Afya ya Kikwete yazua mjadala


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

AFYA ya Rais Jakaya Kikwete sasa imekuwa mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi wa rika tofauti. Kufuatia rais kuishiwa nguvu, kushindwa kusimama na kukatisha hotuba mjini Mwanza mwishoni mwa wiki, wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema, kwa njia mbalimbali, kuwa afya ya rais inastahili kuchunguzwa kwa makini.

Rais Kikwete alishindwa kuendelea kuhutubia Jumapili iliyopita kwenye uwanja wa CCM, Kirumba wakati wa sherehe za miaka 100 ya Kanisa la African Inland Church (AIC) alikokuwa mgeni rasmi.

“Amelazimika kupumzika kwa dakika chache katika chumba cha mapumziko kwenye Uwanja wa Kirumba… kutokana na kuzidiwa na uchovu kufuatia shughuli nyingi mfululizo katika siku za karibuni,” imeeleza taarifa ya Salva Rweyemamu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya rais.

Baada ya mapumziko ya “muda mfupi,” rais aliendelea kushiriki shughuli hizo za Jumapili, 4 Oktoba 2009.

“Mimi naona kuna haja ya rais wetu kupimwa na hata kupata tiba sahihi. Hii ni mara ya pili kuona akitokewa hali hii,” amesema Mohammed Khalfani aliyejitambulisha kuwa amkazi wa Kirumba, Mwanza aliyepiga simu katika ofisi za gazeti hili.

Mama Beatrice Lupembe, mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam amesema “siyo vizuri kusikia taarifa za rais kaanguka, kaishiwa nguvu au kachoka. Wasaidizi wake wanakuwa wapi?” amehoji.

Naye Seleiman wa Mbagala, Dar es Salaam amesema, “Kwani rais analazimishwa kazi? Au tuseme watendaji ikulu hawajui matatizo ya afya ya rais wetu? Mimi naona wanastahili kuwajibika.”

Tukio la Mwanza ni la pili tangu Rais Kikwete aingie kwenye majukwaa makuu ya kisiasa. Mara ya kwanza “kuishiwa na nguvu na kubebwa na wasaidizi wake,” ilikuwa Oktoba mwaka 2005.

Safari hiyo alikuwa akitafuta urais na ilikuwa kwenye mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za uchaguzi, kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Kama ilivyokuwa Mwanza, hata mwaka 2005 wasaidizi wake walisema alikumbwa na “uchovu kutokana na ratiba ngumu ya kampeni.”

Bali mara hii, ikulu na yeye mwenyewe, wamekaririwa wakisema kuwa amekuwa na ratiba ndefu, ngumu na ya kuchosha – kutoka Marekani, kwenda Arusha na baadaye Mwanza.

Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alipoulizwa kwa nini ratiba ya rais inakuwa ndefu na ngumu hadi kumuelemea, alisema “Mimi simo katika nafasi nzuri ya kuzungumza lolote.”

Alipong’ang’anizwa kutoa majibu, alisema, “Siwezi kuongelea hilo.” Akakata simu.

Daktari mmoja jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina, alizidisha ugumu wa “uchovu” wa rais pale alipotumia maneno mengi ya Kiingereza kuliko Kiswahili kuelezea alichokuwa akisema.

“Unajua, uchovu ni fatigue. Kuishiwa nguvu na kuwa na exhaustion au weariness; udhaifu wa mwili au weakness. Mimi naona hapa kuna tatizo la afya ya rais na lazima wanaohusika wachukue hatua zinazostahili kulinda afya yake,” ameeleza.

Hata hivyo, daktari huyo amesema haiingii akilini uchovu kwa maana ya fatigue uwe wa ghafla. Amesema hatua ya kukosa nguvu ghafla yaweza kuwa kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini na siyo uchovu wa kazi au safari.

“Sikiliza bwana, hali ya kuishiwa nguvu ghafla inaweza kutokana na kutokula, kama ambavyo huwatokea wasichana wanaokula kidogo sana au wanaojinyima kwa lengo la kurekebisha miili yao.

“Binafsi siamini kuwa uchovu ndilo tatizo la rais. Anahitaji vipimo. Anahitaji tiba. Sasa haijulikani ni lini tena ataishiwa nguvu; au kama aliwahi kuishiwa nguvu lakini hakuwa hadharani kama ilivyodhihirika Mwanza na Dar es Salaam,” amesema.

Aidha, taarifa ya ikulu ilimnukuu Rais Kikwete akisema mara baada ya kupumzishwa na kupewa huduma ya kwanza, “Nguvu imerudi…napenda sasa kuchukua nafasi hii kuzindua rasmi uchangiaji wa shughuli za Kanisa lenu na mimi naanza na mchango wa sh. 1,000,000.”

“Kwa kweli mshituko huu wa leo ni matokeo ya ubishi wangu. Nilishauriwa na wasaidizi wangu nipumzike baada ya kurejea nyumbani kutoka Marekani. Niliambiwa nisiende Arusha au kuja hapa. Lakini nikakataa. Siku nyingine nitawasikiliza zaidi,” ilieleza taarifa ya ikulu ikimnukuu rais.

Kauli ya rais kwamba haambiliki au anapuuza makusudi ushauri kuhusu usalama wake, nayo imewastua wengi.

“Sasa rais akiambiwa funga mkanda kwenye gari, tena kwa usalama wake, akikataa na ajali ikatokea nani atalaumiwa?” ameuliza Fabiani Lekule wa Kipawa, Dar es Salaam.

Amesema, “Hapa rais ametuacha njiapanda. Akiambiwa tusiende huku au kule kwa kuwa kuna hatari, halafu akaamuru waende na huko yakawakuta, nani atalaumiwa? Uwezo wa urais haupaswi kukiuka masharti ya usalama wake na afya yake pia.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: