Acha Spika afanye kazi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version

TANZANIA haihitaji watu wakamilifu, kwani hawapo duniani; haihitaji watu watakatifu, kwa kuwa hawako mbinguni; taifa hili halihitaji watu wasiokosea, hao nao hawapatikani; bali taifa linahitaji watu ambao wanajua mapungufu yao.

Watu ambao wamesahihisha makosa yao na wanakubali kusahihishwa. Taifa linahitaji watu ambao wanatukuza uadilifu na wanautafuta kwa nguvu zote.

Taifa linahitaji viongozi ambao wanatambua wito wao kuwa ni mkubwa zaidi kuliko makosa au udhaifu wao; viongozi ambao wako tayari kusahihisha walikoharibu, siyo wanaoendelea kunyosha kidole kuwa "fulani naye si safi."

Hawa ndiyo wanahitajiwa na taifa hili. Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, ndiye kiongozi aliyesimamia wito huu wa kulikomboa taifa kutoka mikononi mwa mafisadi.

Hakuna kiongozi yeyote nchini kwa sasa, anayeweza kujilinganisha na Sitta. Huyu amesimama kama ngao kati ya pande mbili, ile ya mafisadi ya kutaka kuliteka Bunge na wananchi wanaotaka Bunge libaki mikononi mwao.

Kuna watu ambao wanatumia hoja ya kuwa "Sitta naye si safi." Hoja hii ni dhaifu na wala haina msingi. Uchafu wa mtu haumfanyi ashindwe kuona usafi au kuutetea usafi. Mtu mchafu ni yule ambaye hataki kusafishika.

Hakuna mashaka kwamba Spika Sitta amelipa Bunge letu kile ambacho kwa miaka mingi tumekuwa tukilalamikia kukikosa: “Meno.”

Kwamba yanang’ata ndiyo sababu kuna kelele na njama za kumsulubu kwa kuwa eti anaruhusu wabunge kutoa maoni yao juu ya ufisadi.

Hivyo basi, habari kwamba spika Sitta alipewa kibano katika mojawapo ya vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), si habari njema.

Taifa hili haliwezi kukubali kuona watu wachache, tena wasio na mamlaka wakijadili kutoridhishwa kwao na mambo yanayofanyika bungeni, kujadili nje ya taratibu za Bunge.

Viongozi waliomjadili Sitta, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, wanajua kuwa Bunge siyo tawi la CCM wala jumuiya za chama hicho. Kwamba spika Sitta ni Spika wa Bunge la Muungano.

Kama kuna mbunge asiyefurahishwa au kuridhishwa na mwenendo wa Bunge, taratibu zipo za kutoa malalamiko yake.

Hawawezi kuleta malalamiko yao, ndani ya bunge kwa sababu, wanajua kuwa Bunge ni mhimili mwingine wa dola na spika ni mkuu wa mhimili huo.

Kwamba ndani ya Bunge hakuna ambaye angewaunga mkono; wakizungumza bungeni taifa zima litajua nani kazungumza nini na ana hoja gani. Hivyo wanaogopa kujulikana.

Maana Sitta anajua kuwa hii ni vita na siyo mapambano. Unaweza ukapoteza pambano moja au mawili, lakini mwisho wa siku utashinda vita. Wao wametumia vikao vya chama, Sitta anawasubiri tena bungeni.

Sitta anajua kuwa Bunge haliongozwi na Katiba ya CCM au maoni ya wana CCM peke yao. Wale wanaoimba spika ni wa CCM na mjadala ni wa CCM na hivyo CCM inaweza kufanya lolote na kwa mwanachama yeyote, hawajui walitendalo.

Hata kama Spika anatoka CCM, siyo mwanachama wa kawaida wa CCM kama vile rais asivyo mwanachama wa kawaida.

Hawa ni wakuu wa mihimili ya dola na ukishafungulia mlango wa kumshambulia mmoja nje ya utaratibu wa kikatiba kwa sababu ni mwanachama wenu, nini kitawazuia msimshambulie mwingine kwa kisingizio kilekile?

Hivyo, tunapoona kikundi cha watu wachache kinajaribu kuliteka Bunge na kulijadili pembeni na kutaka lifanye mambo kwa manufaa ya kikundi cha watu hao wachache kwa jina la "chama" ni lazima tukipinge.

Kama kweli kuna kundi ndani ya CCM ambalo lina matatizo na Bunge au na Spika, lisimame hadharani kusema hivyo, badala ya kufanya uviziaji wa kushtukiza watu njiani.

Hivyo ndivyo ilivyo duniani kote. Majuzi, Spika wa Bunge la Uingereza, Michael Martin alilazimishwa kujiuzulu kufuatia kashfa ya matumizi ya fedha za walipa kodi.

Licha ya majaribio yake ya kutengeneza alichoharibu, alijikuta akilazimishwa kujiuzulu nafasi hiyo na kuwa Spika wa kwanza kufanya hivyo kwa zaidi ya miaka 300.

Kilichofanyika kilifanyika wazi na hadharani. Wabunge wa chama chake wenyewe walimtosa; wakazungumza bungeni na wakajulikana ni nani.

Na hilo pia lilimkuta hata waziri mkuu, Gordon Brown ambapo wabunge wa chama chake na wengine waliowahi kuwa rafiki zake walijaribu (bila mafanikio) kumng’oa kutokana na kashfa hiyohiyo.

Fikiria kama wapo wabunge majasiri (kama tuliowaona wakati wa sakata la Lowassa na Richmond) ambao watasimama bungeni na kutaka Kikwete ajiuzulu urais!

Inawezekana hilo kutokea kwani rais wetu anaweza kuondolewa na Bunge ikibidi na kwa jinsi anavyoshughulikia suala hili nitakuwa mtu wa mwisho kusikitika endapo wabunge wataamua kuonesha nguvu yao dhidi ya rais.

Tunawapinga hawa NEC kwa sababu siyo kazi yao; tunawapinga kwa sababu Bunge si la kwao – ni Bunge la Watanzania; tunawapinga kwa sababu wamefanya kwa woga – wangekuwa majasiri wangesimama bungeni mbele ya Spika Sitta. Hawakufanya hivyo.

Ni vema kama kweli wanaamini walichokisema, Novemba walete hoja zao dhidi ya spika Sitta hadharani. Nina uhakika hakuna mbunge yeyote aliyezungumza kumkandia Sitta katika mkutano wa NEC, ambaye atakuwa na ubavu wa kusema kitu dhidi ya Spika huyo bungeni.

Nawatahadharisha CCM, msiliteke Bunge wala kusababisha Bunge lisimame peke yake, au Spika afanye mambo ambayo yamewahi kutokea sehemu nyingine duniani ambako kumekuwepo na mvutano kati ya Bunge na serikali.

Ninawahakikishia kuwa mkiendelea kulishambulia Bunge letu namna hii (kama walivyofanya wengine mwaka jana), tutawapinga kwa nguvu zaidi kwani sasa hivi ni Bunge tu linasimama kati yetu na mafisadi.

Kama mnafikiri mambo hayaendi vizuri, na mnafikiri mna hoja, Bunge lina watu wenu wengi, na rais anatoka chama chenu; vunjeni Bunge mrudi kwa wananchi sasa.

Kama mnaona Bunge halichezi ngoma mnayoipiga au kuitikia mlio wa sauti zetu, rudini kwa wananchi mtafute uhalali upya.

Kinachooneka sasa, ni kwamba baada ya CCM kuruhusu utajiri wetu utekwe nyara na mafisadi, sasa wanataka kuteka na Bunge. Hili ni tatizo kubwa na la msingi.

Maana kama kuna watu wazima, wasomi na wanaoamini wako huru, lakini bado wanaamini kuwa CCM ndiyo baba yao na mama yao, basi taifa hili siyo tu linaongozwa na watu wasiostahili na hivyo linahitaji kukombolewa, bali pia hata CCM yenyewe imejiondolea uhalali wa kutawala.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “CCM siyo mama yangu.” Je, nani zaidi ya Mwalimu? Yusuph Makamba anayesisitiza kuwa CCM ndiyo baba na mama?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: