Ahadi za Kikwete ‘bomu’ 


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

AHADI kadhaa ambazo Rais Jakaya Kikwete alitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, sasa imethibitika haziwezi kutekelezeka, MwanaHALISI limeelezwa.

Baadhi ya ahadi alizozitoa rais, ambazo zinatiliwa shaka kutekelezwa, ni ujenzi wa reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa.

MwanaHALISI limeelezwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli mpya, na hata kufufua iliyopo ni mgumu kutokana na hatua ya serikali kujizonga katika maamuzi.

Pamoja na kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Kikwete aliahidi kujenga barabara za juu mkoani Dar es Salaam ili kukabiliana na kero kubwa ya foleni.

Aliahidi pia kujenga Machinga Complex mbili katika kila wilaya ya mkoa huo; kujenga hospitali katika kila jimbo na kuhakisha tatizo sugu la maji linabaki kuwa historia nchini.

Jingine ambalo Kikwete aliahidi ni kununua meli kubwa kuliko mv Bukoba iliyozama mwaka 1996, kwa ajili ya matumizi katika Ziwa Viktoria; kuboresha barabara ya Igunga-Tabora na kujenga barabara ya Njombe-Makete kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 109.

Mengine ambayo aliahidi ni kujenga barabara ya Musoma hadi Mto wa Mbu mkoani Arusha na kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Ahadi nyingine ni ujenzi wa barabara ya lami Manyovu-Kigoma-Kaliua hadi Tabora; kukarabati barabara ya Moshi-Arusha Mjini, kuboresha barabara ya Handeni, Kondoa mpaka Singida na hatimaye Dodoma, pamoja kufidia wanakijiji ng’ombe waliokufa wakati wa ukame mwaka 2009 huko Longido.

Hata hivyo, mtoa taarifa, akinukuu waraka maalum wa serikali amesema unaonyesha kampuni ya TRL iliyorithi shughuli ya iliyokuwa shirika la reli la taifa (TRC), inadaiwa dola za Marekani 44 milioni (karibu Sh. 70 bilioni).

Nayo serikali inadaiwa na RITES dola za Marekani 21,656,447.28 (karibu Sh. 32 bilioni) zilizotokana na mikataba mbalimbali ya kikazi ambayo kampuni hiyo iliingia ili kuondokana nayo moja kwa moja.

Waraka huo anaeleza, unahusu taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya serikali juu ya TLR. Unaonyesha pia kuwa serikali sasa inalazimika kutafuta mabilioni ya shilingi kulipia gharama za ukodishaji wa injini 25 na mabehewa 23 ya abiria.

Uamuzi wa kukodisha vifaa hivyo ulifanywa na menejementi ya TRL. Fedha hizo pia zilitumika kulipia gharama za kuleta wataalamu kutoka RITES-India na kulipia gharama za ukarabati wa injini 10 aina ya 73xx, injini mbili aina ya 88xx, vigari vidogo (traction motor armatures) 20 na traction motor magnet frames 30.

Mzigo huo mkubwa wa madeni umekuja kufuatia serikali kulibinafsisha lililokuwa shirika la Reli la Taifa (TRC) mwaka 2006 kwa aliyeitwa “muwekezaji”– kampuni ya RITES kutoka India.

Ilibainika baadaye kuwa RITES haikuwa na uwezo wala sifa ya kuendesha shirika. Ilimilikishwa asilimia 51 ya hisa na serikali ikabaki na asilimia 49. Tayari serikali imevunja rasmi mkataba wake na RITES na imerejesha shirika hilo mikononi mwa umma.

Hata hivyo, kabla ya kuvunjwa kwa mkataba huo, serikali imelazimika wakubaliane na mwekezaji kulipa madai yake yote ambayo kampuni hiyo inasema yalitokana na mikataba mbalimbali ya kikazi kama ilivyokubalika kwenye majadiliano.

Kabla serikali kulirejsha shirika hilo mikononi mwake, ilibidi kuvunja mkataba wa mkopo wa dola za Marekani 44 milioni kutoka IFC.

“Kuvunjika kwa mkataba huu kungeiwezesha IFC kurejesha hisa asilimia 51 za RITES ambazo zilikuwa zimeshikiliwa kama rehani ya mkopo (Acknowledge and Consent Agreement),” inasema sehemu ya waraka unaonukuliwa.

“Baada ya makubalino hayo na IFC, serikali iliingia mkataba na RITES (Deed of Settlement) wa kulipa kwa awamu madai yake yote yenye jumla ya dola za Marekani 21,656,447.28 hapo tarehe 22 Julai 2011,” ameeleza mtoa taarifa akinukuu waraka.

Kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya Sh. 3.9 bilioni (dola za Marekani 2.63 milioni) ambazo zilitolewa na serikali kwa ajili ya kulipa sehemu ya madai ya kampuni hiyo kama sharti la kutiwa saini “hati ya makubaliano ya kuondoka kwa RITES.”

Pamoja na madai ya RITES, kampuni ya TRL inadaiwa pia na taasisi kadhaa za serikali na makampuni mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa nje, hadi kufikia 31 Mei 2010, madeni ya kampuni hiyo yalikuwa yamefikia jumla ya Sh. 32,735,013.32.

Haionyeshwi kati ya fedha hizo, ni kiasi gani kampuni inadai serikali na taasisi zake, wala dola za Marekani 20.7 milioni ambazo zinaonekana kwenye vitabu vya hesabu hazijulikani zinatokana na deni lipi.

Katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2011/2012, fedha zilizotengwa kuboresha miundombinu ya reli, ni Sh. 42.708 bilioni, kurudisha usafiri wa treni Sh. 29.68 bilioni na kulipia baadhi ya madeni Sh. 23.39 bilioni.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: