Afrika yapita kipindi kigumu kidemokrasia


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version

SUDAN imegawanyika; Tunisia inajiunda upya; Ivory Coast inatafuta njia kukwepa machafuko; Kenya inajitahidi kukimbiza viongozi wake waandamizi wasishitakiwe mahakama ya kimataifa ya uhalifu.

Nchi hiyo kubwa zaidi kwa eneo barani Afrika imegawanyika baada ya wananchi wa upande wa kusini kuchagua kujitenga na serikali inayoongoza kutokea mjini Khartoum.

Hatua hiyo inamaanisha kuwa bara la Afrika limepata nchi mpya iitwayo Sudan Kusini ambayo kwa kuijumuisha na nchi 52 wanachama wake sasa Afrika ina wanachama 53.

Hapo ilipofika Sudan pametokana na sera mbovu na kandamizi ambazo hazizingatii mazingira ya wakati na kutatua shida za wananchi.

Tunisia imeingia matatizoni siku nyingi kutokana na utawala mbaya wa aliyekuwa rais Zine al Abidine Ben Ali lakini ikalazimika kukabili machafuko yaliyosababisha mauaji.

Maongozi mabaya yalichochea maandamano ya umma yaliyoanzia kwa wanafunzi na vijana wasio na kazi mjini Tunis, na hatimaye kuungwa mkono na raia wa miji mingine.

Hata pale rais Ben Ali alipojitahidi kulegeza mkono na kuahidi kujadiliana na wapinzani, hakukubaliwa na umma na hivyo kulazimika kuondoka Ikulu na kukimbilia uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Hiyo ni sehemu tu ya mienendo ya mambo katika nchi za Afrika nyingi zikiwa katika mahamaniko ya kutafuta kile kiitwacho ukombozi wa pili baada ya kuondokana na ukoloni wa wazungu.

Wimbi linalozidi kushika kasi sasa ni la mabadiliko ya mifumo ya uongozi kwa lengo la kustawisha demokrasia ya kweli. Wananchi wamekuwa wakitaka kuona utawala bora na mipango mizuri ya kiuchumi.

Kinyume na ilivyozoeleka kwamba uchaguzi ndio njia nzuri ya nchi kupata viongozi waliochaguliwa katika misingi ya kidemokrasia, katika zama hizi imeonyesha dhahiri kuwa safari ya Afrika kupata demokrasia ya kweli ingali ndefu.

Kuanzia na kuwepo kwa hali ya kutoaminika kwa tume zinazosimamia uchaguzi hadi kila mhusika kujenga utamaduni wa kukubali matokeo ya uchaguzi, ni changamoto kubwa zilizopo mabele.

Bali ipo changamoto nyingine kubwa miongoni mwa viongozi wanaoshika madaraka katika nchi mbalimbali Afrika. Wanapaswa kuamiani kuwa hata wananchi wenzao walioko nje ya madaraka wanayo haki ya kuongoza serikali.

Kwa mfano, kinachotokea nchini Ivory Coast sasa ni matokeo ya utamaduni mbaya wa viongozi waliopo madarakani kuamini kuwa ni wao tu wenye haki ya kuongoza serikali katika nchi zao.

Utamaduni huo husababisha viongozi hao kuwa wagumu wa kuachia ngazi hata pale wanapokataliwa na wananchi kupitia masanduku ya kura.

Laurent Gbagbo ameshindwa uchaguzi, lakini amekataa kung’atuka na kutambua ushindi wa mpinzani wake mkubwa Alassane Ouatarra.

Matokeo yake, Gbagbo ameapishwa kama rais baada ya kutangazwa mshindi na mahakama ya katiba iliyopitia na kuyavuruga matokeo halisi ya uchaguzi.

Ikumbukwe kabla ya hatua hiyo, Tume Huru ya Uchaguzi ilitoa matokeo yaliyoonyesha Ouatarra ndiye mshindi. Kule tu kuhitajika matokeo hayo kuthibitishwa na mahakama ya juu kukawa chanzo cha rais kukataa kushindwa.

Ouatarra naye amejiapisha na ameunda serikali yake iliyojichimbia kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa akiungwa mkono na umoja huo, umoja wa Ulaya na jumuiya ya Afrika Magharibi. Umoja wa Afrika pia unamuunga mkono.

Ukorofi wa viongozi waliopo madarakani huonekana mapema wakati wa maandalizi ya uchaguzi wenyewe.

Chukulia mfano wa Uganda ambayo mwaka huu inaendesha uchaguzi wa rais na bunge.

Rais Yoweri Museveni amenukuliwa akisema kwamba ni yeye tu mwenye uwezo wa kuongoza Uganda, kauli inayopingwa na wanasiasa wa upinzani wakiwemo waliojitokeza kushindana naye ili kumtoa Ikulu. Wanaiita kauli yake si ya kistaarabu bali anaonyesha dharau kwa demokrasia.

Museveni tayari anakabiliwa na shutuma kali za wanasheria kufuatia kauli yake ya kutoamini kama tume ya uchaguzi inaweza kumsaidia yeye kubaki madarakani.

Museveni anasema hakuna namna chama chake cha National Resistance Movement (NRM) kinaweza kufanya udaganyifu katika uchaguzi.

“Ukiangalia muundo wa tume ya uchaguzi unaojumuisha zaidi watendaji wa serikali. Na watumishi wa serikali daima wengi wao wanaipinga serikali. Unajua hilo.

“Na hawa ndio wanaosimamia uchaguzi na kupanga mbinu za kuhakikisha upinzani wanashinda,” alinukuliwa akisema baada ya mahakama ya juu ya Uganda kuthibitisha akuwa sheria na taratibu za uchaguzi zilikiukwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2006.
 
Kauli ya rais aliyepo madarakani kuashiria kutokubali kushindwa aliitoa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kabla ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na vurugu na mauaji.

Mugabe alisema mapema kwamba asingekabidhi madaraka kwa mpinzani wake mkuu, Morgan Tsvangirai kwani yeye ndiye anayestahili kuongoza nchi hiyo.

Uongozi wake mbaya ulichochea wakuu wa majeshi pamoja na walipiganaji wa vita vya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Uingereza, nao waliapa hawatakubali kuingia kiongozi asiyekuwa Mugabe.

Wananchi wataendelea kuhimiza uongozi mzuri unaojali maslahi yao wakati wanasiasa wakorofi na walafi wa madaraka wao watakuwa wakitafuta mbinu za kung’ang’ania madaraka.

Ni mpaka pale wanasiasa watakapokubali kushirikiana na wapinzani wao kuongoza serikali ndipo Afrika itanufaika na demokrasia vinginevyo machafuko na migogoro itaendelea kulitafuna bara hili.

0
No votes yet