Ajali mv. Skagit: Watawala wangali usingizini


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

Meli mv Skagit inazama mchana kweupe; makumi ya wasafiri wazama nayo. Ni chini ya mwaka mmoja tangu meli ya Spice Islander I izame tukiwa tumelala. Ilikuwa usiku wa manane tarehe 10 Septemba 2012.

Nini maana yake? Si serikali ya Zanzibar wala ya Muungano Tanzania iliyojipanga sawasawa kukabiliana na janga linaloweza kutokea baharini au kwenye maziwa.

Kweli, ufumbuzi wa tatizo kubwa la ukosefu wa zana na wataalamu wa ukaguzi, uchunguzi na uokozi baharini na kwenye maziwa, haujapatikana.

Ni uthibitisho mwingine wa kile MwanaHALISI ilichogundua ilipotuma timu ya waandishi mapema mwaka huu kuchunguza usafiri na usafirishaji baharini na maziwani nchini.

Je, miundombinu katika nyanja hii ni imara? Zana zipo? Wataalamu wa ukaguzi na uchunguzi wapo? Viwango? Sheria na kanuni za usafiri na usafirishaji zinasimamiwa ipasavyo?

Hakuna zana za kisasa; hakuna wataalamu wa kutosha; wachache waliopo hawana mafunzo ya leo, kiasi kwamba baadhi yao hawajui nini wanatakiwa kufanya na wakati gani. Eneo la usimamizi wa sheria na kanuni ndilo linasikitisha.

Vyombo vinapakia abiria kupita uwezo, manifesto haziandaliwi ipasavyo. Ukiipata manifesto ni nusunusu – baadhi ya wasafiri, wakiwemo watoto, hukuti wameorodheshwa.

Yote haya alipata kusema ofisa mwandamizi wa serikali mwaka 1994. Akidurusu kadhia hii, Ali Ibrahim Muhina, alisema, “Hili ni tatizo sugu. Ufumbuzi wake utachukua miaka mingi.”

Alikuwa mkurugenzi wa bandari na usafiri baharini. Kwa kutambua umuhimu wa kuwepo miundombinu imara ili kukinga maafa na kuratibu shughuli za utafutaji na uokozi katika nchi ya visiwa, alisihi serikali itambue haya.

Ilikuwa katika mada aliyoiita, “Maandalizi ya kukabiliana na majanga ya baharini, shughuli za utafutaji na uokozi Zanzibar” kwa warsha iliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Kwa zaidi ya saa mbili, tangu taarifa za kuzama mv Skagit kufikia uongozi wa juu wa serikali Zanzibar saa 7.30 mchana, huduma za uokoaji hazikufikia wenye shida haraka.

Hata pale wakubwa walipoamua kujali, walipeleka boti iliyojaa maofisa wa serikali waliovalia suti na tai huku wazamiaji wachache wakiwa bila ya vifaa vya kisasa vya kuokolea.

Ni boti ya Kilimanjaro III. Humu kulikuwa na maofisa waandamizi wa serikali na wazamiaji.

Mmoja wa wazamiaji anasema: “Baadhi yetu tulikosa vifaa vya kutusaidia kazi… unajua hii ni kazi ya hatari, inataka uwe umejiandaa ili umsaidie mtu utakayemkuta, vinginevyo ni kwenda matembezi.”

Anataja zana za uokoaji: viatu, vioo vya kujikinga na maji na uchafu, mashine ya kuhifadhi maisha ya binadamu chini ya bahari (chamber), vifaa vya uzamuaji (lifting bag), nguo za kuogelea na mashine ya kujazia hewa (compressor).

Jeshi la polisi Zanzibar, lina kikosi cha askari wanamaji – Police Marine. Wanazo boti mbili ndogo (fibre), zinazotumia mashine ambazo hufungwa nje ya chombo.

Moja ya boti hizi ilipelekwa kwenye tukio. Haikufika kwa kukosa mafuta. Nimeelezwa baadhi ya askari wanajifunza kuogelea.

“Sikiliza, inaonesha kupelekwa (kuhamishiwa) pale ni adhabu. Hakuna vifaa labda kioo kimoja na pea ya kiatu cha kuzamia. Boti zenyewe siku zote unakuta hazina mafuta. Wazamiaji hawana ujuzi na hawalipwi posho yoyote.”

Wale wachache waliosomeshwa na serikali, wanazuiwa kwenda kujiendeleza DMI licha ya kuomba mara kwa mara.

DMI ni Dar es Salaam Marine Institute, chuo cha kufundisha mabaharia kilichopo bandarini Dar es Salaam, kando ya barabara ya Sokoine.

Mapema mwaka huu, askari kadhaa wa kitengo hiki, walihamishwa makao makuu bandarini Malindi, na kupelekwa kituo cha Mkokotoni. Kule kuna bandari ndogo, bali hakuna chombo wala vifaa.

Boti mbili za Police Marine hazina utaratibu wa kufanya doria kwa kile ambacho wanaojua wanaita, “ukiritimba wa uongozi wa juu wa jeshi.”

Wanatuhumu wahusika wanashikilia kila kitu ikiwemo mafungu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuendesha kitengo na shughuli zake.

Hakuna fungu la matumizi linalotolewa kwa ajili ya kikosi hiki. Wala hakuna posho wanayolipwa askari wanamaji. Kila wanapoomba mafuta ili waendeshe doria kutumia boti hizo, wanabezwa.

Maana yake kwa muda mrefu sasa hakuna mazoezi ya mara kwa mara ya uokoaji. Ndio maana, taarifa zinasema, baadhi ya askari wazamaji wana woga wa kuzamia.

“Inasikitisha tunavyofanya mchezo na maisha ya watu... hii nchi inajulikana kabisa kuwa ni ya visiwa. Unashindwa kujiandaa kuokoa watu. Ni hatari. Katika hali kama hii utamuokoa nani,” anahoji msiri wangu.

Hata boti za Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), maalum kwa shughuli za majini, zinakabiliwa na uhaba wa mafuta.

Kikosi hiki kinatunzwa sana. Hotuba ya makadirio ya matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, iliyosomwa barazani 9 Juni, inasema asilimia 88.3 ya fedha ziliombwa kwa ajili ya huduma za utawala kwa mwaka 2011/12.

Waziri Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini aliliambia baraza ofisi hiyo ilipatiwa Sh. 6.082 bilioni, na Sh. 200 milioni kwa kazi za maendeleo kufikia Machi mwaka huu.

Alisema kwa KMKM, walinunua vifaa vya uzamiaji: suti na mitungi ya gesi; boti tano aina ya fibre na mashine zake pamoja na vifaa vya mawasiliano (Radio Base Station). Vyote hivyo ni kwa ajili ya usafiri wa wazamiaji.

Anasema serikali imepanga kuimarisha huduma ya uzamiaji kwa kununua mashine ya kuhifadhi maisha ya binadamu chini ya bahari (chamber), vifaa vya uzamuaji (lifting bags), nguo za kuogelea na mashine ya kujazia hewa.

Yanayotokea yanathibitisha boti hizo na vifaa hutumika zaidi kufukuza waendesha magendo ya karafuu.

Zanzibar haina chuo cha kufundisha wazamiaji. Kwa hivyo, ile rai aliyoitoa Ahmed Khamis (Kipande), aliyefuzu mafunzo ya juu ya uzamiaji nchini Uingereza mwaka 1978, ya kuanzishwa chuo ili afundishe wazamiaji vijana, haijatekelezwa.

Wakati serikali imeunda kamati mbili za kutafiti uanzishwaji wa chuo hicho pamoja na cha usafiri wa anga, matendo yanaonyesha itachukua miaka kufanikiwa.

Serikali tayari imefunga utafutaji waliozama baada ya watu 146 kuokolewa na 68 kukutwa wamekufa. Kwa takwimu zake kuwa mv Skagit ilichukua watu 290, ina maana 76 wamezama na meli.

Jumapili jioni, wavuvi waliokota maiti sita, ikiwemo ya mtoto na kuwafikisha bandarini. Walizubaa nao kwa saa kadhaa kabla ya kumpata ofisa wa serikali kukabidhi.

Aidha, wafanyakazi wa Kilimanjaro III, boti iliyokuwa ikienda Zanzibar kutoka Dar es Salaam, walikuta maiti wapatao watatu wakielea eneo la Chumbe, karibu na ilipozama mv Skagit. Serikali imefunga usakaji!

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)