‘Tulikosea kumpa Kikwete madaraka yote’


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

WACHAMBUZI wa siasa nchini wamekuwa wakisema siku za karibuni kuwa Rais Jakaya Kikwete yuko njiapanda na anakabiliwa na kazi nzito ya kufanya maamuzi magumu ndani ya chama na serikali anayoiongoza.

Ukiwasikiliza kwa makini na kwa muda mrefu, unapata picha kuwa jukumu la kuongoza taifa limekabidhiwa mikononi mwa mtu mmoja aitwaye Kikwete.

Kwa maoni yangu ya haraka, mtizamo huu una kasoro nyingi zinazohitaji kurekebishwa kabla mambo hayajaharibika. Kuongoza chama na serikali ni jukumu la pamoja. Ndani ya chama na ndani ya serikali vipo vyombo vinavyotakiwa kufanya kazi hiyo na kuimiliki.

Kinachoelekea kutokea katika mkanganyiko wa sasa, ni kuwa Rais Kikwete alitaka sana kuongoza na akapewa na kuachiwa kila kitu. Ni kosa kwake binafsi kukubali kupokea mustakabali wa taifa; na ni kosa kwa vyombo husika kusalimisha jukumu la kuongoza taifa mikononi mwa mtu mmoja; na ama marafiki zake au familia yake.

Tujadili. Katika maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Kikwete aliahidi kufanya mabadiliko makubwa ndani ya chama ili kukirejeshea hadhi. Ahadi hiyo ilipokelewa kwa maoni tofauti na wana-CCM.

Pamoja na utamu wake, ahadi ya Kikwete inaonekana itashindikana kutekelezwa na uongozi wa sasa wa chama chake kwa sababu, uongozi huu haukurithi hali hii bali umeijenga wenyewe na kuifanya ikue na kufikia hapa ilipo.

Katika hali ya kawaida, uongozi uliosababisha hali mbaya hauwezi kamwe kuibadili kwa sababu unanufaika na hali hiyo mbaya. Hii ni kusema, yanahitajika mapinduzi makubwa ndani ya chama na tulio wengi, hatudhani Kikwete alikusudia kufanya mapinduzi ndani ya CCM.

Kimsingi CCM kimeliongoza taifa hili kwa takribani miaka 50 –  ukijumlisha na miaka ile ya Tanganyika National African Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP). Ni chama kikongwe kinachoonekana kupoteza mwelekeo kwa sababu kimepitiliza malengo yake.

Mathalani, ni chama kinachodai kuongoza mapinduzi ya fikra na matendo halisi katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi, wakati kiuhalisia ni chama kinachosifika kwa uhafidhina wa fikra.

Mnyukano wa sasa ndani ya chama ni matokeo ya hali hii, kwa sababu kizazi kipya cha vijana hakikubaliani na tabaka la wazee wanaodai kutunza historia ya CCM huku wakinufaika binafsi na msimamo huo.

Mpaka hapa, CCM inajikuta iko njiapanda: Ama kubaki chama chenye nadharia safi isiyoendana na matendo yake, au chama kinachotengeneza nadharia yake kutokana na matendo yake.

Mgongano ndani ya CCM, kati ya nadharia na vitendo, ni chimbuko la makundi ya sasa ndani yake. Nadharia inakataza rushwa wakati matendo ya chama yamekithiri kwa rushwa. Imefika mahali, mtu ukisimama hadharani kupinga rushwa au ufisadi, unaonekana ni mpinzani wa CCM.

Udugu huu kati ya rushwa na CCM umeporomosha kwa kasi, heshima ya chama mbele ya jamii na hasa miongoni mwa vijana. Anahitajika kiongozi jasiri, mwadilifu na anayethubutu ili kuongoza harakati za kuiondoa CCM katika njiapanda hii.

Njiapanda nyingine ni nasaba kati ya chama na serikali iliyo madarakani. Nasaba hii inakifanya chama chetu kuwa chama dola. Makada wengi wa CCM wanafurahia hali hii kwa sababu wananufaika nayo.

Kupitia njia hii, makada hupata posho na “heshima kubwa” kwa kuonekana wako karibu na serikali. Baadhi yao hupata hata kinga zisizoandikwa katika utendaji wao wa kila siku.

Nimeshuhudia kwa macho yangu, kamanda wa polisi wa mkoa mmoja akitetemeka kwa hofu kuu kufanya uamuzi wa kumkamata mwenyekiti wa chama wa kata iliyo makao makuu ya mkoa wake, ambaye anatuhumiwa kwa “mauaji ya kutisha.”

Hii ni kuonyesha kuwa viongozi wa chama tawala wana kinga isiyoandikwa. Ni rahisi sana siku hizi kuona lori lenye shehena ya magendo likipeperusha bendera ya CCM na askari wakiogopa kulisimamisha.

Ni rahisi kumwona katibu wa CCM wa wilaya akimuagiza hakimu wa mahakama ya mwanzo au wilaya kufanya jambo linalokwenda kinyume na utaratibu na misingi ya kisheria, naye akatekeleza aliloagizwa.

Kwa mantiki hii, ile dhana ya chama kuisimamia serikali, inabadilika na kuwa chama kuongoza nchi sambamba na serikali. Mshikamano huu unanufaisha viongozi binafsi na si kwa manufaa ya chama.

Mapenzi ya watu kwa chama hupungua wakati mapenzi ya viongozi kwa chama huongezeka, kwa sababu uongozi wa chama huwa si mzigo tena bali baraka na utukufu. Kwa tabia yake, chama dola kinakuwa mbali sana na wananchi wa kawaida isipokuwa wakati wa uchaguzi.

Kwa mfano, hivi sasa kuna ukali wa maisha katika taifa, vyama vingine vya siasa vinazungumzia hali hii na hata kufanya maandamano, mikutano ya hadhara na kutoa matamko, lakini chama chetu – CCM - kiko kimya kwa sababu ni chama dola.

Pamoja na kwamba kupanda kwa gharama za maisha kunawahusu wana CCM pia, lakini hawaruhusiwi kushiriki maandamano ya kudai serikali iwajibike kurekebisha hali hii. Wakati vyama vingine vikishiriki kwa uhuru, katika mjadala wa kuwa na katiba mpya, wana-CCM wanalazimika kujikunyata au kushiriki shingo upande kwa sababu wao ni chama dola.

Yanahitajika mabadiliko ya mtizamo ili kuwezesha CCM kuwa huru kushiriki maisha ya siasa za taifa bila kujali kuwa ndicho kinatawala.

Hii itaisaidia serikali kuwajibika kwa sababu, ikifanya ajizi inaweza kuondolewa na chama kilichoiweka madarakani. Hali hii imetokea hivi karibuni huko Afrika Kusini, Israeli, Uingereza na Italia.

Chama tawala kuondoa serikali yake madarakani si uhaini, bali ni haki ya chama cha siasa kinachofahamu nafasi yake katika medani za kisiasa.

Rais Kikwete aliingia madarakani kwa nguvu kubwa ya umma. Alibeba dhamana kubwa ya wana-CCM na wasio wana-CCM. Mtaji huo ulitosha kumsaidia kufanya mabadiliko makubwa ndani na nje ya chama chake. Tutahitaji wanahistoria makini kutuandikia ni kwa nini Kikwete alisita na bado anasita kutumia dhamana hii katika kukikarabati chama cha mapinduzi.

Ikibidi watahitajika wana usalama na makachero wenye uzalendo kuliambia taifa, ni nini kilimzuia Kikwete kutumia dhamana hii kubadili hali ya Watanzania waliomchagua kwa kishindo kikubwa.

Chini ya utawala wake ndani ya chama, hata wale waliokuwa magwiji wa fikra pevu wamefumbwa midomo yao na kubakia kunung’unikia chini ya meza. Chini ya utawala wake, CCM imepoteza hazina kubwa ya matumaini ya watu na badala yake inatumia njia za hatari ili kuweza kubaki madarakani.

Siku njia hizo za hatari zinahujumu mshikamano na amani ya taifa letu.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: