Acha ufisadi uiue CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

SASA zipo kila dalili kwamba ufisadi ndio sababu kuu itakayochangia kuanguka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ufisadi umedhoofisha mifumo yote ya uongozi katika chama chenyewe na tayari umehamia kisawasawa kwenye serikali inayoiongoza.

Tunaona hata pale serikali inapopeleka bungeni sheria mpya kwa nia ya kutatua tatizo fulani, ufisadi unapenya na kuiviza isitekelezeke.

Ndio maana zipo sheria nyingi zikiwemo nzuri tu, lakini bado hazijaleta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayokera jamii.

Matokeo yake, utendaji wenye ufanisi katika serikali zote mbili umekosekana na hivyo chama hicho kushindwa kutekeleza ahadi zake.

Inafaa kusema kuwa viongozi waandamizi serikalini, wakiwemo mawaziri ambao ni viongozi wa CCM, wanatambua fika mifumo ya uendeshaji serikalini inalea ufisadi.

Wezi wa fedha za serikali, wafujaji wa mali ya umma na raslimali ambazo nchi zetu zimejaliwa, wanalindwa badala ya kudhibitiwa.

Hili linathibitishwa kwa watuhumiwa ufisadi kutokamatwa ili wafikishwe mahakamani, kama vile wanavyoogopwa wawekezaji wa kampuni za nje zilizoruhusiwa kufungua mitaji yao nchini.

Maendeleo kidogo yanayoonekana, tunaamini yametokana na watendaji wanaokataa ufisadi. Wanatenda kulingana na misingi ya sheria na mapenzi yao kwa nchi yao.

Bali kwa miaka kadhaa sasa, hasa baada ya serikali kufungua milango huria kwa shughuli za uwekezaji katika kila nyanja, kasi ya maendeleo imekuwa ikizidi kupungua.

Kinachojionyesha badala yake, ni ongezeko la umasikini kwa kundi kubwa la wananchi, huku wawekezaji wakijivuna kuingia kiulaini na baada ya miaka michache kutoka wakiwa wameongeza utajiri.

Hayo ni matokeo ya ubia mchafu uliopo kati ya viongozi waandamizi serikalini waliojenga kiburi maana hawadhibitiwi, na matajiri wenyeji na wageni.

Ubia huu umebadilisha dhamira za uhuru. Viongozi hawana tena ujasiri katika kupigania haki za raia wala maendeleo yao.

Tunashuhudia ubia wa viongozi na matajiri dhidi ya maslahi ya Watanzania wanyonge.

Ni ubia huu umeifikisha serikali kwenye mstari mwekundu. Haina tena uwezo wa kulinda raslimali za nchi wala kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Hali imekuwa mbaya kiasi cha hata wabunge wa CCM kuishambulia hadharani serikali yao. Ila inawezekana hawafanyi hivyo kwa kuwatetea raia, wanahofia tu hatima zao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: