hema kwa muda wote huu? Sisi tunaoishi pale tunasubiri kufa tu.

Super Jonaa Saidi ni katibu wa umoja wa familia 86 zilizotimuliwa kwa nguvu kwenye makazi yake ili kutoa nafasi kwa upanuzi wa shughuli za GGM.

Waliishi chini ya miti kwa zaidi ya miezi sita kabla viongozi wa madhehebu ya kikristo ya  African Inland (AIC) kuwafadhili mahema ambayo sasa yametoboka matundu – likiwaka wanaungua, ikinyesha wanalowa.

Said anasema Januari mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima aliwaahidi kuwa serikali itawajengea nyumba; lakini mpaka Januari ya mwaka huu hawajajengewa chochote; Malima hajarudi na karibu wote hawajapata fidia.

Taarifa za Novemba mwaka jana zilisema halmashauri ya wilaya imepata viwanja kwa ujenzi wa nyumba za waathirika, lakini ikakiri kuwa serikali kuu ilikuwa haijaonyesha “dalili zozote” za kumaliza adha hii.

“Nadhani serikali inasubiri wote tufe. Mpaka sasa wenzetu wanne wameshakufa na wengine hatujui watoto wao wamekimbilia wapi,” anasema Said.

Miongoni mwa waliokufa hadi sasa ni pamoja na Ezekiel Kingu aliyefariki mwaka 2008. Mke wake na watoto watano wanadaiwa kwenda kuishi Igunga, Tabora.

Christopher Matuturu (68) ameacha mke aitwaye Ana Christopher (50) na watoto wawili – Innocent (17) na Domina (13).

Aliyekuwa mwenyekiti wa waathirika hao, Bartazal Emmanuel naye amefariki akiwa na miaka 52 na kuacha mke na watoto wawili.

Akisimulia kwa uchungu, mke wa marehemu Bartazal, Veneranda Thomas (45) anasema, “Nakumbuka ilikuwa tarehe 12 Juni, 2010 mume wangu aliponiachia kidonda kisichoweza kupona. Alifariki kwa ugonjwa wa kuharisha na kutapika damu.”

“Ameniacha na watoto wawili, Deus (15) na Alex (13), lakini wote wameshindwa kuishi hapa kwenye mahema, wanarandaranda huko mitaani,” anasimulia.

Gazeti hili lilisharipoti kwa kina mkasa wa wananchi hawa hapo Machi mwaka jana. Mahema yaliyoanza kuchakaa ambamo wanaishi, yako kilometa nne kutoka geti la mgodi wa dhahabu wa GGM.
 
Malalamiko dhidi ya GGM yameenea katika vijiji vya Kalangalala, Nyakabale, Nyamalembo, Mgusu, Salagulwa na Mpovu vilivyoko karibu na mgodi huu unaoendeshwa na kampuni ya AngloGold Ashanti ya Afrika Kusini.

Wakazi wote 23 wa kitongoji cha Katoma waliokwenda mahakamani kudai haki yao kutokana na mashamba na nyumba zao kuchukuliwa na mgodi wamelipwa kwa “kukomolewa.”
 
Timu ya uthamini ikiongozwa na mthamini Juma Mkuki, ilikuwa na wajumbe wafuatao: Mwenyekiti wa kitongoji John Kigundu, Afisa Mtendaji wa kijiji, Samson L. Muhondwa, mwakilishi wa Afisa Ardhi wa wilaya, Lucas N. Malulu, mwakilishi wa Afisa kilimo wa wilaya, Swai J. Benny, mwenyekiti wa kijiji, Peter W. Chipaka na mwakilishi wa Mgodi, Denis Mihayo.

Mali na mazao mengine yaliyothaminiwa ni pamoja na magimbi, nanasi, migomba, grevelia, mizambarao, miti yote ya matunda, vanilla, miti ya mninga, mibuni, soya, sungwi, nyonyo, milonge, michikichi, minazi, miboyo, mibono, misindano, cocoa mininga na nyumba.

Kinachoshangaza na kusikitisha wengi ni kwamba mali zilizohesabiwa siyo zilizofidiwa. Kwa mfano, katika shamba la Charles Fikiri Toyi, migomba iliyokua (iliyozaa au inayokaribia kuzaa) ilikuwa 1,770, lakini iliyoonyeshwa kufidiwa ni 151. Hii ina maana kwamba migomba 1,619 iliondolewa kwenye hesabu.

Miembe iliyokua kwa asilimia miamoja na kuthaminiwa na kuandikwa kwenye fomu ya uthamini ilikuwa 39, lakini katika fomu yake ya malipo imeandikwa miwili (2) tu. Mapunjo hayo yako kwenye karibu kila zao lililoorodheshwa.

Pamoja na kupunguziwa mazao, fomu yake ilionyesha kuwa anatakiwa kulipwa Sh. 43,454,222.44. Lakini amelipwa Sh. 32,138,024.06. Jumla ya Sh. 11,407,198.38 hazijulikani zilikopotelea.

Malipo kwa Charles Toyi, yalifanyika tarehe 13 Julai 2010 kupitia benki ya NBC tawi la Geita kwa hundi Na. 015225.  

Mfano mwingine ni alichofanyiwa Super Jonaa Said. Timu ya uthamini ilijaza kwenye fomu zake migomba 4,565 iliyokua. Aliporudishiwa fomu kwa ajili ya malipo, ilikuwa imeandikwa migomba 277. Migomba 4,288 iliondolewa kwenye orodha.

Mibuni ilikuwa 1,438, lakini ilipunguzwa mpaka kufikia 262. Miche 180 ya nanasi ilipunguzwa hadi 74. Miparachichi 170 ilipunguzwa hadi 40. Mapunjo hayo yalifanywa kwa mazao mengine pia katika shamba lake.

Pamoja na mazao kupunguzwa, kutokana na hesabu zilizopo kwenye fomu yake ya malipo alitakiwa alipwe Sh. 83,757,947.56 Kitu cha kushangaza ni kwamba alikabidhiwa hundi ya Sh. 58,983,633.22. Hii ni pungufu kwa Sh. 24,774,314.34. Hakupewa maelezo yoyote.

Malipo haya yalifanyika tarehe 13 Julai 2010 kupitia benki ya NBC tawi la Geita kwa hundi Na. 015226.

Jackson Manyelo, mmoja wa waathirika anasema wamepanga kuuandikia barua uongozi wa mgodi na kuwapa muda; na kama muda watakaotoa hawatakuwa wamelipa haki zao, watarudi kwenye mashamba yao ili kuyaendeleza.

“Nakuhakikishia, kama hatutalipwa tutarudi kwenye mashamba yetu. Hizi ni haki zetu. Bora tufe kuliko kudhulumiwa nguvu zetu tukiwa tunaona,” anasema Manyero.

Manyero alilipwa Sh. 45,709,484.20 badala ya Sh. 64,616,100.40 zilizojazwa kwenye fomu; kukiwa na pungufu ya Sh. 18,906,616.20. Anasema, “Kinachokera ni kwamba hawatwambii zilizokatwa ni za nini na zinapelekwa wapi.”

Taarifa zinazothibitisha makato ya mamilioni ya shilingi yasiyo na maelezo kwenye fidia za wananchi, zinadaiwa kufichwa ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Geita.

MwanaHALISI limefanikiwa kuona majedwali yanayohusiana na malipo. Jedwali la kwanza ni la takwimu za awali lenye kuonyesha mali na gharama zake za asili. Jedwali la pili ni lenye kuonyesha jinsi mali na, au mazao yalivyopunguzwa na thamani mpya ambao wananchi wanalalamikia.

Mwandishi amepekua na kusoma lundo zima la majedwali yanayohusu wananchi 23 ambao wamelipwa lakini wanalalamika kwa kupunjwa na kunyimwa maelezo.

Ukimya wa serikali katika hili, kuanzia ngazi ya kata hadi taifa, siyo tu unaweza kuleta maafa, hasa baada ya baadhi ya wananchi kujiapiza kurudi walikong’olewa, bali pia baadhi yao kufa kabla hawajapewa haki yao.

0
No votes yet