Ahadi ya Kikwete inatekelezeka?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

MADAKTARI wamesema kuwa wamekubali kurejea kazini kwa kuwa wana imani na Rais Jakaya Kikwete; kwamba atatatua matatizo waliyomweleza.

Kauli yao imeleta afueni kwa waliokuwa roho juu wakifikiria jinsi ya kutougua au kuugua na kufa, kwani wasingepata matibabu.

Bali kuna jambo moja muhimu. Wamemwambia rais kuwa pamoja na kurejea kazini, hawako tayari kuendelea kufanya kazi chini ya Dk. Hadji Mponda na Dk. Lucy Nkya.

Je, katika mazingira haya tunaweza kutulia na kusema mgomo umeisha? Hautakuja mwingine?

Katika tamko lao lilitolewa na Jumamosi iliyopita – siku moja baada ya kukutana na Rais Kikwete, madaktari wanasema, “Hatuko tayari kufanya kazi na waziri wala na naibu wake.”

Kwamba pamoja na Kikwete kuendelea kuwang’ang’ania mawaziri wake hawa, madaktari wameamua “kuwafuta kazi.” Huu ndio ujumbe waliomfikishia. Ni kazi yake kuupima.

Je, viongozi waliofutwa kazi, walioambiwa na wasaidizi wao kuwa “hatutawasikiliza; hatutawapa ushirikiano;” na kumsimamisha Dk. Nkya uanachama katika chama chao, watawezaje kutimiza majukumu waliyopewa?

Hilo ni moja. Pili, madai ya madaktari ni mengi. Je, serikali itayamudu?

Madaktari wanatuhumu Katibu Mkuu Blandina Nyoni na Mganga Mkuu Dk. Deo Mtasiwa, kuingiza nchini robo tatu ya vifaa bandia vya vipimo vya ukimwi kutoka Korea Kusini.

Wakati huohuo wanatuhumu Mponda na Nkya kushindwa kufanyia kazi madai hayo ya watuishi walio chini yao.

Aidha, madaktari wanasema vigogo hao serikalini ndiyo kiini cha kukosekana huduma bora hospitalini; ndiyo sababu ya matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya wizara na ndiyo chanzo kikuu cha mgomo.

Katika hatua nyingine, haya yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa wahusika kufikishwa mahakamani. Je, hilo linawezekana katika mazingira ya kulindana ya serikali ya CCM?

Tatu, mgogoro huu unaweza kuisha vipi kama tutazingatia tabia ya Rais Kikwete ya kushughulikia migogoro? Ukweli ni kwamba amekuwa akikimbia mogogoro.

Wanaomfahamu Kikwete vema wanasema, yeye ana tabia ya kusema, “...wamenikosa. Wameondoka kama walivyokuja.” Anaweza kumtosa huyu na kumbeba yule kutegemeana na upepo unavyovuma.

Hata hili la madaktari, inadaiwa rais ameliingilia baada ya “kuangalia upepo;” ndiyo maana muda wote amekuwa kimya akimwacha Pinda kujikanyaga.

Naye Pinda mara akae kimya, mara akubaliane na madaktari; mara awafukuze kazi; mara akubali warejee kazini, mara ageuke na kusema hajasema ameahidi kumwambia rais kufukuza mawaziri wake.

Haya ndiyo mazingira ambamo Rais Kikwete ameahidi kumaliza matatizo au kero za madaktari. Kuna wanaosema rais bado ana mzigo mkubwa wa kumaliza matatizo katika chama chake pia – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wapo wanaomlalamikia hata jinsi alivyoshughulikia suala la mgombea wa Arumeru hivi majuzi. Wanadai “aliagiza kumshughulikia Siyoi Sumari.”

Kuna taarifa kwamba walioagizwa kufanya hivyo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu CCM, Bara, John Chiligati.

Lakini ilipofika Kamati Kuu (CC), ambako uteuzi wa mwisho unafanyika, Kikwete ndiye alitetea Siyoi kwa nguvu zote, kana kwamba hakuna ambacho aliagiza wenzake wakifanye. Mtoa taarifa anasema Chiligati aliishia kumwaga chozi.

Au angalia alivyoshughulikia mgogoro wa kupitisha sheria ya kuandikwa kwa katiba mpya. Alichokisimamia awali, sicho alichokuja kutenda.

Awali Kikwete alisikika akipuuza madai yote ya wadau, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Katika mkutano wake na walioitwa wazee wa Dar es Salaam, Kikwete aliwashambulia CHADEMA akisema wanasukumwa na ajenda ya siri.

Lakini alipokutana nao, akabadilika na kusema “wana hoja nzito.” Lakini walichokubaliana naye pia siyo chote alichotekeleza.

Alipokutana na wabunge wa CCM mjini Dodoma, mengi ambayo wabunge wale walifanya bungeni, inadaiwa yalikuwa na baraka zake.

Nne, kuitishwa kwa mgomo mpya kulikuja mwezi mmoja tu, tangu kumalizika kwa mgomo mkubwa wa awali ulioathiri, kwa kiwango kikubwa, huduma za afya katika hospitali za serikali na zile zinazomilikiwa na taasisi za dini.

Mgomo wa awali ulichukua siku 17 – ulianza tarehe 24 Januari 2012 na kumalizika 10 Februari 2012.

Je, kama serikali imeshindwa kutoka katika usingizi katika mgomo wa awali na pia katika mgomo huu uliositishwa, nani ataweza kuisukuma nje ya mgogoro huu mpya?

Kwa mfano, karibu madai yote ambayo madaktari walikuwa wameyadai katika mgomo wa awali, bado yako palepale. Kilichobadilika ni staili ya kile kinachoitwa “dhamira ya kuyashughulikia.”

Sasa inadaiwa Rais Kikwete ndiye atashughulikia madai ya madaktari. Imesemwa kwamba amewaambia madaktari kuwa wakikwamishwa warudi kwake. Sasa, kama hivyo ndivyo, mawaziri wake wanafanya kazi gani?

Kama kazi za mawaziri zinafanywa na rais, hii ina maana kuwa mawaziri  wameshindwa kazi; na hakika hawana kazi. Je, kwa nini wasiondoke?

Ukiangalia suala la madaktari na jinsi ambavyo serikali inalichukulia, utaona kwamba serikali, na viongozi wake, wamekosa ubunifu katika kushughulikia matatizo ya wananchi.

Unaweza kufikia hatua ya kusema kuwa waliokimbilia ikulu hawakujua wakifika huko watawafanyia nini wananchi.

Waweza kudiriki kusema pia kuwa serikali inasukumwa na upepo na inaendeshwa na matukio.

Wimbo wa maisha bora kwa kila Mtanzania haupo tena; hasa katika eneo la afya ambalo madaktari wanajitahidi kutetea.

Badala yake madaktari na wananchi wanashuhudia misululu ya viongozi wa kitaifa kwenda nje kutibiwa, huku hospitali za umma zikiwa hazina dawa wala vifaa.

Iko wapi sera ya serikali iliyohubiriwa na Kikwete ya kutoa kwa wananchi wote huduma za bure za uzazi?

Rais anasema, serikali yake inatambua, inajali na kuthamini kazi za madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini katika kulinda na kudumisha afya za wananchi wake.

Je, hii ni kweli? Kama ni kweli, lipi bora kati ya maisha ya wananchi na afya zao, kwa upande mmoja, na Mponda na Nkya kwa upande mwingine?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: