‘Utajiri’ wa Adam Malima


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

KUIBIWA kwa vitu mbalimbali vya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima akiwa hotelini Nashera ya mjini Morogoro, kunaibua maswali mengi.

Hebu tuangalie vitu vilivyoibiwa:

 1. Kompyuta (laptop) tatu, aina ya Dell zenye thamani ya Sh. 5.6 milioni.
 2. Vinasa sauti (tape recorder) viwili vya digitali vyenye thamani ya Sh. milioni moja.
 3. Simu tatu za mkononi (Nokia C6 ya thamani ya Sh. 500,000, Nokia E200 ya Sh. 250,000 na Blackberry yenye thamani ya Sh. 5.5 milioni).
 4. Pete mbili za almasi zenye thamani ya Sh. 2.5 milioni.
 5. Dola za Marekani 4,000 ambazo ni sawa na Sh. 6.5milioni.
 6. Fedha taslimu za Tanzania Sh. 1.5 milioni.
 7. Kadi mbili za benki (ATM).
 8. Mabegi matatu yaliyojaa nguo.
 9. Baraghashia mbili zenye thamani ya Sh. 50,000.
 10. Nyaraka “mbalimbali” za serikali na za binafsi.
 11. Pasipoti mbili za kusafiria. 

Miongoni mwa vitu ambavyo havikuibiwa ni pamoja na bastola na bunduki aina ya shotgun. 

Kwa maoni yangu, kubeba vitu vyote hivi, ni ulimbukeni kama wa hadithi ya zuzu aliyeshinda bahati nasibu akaamua kununua kila kitu mtaani kwake, hadi kituo cha basi.

Katika hali ya kawaida, mwanasiasa anasafiri na laptop tatu za nini? Vinasa sauti: Je, yeye amekuwa mwandishi wa habari au mpelelezi anayetafuta ushahidi wa sauti? Nini hasa?

Simu tatu: Bahati mbaya huu ni utamaduni nchini Tanzania, lakini pia sijawahi kusikia Blackberry ya gharama zote hizi karibu zaidi ya dola 3,400 za Marekani. Hiki ni kiroja…Ina nini hiyo simu?

Pete mbili: Hizo sawa lakini bado alipoongea na waandishi alikuwa amevaa mapete mengine. Sasa yote ya nini?

Dola za Marekani zote hizo kwa safari ya vijijini ni za nini? Au alizipata hukohuko?

Kiasi cha fedha za Tanzania, nadhani hicho ni sawa, maanake alihitaji kulipia gharama kadhaa. Pia, kadi mbili za benki ni sawa na hata mabegi matatu ya nguo si ajabu kama alikuwa na safari ndefu. Hata baraghashia mbili si tatizo.

Nyaraka za serikali: Hii ni fedheha kubwa, kwa kuwa kama naibu waziri alipaswa kujua jinsi ya kutunza nyaraka za serikali mara aingiapo hotelini au popote pale. Huwezi kuziweka nyaraka nyeti hovyohovyo tu.

Pasipoti mbili zote za nini? Alihitaji kwenda nazo Morogoro…? Silaha: Magazeti yameandika kuwa ni bastola na shotgun. Kwa kubeba silaha zote hizi anaogopa nini au analinda nini…? 

Mavitu, makompyuta, mahela, masilaha, mavinasa sauti, mapete, madude mengi tu. Swali: Je, kuna utu-uzima hapo? Hii ni sifa nzuri ya kiongozi kweli…? 

Pana tatizo hapa; ni zaidi ya kuibiwa naibu waziri fulani. 

Imechotwa kwenye mtandao wa Wanabidii na imehaririwa
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: