‘Waasisi wa CCJ wafukuzwe CCM’


Andrew Kamanda's picture

Na Andrew Kamanda - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version

TANGU taarifa kwamba spika wa zamani wa Bunge, Samwel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe, ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Chama cha Jamii (CCJ) ziibuke, mjadala mkubwa umekuwepo ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Makundi mawili yamechomoza. Wale wanaoshinikiza chama kuwafukuza uanachama wote waliohusika na uanzishaji wa CCJ, wakati wakiwa bado wanachama na viongozi wa CCM.

Wapo pia wanaowatetea kina Sitta na kutaka chama kupuuza madai hayo.

Mbali na Sitta na Dk. Mwakyembe wengine wanaotajwa kuwa waanzilishi wa CCJ, ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kada wa chama hicho, Daniel ole Porokwa na mwenzake Paulo Makonda.

Wanaotetea wale wanaoitwa “wasaliti wa ndani ya chama,” wamejenga hoja kuu tatu kuhalalisha hoja yao.

Kwanza, kwamba shutuma hizo si za kweli, kwa hoja kuwa majina ya wote waliotajwa hayapo kwenye kitabu cha Msajili wa Vyama vya Siasa.

Pili, aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi wa CCJ, Richard Kiyabo amekana kuwafahamu Sitta, Dk. Mwakyembe na Nape katika kilichokuwa chama chake.

Tatu, hoja ya kuanzishwa CCJ, ni hoja mfu. Kwamba suala hilo limepitwa na wakati; na kwamba tayari msajili wa vyama alifuta chama hicho. Tuanze kujadili hoja mojamoja.

Kwanza, kutokuwapo kwa majina ya watuhumiwa kuanzisha chama katika daftari la msajili wa vyama vya siasa. Hii si hoja yenye mashiko na haitoshi kuwa ni utetezi.

Rostam Aziz, mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, anamiliki makampuni mengi, lakini hakuna hata kampuni moja ambako jina lake linaonekana.

Hata hivyo, nani anaweza kutetea Rostam kuwa si mshirika kwenye wizi uliofanywa na makampuni ya Kagoda, Richmond na sasa Dowans?

Kikubwa cha kuangalia hapa, ni kwamba tuhuma hizi zimetolewa na watu waliokuwa wanafahamu kwa undani uanzishwaji wa CCJ.

Fred Mpendazoe, mbunge wa zamani wa Kishapu (CCM) na swahiba mkubwa wa Sitta na Dk. Mwakyembe, alishiriki katika hatua zote muhimu za kuanzisha chama hicho. Naye Porokwa amethibitisha kuwa CCJ, ni mali ya Sitta na Mwakyembe.

Aidha, mkakati wa kuficha majina unaweza kuwa ulilenga kutojulikana mapema, hasa ukizingatia kwamba wahusika walikuwa bado ni wabunge na watumishi katika chama na hivyo, wangependa kwanza wamalize kipindi chao cha ubunge ili wasipoteze mafao yao na hata kuharibu mpango.

Pili, kuhusu kauli ya Kiyabo, kwamba wahusika hawakuwa waasisi wa CCJ, nayo haiwezi kuaminiwa. 

Kwanza, ni Kiyabo huyuhuyu aliyekuwa anahubiri kuwa chama chao (CCJ) kinaundwa na viongozi waandamizi ndani ya CCM.

Je, kama hao waliotajwa si miongoni mwao, wako wapi basi wale aliopata kuwaita wakati huo kama “viongozi waandamizi ndani ya CCM?”

Kwa wanaomjua Kiyabo wanafahamu kuwa tokea aliporejea chama hicho, Agosti mwaka jana, maisha yake yote yamekuwa yakitegemea CCM.

Hivyo katika hali ya kawaida, ilitarajiwa kuwa Kiyabo hawezi kuwataja wanaomfadhili hadi hapo Nape na wenzake watakaposhindwa kumwezesha.

Tatu, hoja kwamba CCJ haipo na hivyo hakuna sababu ya kujadili “waasisi,” haiingii akilini. Kukubali hoja hiyo ni sawa na kusema waliokamatwa kwa uhaini wa kutaka kupindua serikali waachiwe kwa kuwa serikali haikupinduliwa.

Ni sawa basi tuseme mwamuzi asimuadhibu mchezaji aliyemchezea rafu mwenzake mchezoni eti kwa sababu tu aliyelengwa hakuumia. Hatwendi hivyo.

Hoja kuu hapa kama alivyoeleza mchambuzi maarufu wa gazeti hili, Kondo Tutindaga, ni kule mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete kuzungukwa na vigeugeu, wasaliti na watu wanaoweza, wakati wowote, kukihujumu chama na yeye mwenyewe.

Kama walithubutu kutumia rasilimali za chama na serikali na kutumia madaraka waliyopewa na chama kukihujumu chama, kwa maslahi ya binafsi ya kufanikisha mipango ya kuanzisha CCJ, watashindwaje kumhujumu Kikwete?

Inawezekana kwa sababu nia yao ya kuanzisha chama cha kukitoa madarakani CCM ilishindikana mwaka jana, lakini nani anaweza kueleza kuwa mpango huo hautaweza kufanyika tena?

Kwa nini tusiamini kuwa hata hicho kilichokuwa kinafanyika wakati huo – kuimega CCM vipande viwili – ndicho kinachofanyika sasa ili kurahisisha mpango wao wa kuiondoa CCM madarakani?

Hili linathibitishwa na matamshi ya Samwel Sitta kuwa mazungumzo na vyama vingine katika masuala ya siasa, ni jambo la kawaida.

Kama ni suala la mazungumzo hilo si tatizo. Lakini kilichoendelea hakikuwa mazungumzo; ulikuwa ni mkakati wa kuanzisha chama na wahusika hawakuwa wanachama wa kawaida. Ni viongozi waandamizi ndani ya CCM.

Kama Kikwete anakitakia mema chama, ni muhimu akalizingatia hili. Vinginevyo, muda si mrefu umma utashuhudia akiachwa njiani na wale anaoonekana kuwaamini.

Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa ni msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kupitia imeili: allimussa@hotmail.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: