‘Sitta, Mwakyembe watoswe’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version
Ni kwa ‘usaliti mkuu’ ndani ya CCM
Lowassa, Rostam, Chenge nao wafukuzwe
Dk. Harrison Mwakyembe

TUHUMA za kukisaliti chama zinazowakabili spika wa zamani wa Bunge, Samwel Sitta na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, zaweza kuwafukuzisha kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.

Sitta, ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki na Dk. Mwakyembe wametajwa kuhusika na uanzishaji Chama cha Jamii (CCJ) wakiwa bado wanachama na viongozi katika CCM.

Aliyekuwa wa kwanza kutaja majina ya viongozi hao ni Fred Mpendazoe aliyekuwa mbunge wa Kishapu. Alihama CCM Aprili mwaka jana akituhumu chama hicho kukumbatia mafisadi na kupoteza mwelekeo.

Mpendazoe aliuambia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Njombe wiki iliyopita kuwa yeye, Sitta na Mwakyembe ndio walianzisha CCJ; bali yeye alitangulia kutoka CCM ili kurahisisha usajili wa chama hicho. Wenzake walikuwa wamfuate baadaye.

Wengine ambao Mpendazoe alitaja kuwa waanzilishi wa CCJ ni Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye. Alisema walianzisha chama hicho ili kipokee wanachama waliokuwa wanapinga ufisadi ndani ya  CCM na ambao ingekuwa vigumu kwao kupitishwa kugombea ubunge.

Tuhuma kubwa zinazowakabili Sitta, Mwakyembe na wenzao ni utovu wa uaminifu na usaliti kwa kuanzisha chama ndani ya chama.

Wakati hao wametajwa hivi karibuni, Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge tayari wamethibitishwa na vikao kuwa wamedhoofisha chama chao mbele ya jamii na kusababisha kisifanye vema katika uchaguzi mkuu uliopita.

Dk. Hassy Kitine, mmoja wa makada wa CCM anasema, tuhuma za kuanzisha chama ndani ya chama ni kubwa na kwamba iwapo CCM inataka kuaminika mbele ya wananchi, sharti ifanyie kazi tuhuma hizo.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano ambayo yatachapishwa kwa ukamilifu katika toleo lijalo, Dk. Hassy Kitine amekitaka chama chake kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ushahidi wa tuhuma zote zinazowakabili viongozi wake.

“Kuhusu hili la hawa walioanzisha chama ndani ya chama; na wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ni lazima chama chetu kitafute ushahidi wa kutosha na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika kufuatana na katiba na taratibu za chama,” ameeleza.

Dk. Kitine ambaye aliwahi kuwa waziri wa utawala bora wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, mkurugenzi wa usalama wa taifa, mbunge na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, anasema kuanzisha chama ndani ya chama ni kosa ambalo haliwezi kuachwa bila kutolewa maelezo.

“CCM isifanye parapara. Pamoja na kwamba kumfukuza mtu ndani ya chama ni hatua kubwa. Lakini utafutwe ushahidi; ikithibitika kwamba hawa watu walishiriki katika kuazishwa kwa chama wakiwa bado ndani ya CCM, basi wawajibishwe,” ameeleza.

Anasema, “Ushahidi huu lazima ueleze ushiriki wa kila mmoja. Ukipatika wote wafukuzwe.”

Anasema CCM hakiwezi kuwafukuza watuhumiwa wa ufisadi kikawaacha wanaotuhumiwa kukidhoofisha kwa kuanzisha chama ndani ya chama.

“Wote washughulikiwe kwa mujibu wa taratibu za chama chetu. Wapewe nafasi ya kujitetea. Umma uridhike kwamba haki imetendeka na wao wajiridhishe kuwa wametendewa haki. Kisha chama kiamue kufanya maamuzi magumu ya kuwafukuza,” ameeleza.

Anasema, “Na hili ni kwa wote, wakiwemo wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi. Hapo ndipo chama chetu kitakapolinda hadhi na heshima yake mbele ya wanachama na wananchi wengine kwa jumla.”

Kauli ya kutaka kufukuzwa waasisi wa chama ndani ya chama imekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Nape Nnauye ni miongoni mwa waazilishi wa Chama Cha Jamii (CCJ).

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa walitafsiri hatua ya akina Sitta kuwa ni kumweka Rais Kikwete katika wakati mgumu wa vyama viwili vya siasa katika utawala mmoja, mithili ya serikali shirikishi ya umoja wa kitaifa.

Sitta ni Waziri wa Afrika Mashariki na Mwakyembe ni naibu waziri wa ujenzi; naye Nape ni msemaji wa CCM. Wengine waliotajwa katika CCJ ni Daniel ole Porokwa, katibu msaidizi wa CCM wilaya ya Moshi Mjini na Victor Mwambalaswa, mbunge wa Lupa.        

Jumapili iliyopita, Porokwa aliweka wazi ushiriki wake katika kuasisi CCJ na kushindilia akina Sitta kuwa walikuwa pamoja naye.

Katika tamko lake la kurasa nne kwa waandishi wa habari, Porokwa amesema CCJ ni chama kilichoanzishwa na kuasisiwa na Nape, Sitta, Dk. Mwakyembe na Mpendazoe.

Katika taarifa inayoonyesha kuugama, Porokwa anasema, “Nimeamua kuyasema haya ili kuondoa unafiki unaojengeka ndani ya chama chetu na taifa kwa jumla, kwamba kuna kikundi cha watu wanaotaka kupotosha umma juu ya uanzishwaji wa CCJ na ujio wake.

“Nikiwa kada wa CCM niliyefundishwa na kuaminishwa kuwa uongozi ni dhamana na ninayeamini katika misingi aliyotuachia Baba wa Taifa,  Mwalimu Nyerere, nimeamua kuyasema haya ili ukweli ubaki ukweli katika historia ya taifa letu,” alisema Porokwa.

Porokwa anasema, “Kuyumba kwa chama chetu na hata kufikia hatua ya kuanza kuporomoka kwa kupoteza nafasi mbalimbali kwa vyama vingine kwa wingi tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi katika nchi hii, ni kwa sababu ya kuwa na viongozi wenye malengo na ajenda binafsi, tofauti na zile za chama chenyewe.”

Amemtaka Rais Kikwete kulitazama suala hilo kwa undani kwa kile alichodai “…katika timu yake, kuna wachezaji ambao wako tayari kujifunga na kuinyima timu yao ushindi.”

Anasema, “Ni maoni yangu kwa dhati kabisa na rai yangu kwa viongozi wa chama changu, kwamba ni wakati mwafaka sasa umefika kwa watu kama hawa wawajibike au wawajibishwe kutokana na matendo yao.”

Porokwa ambaye amejitambulisha kwa maneno na vitendo kuwa ni kutoka kundi la Edward Lowassa anasema, mbali na kusukumwa na mapenzi ya chama chake katika kutoa ushuhuda huo, ushahidi anaoutoa unalenga kuonyesha kuwa Sitta, Dk. Mwakyembe na Nape, ni     wasaliti.

“Hawa ninaowataja, si wasaliti kwangu tu, bali hata kwa chama chenyewe. Nisingeshutuka mapema yangenipata yaliyompata Mpendazoe…,” anaeleza.

Anasema, “Na hili la Mpendazoe ambaye alikuwa mbunge, akaacha mishahara kadhaa na mafao yake kwa makubaliano ya kazi ya pamoja ambayo nilishirikishwa katika hatua za awali na mwisho wake wakamtosa na sasa wanamkana hadharani, ni moja ya sababu iliyonisukuma sana kutoa ushuhuda huu.”

Naye mjumbe wa NEC na mwenyekiti wa baraza la wadhamini la CCM, Peter Kisumo pamoja na kutoingia kwa undani kuzungumzia suala hilo amesema, “Wanaotajwa kuanzisha CCJ, zamu yao ikifika watashughulikiwa.”

Hata hivyo, Kisumo amesema suala la kuanzishwa kwa CCJ linaweza kuonekana halina maana yoyote kwa sasa, lakini sharti uchunguzi ufanyike na wanaohusika wachukuliwe hatua.

Mchambuzi maalum wa gazeti hili, Kondo Tutindaga ananukuu Nyerere akishupalia baadhi ya wana-CCM waliounga mkono hoja ya kuunda Tanganyika pale walipochukua fomu kugombea urais mwaka 1995.

Anamnukuu Nyerere akisema mwaka 1995 walikuwa wanatafuta rais wa Tanzania na siyo Tanganyika; na kwamba wanaotaka urais wa Tanganyika wasubiri.

“Ni kwa msingi uleule…Kikwete aweza kuwaambia waanzilishi wa CCJ walio ndani ya CCM, kuwa waondoke wakaunde CCJ ili iwe rahisi kwao kutekeleza madhumuni yao. Hata kama chama si mama, lakini pia chama si koti la kuvaa na kuvua kila unapohisi kero ya joto au baridi,” anaeleza mchambuzi huyo.

Kwa kuwa sasa ni dhahiri CCJ ilianzishwa na wana-CCM waliokerwa na sera za CCM, pamoja na kiongozi wake, yaani Rais Kikwete, sisi tulio wana-CCM msimamo, tuna mashaka na viongozi wa namna hii.

Walioanzisha CCJ, mwandishi anasema, “…si wanachama wa kawaida, bali viongozi waandamizi ndani ya CCM. Usaliti wa namna hii, siku moja utazaa uhaini.”

0
Your rating: None Average: 2.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: