Ahmedinejad aapa kuendeleza madini ya uranium


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version
Ahmedinejad

KATIKA hotuba yake yenye kuonyesha jeuri na kiburi, Rais wa Iran,Mahmoud Ahmedinejad amesema nchi yake itaendelea kulimbikiza shehena ya madini ya uranium, ukiwa ni msimamo mpya dhidi ya wito wa kimataifa kutaka nchi hiyo iachane na mpango huo wa nyukilia.

Wataalam wanasema msimamo huo utaifanya Tehran kuwa na mpango wa kutengeneza silaha hizo kali ili kujihami na vita yoyote inayoweza kutokea siku zijazo.

“Ninatangaza hapa kwamba kwa baraka za Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litazalisha asilimia 20 ya mafuta na chochote kingine ambacho itakihitaji,” Ahmedinejad aliuambia umati wa watu waliokuwa wakimshangilia kila mara kwenye Jiji la Isfahan.

Mara kadhaa Iran imekuwa ikikanusha kuwa na mpango wa kutengeneza silaha za nyukilia. Hata katika hotuba yake Rais Ahmadinejad hakugusia mpango wowote wa kuyatumia madini ya uranium kwa ajili ya kutengeneza silaha hizo.

Ahmadinejad anasema kwamba Tehran iko tayari kwa kulimbikiza akiba yake ya madini hayo, ambayo sasa ni asilimia 3.5 hadi kufikia asilimia 20. Kwamba kiwango hicho ndicho kitahitajika kutengeneza mafuta kwa ajili ya utafiti wa kitabibu katika mji mkuu wa Iran.

Madini ya uranium yakilimbikizwa katika viwango vidogo yanaweza kutumika kama nishati kwa ajili ya nguvu ya nyukilia. Hata hivyo, yakilimbikizwa hadi kufikia asilimia 90 na zaidi yanaweza kutumiwa kwa ajili ya silaha.

Marekani na nchi nyingine tano zimekuwa zikijaribu kuishawishi Iran ili ikubali kusafirisha nje ya nchi hiyo kwa ajili ya kutengeneza mafuta kwa ajili ya utafiti wake.

Hiyo pekee itaiacha Iran, angalau kwa muda, bila kuwa na kiasi cha kutosha cha uranium kwa ajili ya kutengenezea mabomu. Hata hivyo, baada ya kuonyesha dalili za kukubaliana na wazo hilo mwezi Oktoba, bado Iran imeendelea na wazo lake la kutunza madini hayo nchini humo.

Jumatano iliyopita, Ahmadinejad alikwenda mbali zaidi, akiapa kwamba nchi yake italimbikiza madini ya uranium kwa ajili ya utafiti wake.

“Tuliwaambia tupeni asilimia 20 ya nishati inayohitajika kwa ajili ya vifaa vya utafiti,” kiongozi huyo wa Iran alisema akiwa jijini Isfahan na kuongeza, “badala yake walianza kutuongezea vikwazo.”

“Kwa hiyo, tuliwaambia ‘kama mkitaka kutupa mafuta, tutachukua. Kama sivyo,basi na waende zao’.”

Kiasi cha kilo 15 hadi 30 za uranium ikilimbikizwa hadi zaidi ya asilimia 90 kinaweza kutumika katika kutengeneza bomu la nyukilia. Mpaka sasa Irani ina kiasi cha kilo 1,500 ikiwa ni asilimia 3.5, likiwa ni limbikizo dogo, ambalo linaweza kutumika katika kutengeneza mabomu mawili.

David Albright wa Taasisi ya Sayansi na Usalama wa Kimataifa, iliyoko Washington, anasema mchakato wa kutoka viwango vidogo vya madini hayo hadi angalau asilimia 20 unaweza kuchukua miezi kadhaa.

Mtaalam wa nguvu za nyukilia ambaye amekuwa akifuatilia mipango ya atomiki ya Iran anasema kwamba nchi hiyo inaweza kulimbikiza madini ya uranium hadi viwango vikubwa katika miezi michache ijayo, baada ya kuvifanyia majaribio vifaa vinavyohusika na madini hayo.

Mtaalam huyo-ofisa wa serikali mojawapo kati ya mataifa matano ya kudumu katika Umoja wa Mataifa, alikataa kutaja jina lake kwa kuwa hakuruhusiwa kuzungumzia suala hilo.

Hotuba ya Ahmadinejad ni kati ya kauli kali za hivi karibuni kutolewa na taifa hilo la Kiislam, zikiwa ni kuonyesha kukerwa kwake na upinzani wa kimataifa dhidi ya msimamo wake kuhusu madini hayo.

Wiki iliyopita bodi ya kimataifa inayosimamia madini hayo ilipitisha azimio kutoka nchi sita-Marekiani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kufuatia upigaji kura.

Azimio hilo liliishutumu Iran kwa kupuuza marufuku iliyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusu ulimbikizaji wa madini ya uranium, na badala yake inapanua zaidi shughuli hiyo katika kiwanda cha Natanz. Iran pia inalaumiwa kwa kujenga kiwanda cha pili kwa siri na kuitaka isitishe mara moja mpango wake huo.

Pia taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa mkuu wa nguvu za atomiki, Mohamed El-Baradei, ambaye hivi sasa amejiuzulu, hajathibitisha kama mpango wa Iran unalenga katika amani.

Jumapili iliyopita, Ahmadinejad alitangaza kwamba Iran itajenga viwanda vingine 10 kwa ajili ya kushughulikia madini ya uranium, licha ya kuwapo imani nchini humo kuwa Iran haina rasilimali za kutosha kwa ajili ya kazi hiyo.

Ingawa Iran bado haijatoa msimamo wa kupinga rasmi pendekezo la Umoja wa Mataifa, la kuitaka kusafirisha nje madini hayo, kwa ajili ya utengenezaji zaidi, kauli ambazo zimekuwa zikitolewa hivi karibuni zinaashiria kuwa haikubaliani na mpango huo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, anasema kuwa pendekezo la Umoja wa Mataifa limekataliwa kabisa na Iran.

Mwanadiplomasia kutoka mataifa sita, Jumatano iliyopita alisema kuwa Marekani na washirika wake wa magharibi wanasubiri Marekani ionyeshe kutoivumilia Iran, jambo ambalo wanadhani linaweza kuibuka wakati wowote kuanzia sasa.

0
No votes yet