Aitwa diwani kabla ya uchaguzi


Sospeter Bandihai's picture

Na Sospeter Bandihai - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version

ANAJIITA diwani tayari. Wanachama wenzake wa Chama cha Wananchi (CUF) na wapambe, wote wanamwita diwani.

Huyu ni Kilama Christopher  Theobard,  mgombea udiwani kata ya Magata/Karutanga jimbo la Muleba Kusini.

Mwandishi: Kwa nini unajiita diwani wakati uchaguzi bado uko mbali?

Mgombea: Ni wananchi wanaoniita hivyo.

Mwandishi: Kwa nini usiwaelimishe kuwa hujawa diwani?

Mgombea: Siwezi, na wala sitaki kufanya hivyo. Hii ni kwa kuwa napenda kuwa diwani na wao wanaona udiwani ndani yangu.

Mwandishi: Kama wanaona udiwani ndani yako, kwa nini basi uliamua kugombea na usiwe diwani moja kwa moja?

Mgombea: Hilo sasa ni suala la kisheria na utaratibu. Ili niwe mtendaji, sharti nipite kwenye taratibu za kupigiwa kura na wao wanithibitishe kazini.

Theobard anasema wanaomwita diwani waliishaona zamani kuwa anafaa. “Wanajua ninavyowatetea au ninavyosimama nao kupinga udhalilishaji.”

“Chukua mfano huu. Mama mmoja alipeleka samaki kuuza kwenye gulio la Lambikiliza, hapa Magata. Mtendaji wa Kata akataka kumkamata eti kwa kufanya biashara isivyo halali. Mimi na wenzangu tuliingilia kati,” anaeleza.

Kuna matukio mengi ya unyanyasaji wa aina hii, anasema Theobard, ambao unawakabili akina mama, vijana na wazee na kwamba yeye amekuwa mstari wa mbele kuwasemea.

Mgombea ni mjumbe wa serikali ya kijiji Karutanga, mahali alipozaliwa miaka 43 iliyopita.

“Labda nikueleze moja ya sifa zangu. Sihongwi. Nasimama kwenye ukweli na haki. Ningekuwa nanunuliwa nisingekuwa katika kinyang’anyiro hiki,” anasema.

Anasema ukitumikia haki sharti uishi maisha ya haki na kwamba hicho ndicho anaahidi wapigakura wa Magata/Karutanga.

Theobard anasema wananchi wa Magata/Karutanga siyo wa kukunua pia. “Ni watu huru wanaotaka kuishi maisha huru na kuongozwa na haki,” anaeleza.

Kuhusu wananchi wengi vijijini kuwa woga; kutishiwa na wakati mwingine kuonewa; Theobard anasema ambacho amekuwa akifanya na atakachoendelea kufanya ni kuwapa wananchi ujasiri wa kujisimamia wao na haki yao.

Mwandishi: Utafanyaje katika hilo?

Mgombea: Nitasambaza elimu ya uraia juu ya haki za kila mmoja – mwanamke, mwanamume na mtoto.

Mwandishi: Lakini watu wengi shamba hawapendelei mafunzo ya aina hiyo…

Mgombea: Wewe! Nani amekudanganya? Hakuna anayekimbia ukombozi. Hata kama hawana chakula au fedha, kama wana uhuru wanaweza kufikiri jinsi ya kujikwamua. Huo ndio msimamo wangu.

Mwandishi: Una uhakika gani kuwa utashinda?

Mgombea: Wananchi wamesema watanipa kura, nami sina sababu ya kuwatilia shaka. Nimeomba kazi; sina vitimbi wala majivuno; ni mweupe wa moyo na matendo.

Alipoulizwa juu ya pingamizi lake dhidi ya mgombea wa CCM, alisema kwa ufupi, “Lingali na mgogoro. Mtausikia siku ukifumuka.”

Theobard ni mkulima wa mibuni na migomba ya kisasa (FHIA). Ni mashuhuri kwa kununua na kuuza ndizi kwa takriban miaka 26 sasa, shughuli ambayo imenufaisha wakazi wa Kata Magata/Karutanga na kata jirani.

Mgombea ameoa. Ana watoto sita – wasichana watatu na wavulana watatu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: