‘Wapinzani wa Muungano kusikilizwa’


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

WATANZANIA hawatazuiwa kutoa maoni juu ya wanavyotaka Muungano uwe, MwanaHALISI limeambiwa.

“Sisi kazi yetu ni kukusanya maoni ya wananchi na  siyo kuwazuia kusema watakacho,” ameeleza mjumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni juu ya Katiba Mpya.

Wajumbe watatu wa tume hiyo, waliohojiwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, wamesema wanatafuta maoni na siyo kuzuia wananchi kutoa kauli zao kwa uhuru.

“Sheria inatuelekeza tusikilize wananchi. Tutawasikiliza. Tutazingatia kile wanachokitaka. Tutawanukuu. Labda hata kuwafafanulia pale ambako watataka maelezo. Lakini siyo kuwabana,” ameeleza mjumbe.

Wiki iliyopita wajumbe wote 30 – wakiwa 15 kutoka pande mbili za Muungano – walikabidhiwa ofisi na kutangaziwa kupewa nyumba, vifaa vya kufanyia kazi na magari.

Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ndiye alikabidhi ofisi hiyo iliyoko Mtaa wa Ohio.

Gazeti lilikuwa linataka kujua wajumbe wanaichukulia vipi kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba maoni juu ya Muungano yawe tu ya kuuimarisha na siyo kuuvunja.

Lakini, wajumbe hao wamesema msimamo wao, na hasa baada ya majadiliano ya awali ya kutambuana, ni kwamba hawatafungwa na kauli ya kiongozi yeyote.

Watakachosema, ndicho tutakachonukuu na hatimaye kuwasilisha, ameeleza mjumbe kutoka Zanzibar.

Mjumbe kutoka Bara alipoulizwa iwapo misimamo yao kuhusu Muungano itazuia kukusanya maoni ya wananchi yanayopingana nao, alisema suala la kuujadili Muungano haliwezi kuzuilika.

Amesema, hata kama kila mmoja kati yao wajumbe ana maoni yake, haitaathiri kazi waliyopewa na taifa; watakusanya na kuratibu maoni ya wananchi katika namna yoyote ile yatakavyotolewa.

Mjumbe huyo amesema, “Sisi ni wajumbe wa tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba mpya wanayoitaka Watanzania. Suala la Muungano halizuiliki kujadiliwa kwa kina na Watanzania.”

Amesema wananchi wako huru kujadili Muungano kwa kuwa kwanza, sheria yenyewe ya tume ina kipengele kinachozungumzia Muungano. “Hili suala lipo kwenye sheria. Utazuiaje?” alihoji.

Pili, amesema mwananchi atakapotoa maoni kutaka Muungano uvunjwe, “Tutamsikiliza. Hatuwezi kumzima. Tutachukua maoni yake na sababu au hoja zake. Uchambuzi wa maoni hayo hapo baadaye, utazingatia hoja alizotoa.”

“Kutakuwa na mtu mwingine atasema ‘Muungano uendelee.’ Hatutachukua maoni tu kwamba Muungano uendelee; bali tutarekodi na hoja zake. Naamini watakuwapo wale wanaosema uboreshwe kwa namna fulani, nao pia tutachukua maoni yao kwa hoja watakazozitoa,” amefafanua.

Amesema, “Suala la Muungano litajadiliwa kwa sababu maoni na katiba hiyo vinahusu Watanzania na taifa lao,” amesisitiza.

Mjumbe mwingine kutoka Zanzibar amesema kwa uelewa wake ni kwamba tume haijafungwa na sheria wala rais kusikiliza maoni yenye mrengo fulani na kuacha maoni ya mrengo mwingine kuhusu Muungano.

“Unajua, wengine tunaamini kabisa kuwa Muungano ndio msingi hasa wa kuwepo katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utaacha vipi maoni yanayopingana kuhusu Muungano.

“Mwenyekiti wetu alipotuhutubia baada ya kuapishwa, aliweka wazi suala la uhuru wa watu kusema wanavyojisikia. Alisema sisi jukumu letu ni kuachia watu kusema na tutawasikiliza kwa yale maoni watakayoyatoa. Na yote tutayanukuu,” amesema.

Kumekuwa na mgongano wa kauli kuhusu maoni yanayohusu Muungano hasa pale Rais Kikwete aliposema maoni yanayotafutwa siyo juu ya kuwepo au kutokuwepo Muungano bali juu ya kuuimarisha.

Viongozi wa serikali zote mbili, hususan wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanashikilia mtizamo huo kiasi cha watu kuchukulia kama kwamba wanaashiria watu wasijadili Muungano kwa upana wake; ikimaanisha kuendeleza mfumo wa serikali mbili.

Akizungumza mara baada ya wajumbe kuapishwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema lengo la kuweka msisitizo kwenye Muungano ni kuwaongoza wananchi waamue aina ya Muungano na siyo kuuvunja.

“Lengo ni wananchi kuamua Muungano wanaoutaka. Wengine wanataka serikali moja, wengine serikali mbili, tatu au mambo ya Muungano yamekuwa mengi tupunguze. Nia ni kurekebisha siyo kuvunja.” alisema Balozi Sefue na kuongeza:

“Kuna mambo yamewekwa katika ile sheria, kama urais, mnataka tuseme tusiwe na rais? Hapana ila tunaweza kusema labda madaraka yake yamekuwa madogo tuongeze… kama hivyo.”

Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary aliitaka Tume hiyo kutoa elimu ya Muungano kwa wananchi na kunukuu kauli ya  Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1970 alipozungumzia suala hilo.

“Nakumbuka katika hotuba ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa 6 Julai 1970 akihutubia Bunge alisema, ‘Watu wengi hawaujui Muungano. Ila sishtushwi na wageni wasioujua Muungano, bali Watanzania wasioujua Muungano wetu.”

Waziri Bakary alilenga kuhimiza tume kujitahidi kuelimisha Watanzania kuhusu Muungano.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba ameahidi “...kutumia uwezo wetu wote kutekeleza yote ambayo Watanzania wanayataka. Tunakwenda kwa Watanzania watuambie wanataka Tanzania ya aina gani.

“Nyinyi si mmetupa kazi ya kuisuka Katiba; wananchi watakuwa na hoja zao, watataka kujua uzuri wa Katiba ya sasa na upungufu wake. Hayo yatasaidia Watanzania kuifahamu zaidi Katiba,” alisema.

Tume imepewa miezi 18 kukamilisha kazi ya kukusanya maoni na kukabidhi ripoti kwa Rais Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

Hata hivyo, sheria iliyounda tume hiyo inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar, kuongeza muda wa tume hiyo kukamilisha kazi yake.

Tume itaandaa rasimu ya katiba ambayo pia itakabidhiwa kwa viongozi hao na ndiyo itajenga msingi wa katiba itakayowasilishwa mbele ya bunge la katiba kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.

Hatua ya mwisho ni kura ya maoni juu ya katiba. Kura itasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ushirikiano na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: