‘Sijatumia robo ya elimu yangu’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

MZAMIAJI Ahmed Khamis anasema serikali ndiyo ilimsomesha hadi Uingereza; kujifunzia uzamiaji, lakini hajatumia hata robo ya elimu hiyo kwa nchi yake.

Anasema hata katika umri huu (66), akiitwa kufundisha “vijana wetu, sitakawia kukubali.”

Ahmed Khamis, maarufu kwa jina la Kipande, anajitaja kuwa mtaalamu wa shughuli za uzamiaji na uokoaji baharini.

Mzaliwa wa kijiji cha Kiembesamaki, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Kipande anasema amekuwa mzamiaji kwa miaka 34 wakati anastaafu kazi mwaka 2006.

“Ujuzi nilionao haujatumika. Kwa Zanzibar nzima ni mimi tu niliye na elimu hii; lakini bahati mbaya hawataki kunitumia,” anaeleza.

Hamu ya Kipande ni kupata chuo cha kufundishia vijana wanaotaka kubobea katika fani ya uzamiaji na uokoaji.

Akirejea  ajali ya m.v. Spice Islander I na ajali nyingine majini, Kipande anasema serikali inapaswa kufanya maandalizi ya kutoa huduma za dharura pindi ajali inapotokea.

“Ni jukumu la serikali kuokoa watu, vyombo vya usafiri na kulinda bahari dhidi ya uchafuzi,” anaeleza.

Katika mahojiano na MwanaHALISI hivi karibuni, Kipande anajielekeza katika sekta ya utalii inayokua mwaka hadi mwaka.

Anauliza, “Tuseme ndege ya watalii 500 imeangukia baharini, tutafanyaje kusaidia abiria na wafanyakazi wa ndani ya ndege hiyo?”

Ni hapo anapogusia umuhimu wa kuwepo wataalam kama yeye, zana za kazi na chumba cha kisasa cha kuhifadhia maiti.

Mochwari pekee iliyopo Zanzibar ni katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, ambayo uwezo wake ni wa kuhifadhi maiti zisizozidi 30 kwa wakati. Anasema iko haja ya kujenga mochwari kubwa.

Kipande alihitimu mafunzo ya ngazi ya juu ya uzamiaji na uokoaji katika chuo cha Royal Navy kilichopo mji wa Portsmouth, nchini Uingereza kati ya 1976 na 1978.

Anajigamba kufuzu mafunzo kwa kiwango cha kimataifa hadi Waingereza kumpa fursa ya “kuishi nchini humo kwa muda atakao.” Anasema hakukubali.

Kipande anasema mbali na kuzamia na kuokoa watu, amesomea kutambua na kuondosha mabomu yaliyotegwa baharini.

Anasema fani yake inahitaji kijana aliyehitimu vizuri masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati, masomo ambayo alifanya vizuri alipohitimu kidato cha nne mwaka 1970 shule ya sekondari ya Gamal Abdel Nasser.

“Ninazeeka na ujuzi wangu. Laiti ningepata pa kuuwekeza kwa vizazi vijavyo,” anasema kwa sauti ya kulalamika.

0
No votes yet