Afghanistan: Mtihani mkubwa kwa Obama


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version

MAREKANI inaingia mwaka wa kumi tangu ijiingize katika vita nchini Afghanistan, hivyo kuifanya vita hiyo kuwa ndefu kuliko vita nyingine yoyote ambayo Marekani imepigana katika historia yake.

Mwaka wa kumi umeingia katikati ya mtiririko wa habari mbaya kutoka viwanja vya mapambano – kukatwa kwa njia za kupeleka mahitaji na zana kwa wanajeshi wa Marekani, kuchomwa moto kwa matenki yao ya mafuta na kuongezeka kwa vifo vya askari wake na raia wa Afghanistan.

Pamoja na ripoti kwamba sasa hivi Marekani yenyewe imeanza kuwanunua baadhi ya wapiganaji wa Taliban kwa ajili ya kulinda vikosi vyake, ushindi bado ni ndoto kubwa kwa nchi hiyo.

Wachunguzi wa mambo nchini Marekani wanasema kama Rais Obama anafikiri ana mbinu za kukwepa kipigo katika uchaguzi wa mabunge yote mawili nchini mwake mapema mwezi ujao, hawezi kuwa na mbinu kama hizo ifikapo mwaka 2012, mwaka ambao yeye mwenyewe atajaribu kuomba tena kura kutoka kwa wananchi endapo hali ya kijeshi nchini Afghanistan itaendelea kuwa mbaya.

Hii ni vita ambayo haina tija, manufaa au ulazima wowote kwa Marekani, sana sana inaiangamiza mojawapo ya nchi masikini sana duniani, ikiua raia wa nchi hiyo kwa kasi kubwa na hivyo kuitia doa Marekani yenyewe kwa njia kadha.

Vita hii inazidi kuisukuma Marekani kuingia katika madeni makubwa kwani inatumia zaidi ya dola 1.5 bilioni kila mwezi – hela za kukopa. Aidha vita hiyo inaathiri utawala wa sheria –

Marekani inashikilia katika magereza mbali mbali nchini humo maelfu ya raia wa Afghanistan pasipo kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Utesaji wa wafungwa nao umekuwa ukiripotiwa, ukikumbusha utesaji ule wa gereza la Abu Ghraib nchini Iraq miaka sita iliyopita. Ndege zisizokuwa na rubani (drones) nazo huua mamia ya raia kila mwezi. Wanaharakati wa masuala ya sheria nchini Marekani wanatamka waziwazi kwamba vitendo vyote hivi si kitu kingine bali uhalifu wa kivita.

Isitoshe Marekani inaikandamiza demokrasia nchini humo kwa kumbeba kiongozi asiyependwa – aliyeingia madarakani kutokana na uchaguzi uliojaa wizi mkubwa wa kura. Huyo ni Hamid Karzai ambaye hata maafisa wakuu wa serikali ya Marekani wanamuona ni kiongozi aliyezama katika dimbwi la rushwa.

Aidha vita hiyo inaathiri usalama wa Marekani yenyewe kwa kuongeza maadui kila siku, maadui ambao huenda wataichukia Marekani kwa miaka mingi ijayo.

Kibaya zaidi ni kwamba vita hii inakua na kuchukua sura ya mvurugano mkubwa usioeleweka baina ya nchi mbili zinazopakana – Afghanistan na Pakistan.

Tangu aingie madarakani, Obama aliamuru uzidishwaji wa mashambulio katika maeneo ya Pakistan kwa kutumia zile ndege zisizokuwa na rubani na kuua raia pamoja na viongozi wa wapiganaji. Yote hii ni katika lile lengo la kuwasaka na kuwaangamiza wapiganaji wa Taliban katika maeneo ya mipaka baina ya nchi hizo mbili.

Walengwa nao wameamua kulipiza kisasi kwa kulipua matenki ya mafuta na kuharibu njia za mawasiliano katika maeneo ya mipaka ili mahitaji yasiwafikie majeshi ya Marekani nchini Afghanistan. (Kwa kuwa Afghanistan haina ukanda wa bahari, mahitaji yote ya kijeshi hupitia Pakistan).

Wachunguzi wa masuala ya kijeshi wanasema kwamba kuharibu kwa njia hizi za mawasiliano na kuteketezwa kwa moto kwa matenki ya mafuta, vitu ambavyo ni muhimu katika kuendesha vifaru na ndege za kijeshi vinaweza vikawa ndiyo msumari wa kwanza katika jeneza la vita ambayo Marekani haiwezi kamwe kushinda.

Hata kabla ya kuanza kwa uharibifu huu wa njia za mawasiliano, gharama ya kumuweka askari mmoja wa Marekani nchini Afghanistan ni Dola milioni moja kwa mwaka. Gharama hizi sasa bila shaka zitapanda kwa haraka.

Na nchini Marekani kwenyewe, kuna wasiwasi mkubwa kwa chama cha Democrat cha Obama kitapoteza wapiga kura, na kwa maana hiyo kupoteza viti katika mabunge yote mawili (Bunge na Seneti) katika uchaguzi mapema mwezi ujao.

Hii ikitokea, itakuwa imesababishwa na chama hicho kukimbiwa na wapiga kura kwa sababu, pamoja na masuala mengine, kuiendeleza vita hii ya Afghanistan ambayo haina tija yoyote kwa nchi hiyo.

Ikumbukwe kwamba katika kampeni zake za kuwania urais mwaka 2008, Obama alijinadi kwa kusema kwamba angetoa kipaumbele kumaliza vita vya Iraq na Afghanistan.

Sasa hivi viongozi wengine kutoka chama chake wanamlalamikia Obama na viongozi wake wengine kwa kupuuza wito wa wafuasi wa chama hicho ambao wanamuona anaendeleza sera za kuzidisha vita nje ya mipaka ya nchi hiyo, hivyo kuongeza gharama za matumizi ya kijeshi na kusababisha uuzwaji mkubwa wa zana za kivita nchi za nje katika historia ya nchi hiyo.

Wachunguzi wa mambo wanaongeza kwa kusema kwamba iwapo vita hii itaendelea kurindima ifikapo 2012 – mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Marekani – hasira za Wamarekani zitaongezeka na hivyo kuweza kumuangusha katika jitihada zake za kuchaguliwa tena – hasa kupata uteuzi kutoka chama chake mwenyewe.

Wachunguzi wanasema kampeni ya kutaka vita (vya Iraq na Afghanistan) vimalizike vilianza kabla ya mwaka 2006 na ndiyo zilikipatia chama cha Democratic ushindi wa viti vingi katika mabunge yote mawili ya nchi hiyo kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10. Kabla ya hapo, chama cha Republican ndiyo kilikuwa na uwingi wa viti katika mabunge hayo.

Wanaharakati wanaopinga vita wanataka Obama na serikali yake waupate ujumbe huu – kwamba ni lazima amalize vita ya Afghanistan na angalau kuanza kuondoa askari wake kabla ya 2012 ama sivyo asahau urais wa muhula wa pili.

Lakini kwa kuwa sasa vita hiyo imeanza kujipanua na kuingia katika ardhi ya Pakistan, kumalizika kwa vita hiyo kabla ya 2012 itakuwa ni ndoto tu.

0
No votes yet