Abiria walipanda ‘mgongo wa mauti’


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

JIJINI Dar es Salaam, Zanzibar, Mkoani na Wete (Pemba), wasafiri wengi waliohojiwa na ambao wanatumia vyombo vya majini, wana lugha moja kuhusu hali ya usafiri kabla ya mkasa wa m.v. Spice Islander I, tarehe 10 Septemba 2011.

Wakati huyu atasimulia adha za kupata tiketi kwenye baadhi ya madirisha ya kampuni za usafirishaji majini, yule ataeleza alivyolipa mlungula ili aingie katika chombo ambacho tayari kiliishajaa.

Palipokuwa na kukimbizana kupata tiketi za mlungula, kulikuwa pia na msukumano wa kuingia kwenye chombo na mashindano ya nani atapata kiti.

Kwenye milango ya kuingilia hakukuwa na usimamizi madhubuti. Kuna waliokuwa wakiingia wamebeba mizigo, wakijiita “ma-porter.”

Katika msukumano huo, hata abiria aliyechelewa au asiye na tiketi alijiita porter ili apite. Hakurudi. Alisafiri na wakati mwingine bila kuulizwa tiketi.

Kwenye milango hiyo pia kulikuwa na “askari maslahi_ - wengine wakiitwa “mabwana usalama.” Hawa walivutana; kila mmoja akijaribu kuingiza mwenzake aliyepatana naye awali ili apitishe mizigo yake.

Kwa njia hii, vyombo vya usafiri vilishindiliwa abiria na mizigo hata kupita ukomo wa uwezo wake kiufundi. Wao walibaki bandarini “wakijipongeza.” Mkasa wa mv. Islander I ni mfano hai.

Katika baadhi ya vyombo vilivyobeba abiria wengi, hakukuwa na utamaduni wa kuhakiki tiketi zaidi ya mara moja kabla ya safari kuanza.

Kwa mtindo huu, wale ambao walifanikiwa kujipenyeza bila kulipa nauli, kama hawakunaswa wakati wa safari, wangeweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar na Pemba.

Mwandishi mmoja wa habari amekiri kuwa kuna wakati alikuta chombo kinakaribia kuondoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam; akiwa hana tiketi lakini akiwa na fedha mkononi. Aliingia na kusafiri bila kuwa kwenye manifesto, kama ilikuwepo, iliyoachwa bandarini.

Kituko cha m.v. Spice Islander I kukutwa na orodha ya wasafiri (manifesto) inayotiliwa shaka na wachunguzi, ni sehemu ya utamaduni wa baadhi ya vyombo.

Kwa mfano, hata tume ya rais wa Zanzibar ya kuchunguza ajali hiyo, imeshindwa kuoanisha kile ilichokikuta kwenye “makaratasi” yanayoitwa manifesto na kauli za wananchi wanaodai kupotelewa na ndugu na jamaa zao.

Kinachoelezwa kwa uchungu na hasa Pemba, ni kuwemo watoto wengi kwenye meli iliyozama. Hata katika mazingira ya kinachoitwa “manifesto ya ovyoovyo,” inaelezwa hakuna majina ya watoto kwa vile kumekuwa na utamaduni wa kutochukulia watoto kuwa abiria.

Yanatajwa mazoea ya mzazi au mlezi mmoja kumpa rafiki yake watoto wake ili awasindikize hadi mwisho wa safari; hasa wale wa umri chini ya miaka 12.

“Hata kama ana umri wa miaka 18, kama mwili wake ni mdogo na aliyenaye anadai ni miaka 11 au 12, basi alikuwa anabebwa, ama kwa kulipa nusu au bila kutoa nauli,” ameeleza Fatma Hatib wa Kichungwani, Chake Chake.

Watoa taarifa wanasema hakukuwa na udhibiti wa vyombo vya usafiri. Udhibiti umo katika maeneo mawili.

Kwanza, wingi wa abiria na mizigo. Wanatoa mfano wa meli m.v. Maendeleo inayomilikiwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Inadaiwa kubeba abiria zaidi ya 1,000 wakati uwezo wake ulikuwa 750 tu. Hivi sasa imeruhusiwa kubeba abiria 450 tu kwa uangalizi.

Pili, usalama au ubora wa chombo. Ilikuwa baada ya mkasa wa Spice Islander ndipo serikali ilisikika ikiamuru kuzuia vyombo vingi vya usafiri ili vifanyiwe uchunguzi.

Ni wakati huohuo serikali iliagiza kuwa vyombo ambavyo vilikuwa na hitilafu, lakini viliachwa kuendealea kufanya kazi, visimamishwe mara moja.

Hapa ndipo wasafiri walielewa kuwa kumbe walikuwa wakipanda kwenye “mgongo wa mauti.”

0
No votes yet