Afrika Kati wapania kuinyanyasa Stars


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version

NILIBAHATIKA kukaa katika kambi ya timu ya soka ya taifa ya Afrika Kati, Les Fauves (Simba kwa Kiswahili), tangu ilipotua nchini Jumatatu usiku nikiwa mkalimani wao, hadi Jumapili ilipoondoka.

Nilikaa nao, nilizungumza nao, nilicheka nao wakati wa mazoezi na mjini nilipowapeleka kununua vitu kama vile viatu vya mpira na jezi kwa ajili ya timu za Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.

Baadhi walinunua baiskeli, televisheni, helmeti kwa ajili ya pikipiki, simu za mkononi, vioo vikubwa na vitu mbalimbali. Kila kitu walichouliza, bei ya hapa ni chini kuliko Bangui.

Walishangaa wingi wa magari na wingi wa maghorofa na hata idadi ya watu. Walisema mji wa Bangui una watu wapatao 700,000 na nchi nzima ina watu 4 milioni.

Uhusiano kati yangu na wao ulikuwa mzuri isipokuwa uwanjani wakati wa kukagua wachezaji kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na wakati wa mchezo.

Ghafla wote—viongozi na wachezaji—walifura kwa hasira pale kamisaa wa mechi ile, Mohamed Hatimy kutoka Kenya na nahodha wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa walipopinga uhalali wa Les Fauves kumtumia Enza Manasse.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inaonyesha Enza Manasse hapaswi kucheza kwa vile ana kadi mbili za njano. Les Fauves walikuja juu wakidai mwenye kadi mbili za njano ni Enza-Yamissi Manasse na waliyekuja naye ni Enza-Yamissi Elodge.

Jambo la kushangaza ni kwamba Afrika Kati walikuja na pasipoti mbili mbili—moja ya kidiplomasia ya pili ya kawaida. Kwa nini? Wanadai ili kurahisisha usafiri wa wachezaji wao.

Kamisaa alikubaliana nao kwa sharti waandike barua ya uthibitisho na kutia saini ambayo aliambatanisha katika ripoti yake. Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika Kati, Gregoire Zowaye ndiye aliandika barua hiyo.

Mechi ilipoanza na timu yao kupata bao la kuongoza, waliruka kwa furaha kwenye meza kuu ambako mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. John Nchimbi.

Hata bao la Stars kusawazisha bado walikuwa na furaha. Uhusiano kati yangu na wao ulivunjika baada ya bao lao ambalo lingekuwa la pili kukataliwa na mwamuzi Eddy Maillet wa Ushelisheli kwa madai mfungaji Mabide Vianney alikuwa ameotea.

Rais wa Shirikisho,  Edourd Ngaissona alivurugikiwa na kukosa ustaarabu, akatoka kwenye meza kuu akitaka kushuka kupambana na mwamuzi. Waziri wao wa michezo Zingas Simplice alivumilia, kazi ikawa kwa Gregoire kumtuliza bosi wake.

Ngaissona alifoka: “Vous allez voir pendant le match retour” yaani Stars itaipatapata wakati wa mechi ya marudiano kwao.

Bao la pili kwa Stars lililofungwa na Mbwana Samatta liliwanyong’onyeza na kubaki kila mmoja akiapiza kuwa Stars lazima ‘ifanyiziwe’ Bangui.

“Le math retour sera autre chose, mon frere” aliapa meneja wa vifaa Maurice Dimanche akiwa na maana mechi ya marudiano itakuwa kitu kingine ‘rafiki’ yangu.

Akionekana kuridhika na matokeo, kocha mkuu Jules Accorsi alisema, “C’est comme ça partout” yaani soka ndivyo ilivyo kote na akasisitiza kwamba mechi ya marudiano itakuwa ngumu kwa Stars.

Japo Mfaransa Jules alionekana kuridhika na matokeo hakuelewa kwa nini hawakupewa penalti Kado alipodaka mpira na kumlalia mshambuliaji wa Les Fauves.

Hotelini basi lilipochelewa kwa dakika 10 kuwapeleka mazoezini Jules alitema vitisho: “On va vous souffrir chez nous,” akimaanisha msafara wa Stars utateswa katika mechi ya marudiano itakayofanyika Juni mwaka huu katika jiji la Bangui.

Afrika Kati ilikuja kimitego mitego. Walitua nchini kwa mafungu na hawakutaka kuwa wazi kuhusu programu yao jambo lililochangia ugumu wa mawasiliano na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania).

Jumatano walikasirika basi lilipochelewa kuwachukua kutoka hoteli ya Tansoma, Gerezani kwenda uwanja wa Karume kwa ajili ya mazoezi. Lakini Alhamisi wakawa wasumbufu.

Asubuhi walijichelewesha na walipoamua wakaenda zao kutembea Coco Beach. Mchana wakaenda Uwanja wa Karume ambako Stars ilikuwa inafanya mazoezi. Kwa kuwaheshimu wageni, Stars walitoka uwanjani kupisha Les Fauves ambao walilalamikia uwanja huo kwa madai ungewaathiri.

Ieleweke kwamba Les Fauves hawakugomea uwanja wa Karume kwamba haufai, ila walihitaji uwanja wa nyasi halisi kwa vile mechi ilipangwa kufanyika kwenye uwanja wenye nyasi halisi.

Mazoezini walikuwa wanatumia maji yaliyonunuliwa na TFF lakini siku ya mechi walinunua maji yao wakaacha waliyopewa na wenyeji wao.

Waliovutia
Kocha msaidizi Herve Loungoudji amewamwagia sifa kipa wa Stars, Shaaban Hassan ‘Kado’ na winga wa kushoto Mrisho Ngassa.

“Mna kipa bora na winga machachari sana,” alisema Herve akiwa amevaa tabasamu Jumapili asubuhi.

Lakini Jules alimsifu Ngassa zaidi akisema ana kasi na mwepesi. “Kipa ndiyo mzuri, lakini hakuwa na kazi, hakupata misukosuko mingi. Mchezaji wenu hatari ni yule winga wa kushoto, ana kasi sana, ametusumbua mno,” alisema.

Kuhusu Samatta, Jules alisema alipata bahati tu kwa vile mabeki wake walikosa uzingativu dakika za mwisho. “Mais vous avez la meilleure équipe” yaani Tanzania ina kikosi kizuri.

Baada ya matokeo ya juzi na jana ya timu za kundi D, kila timu ina pointi nne ila Les Fauves wanaongoza kwa wastani mzuri wa mabao wakifuatiwa na Stars Stars, Morocco na Algeria. Stars bado ina mechi mbili nje dhidi ya Afrika Kati na Morocco na inaisubiri Algeria kwenye Uwanja wa Taifa.

0
No votes yet