Ajali ya MV Faith: Majibu ya uchunguzi yasije peke yake


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MMILIKI wa mv Fatih, Said Abdulrahman maarufu kwa jina la Said Mbuzi, analalamika ametengwa kimaamuzi tangu meli hiyo ilipofidikia na kuzama tarehe 29 Mei.

Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZSC), Mustafa Aboud Jumbe anasema kazi ya kuokoa watu na kutoa meli chini ya maji imekuwa ngumu kwa sababu mmiliki hakutoa mchango wa kutosha.

Kulingana na magazeti niliyosoma, Said, mfanyabiashara binafsi, ndiye aliyetangulia kutoa kauli; Mustafa ambaye ni ofisa mwandamizi wa serikali, akafuata.

Jitihada nilizofanya kuzungumza nao zimeshindwa. Sikufanikiwa kupata simu ya Said, na ya Mustafa, Na. 0777 411711, haikupokewa kila nilipopiga mara nne siku tatu tofauti.

Washuhudiaji wamenieleza bandarini paliwekwa ulinzi mkali ili pamoja na mambo mengine, kudhibiti uingiaji holela wa watu baada ya kutokea wizi wa mali zilizokuwa melini.

Polisi ambao siku hizi wamekuwa hodari wa kutumia silaha kwa raia kuliko kwa wahalifu, walifyatua risasi hewani asubuhi ya 30 Mei ili kupunguza watu bandarini.

Ninaona uhusiano usioridhisha kati yao au na baina ya Said na serikali. Inawezekana sababu kubwa ni kauli ya mwanzo kabisa ya nahodha wa mv Fatih, Ussi Ali, baada ya ajali.

Baada ya kugundua hitilafu na kupima hali ilivyo, nahodha aliomba mapema wafanyakazi wa Kitengo cha Uongozaji Vyombo (Control Tower) bandarini Zanzibar wamruhusu kushusha abiria na mizigo eneo la Forodhamchanga.

Alihisi inaweza kuwa tatizo akienda gati kuu ambako angelazimika kupandisha ngazi tunayoambiwa ilikatika na meli kukosa uwiano ndipo ikafidikia.

Alikataliwa na kusisitizwa aingie gatini na kutia nanga.

Haya ni mambo yanayochunguzwa. Ila mtu anaweza kuamini kauli ya nahodha maana historia mbaya ya chombo hiki inathibitisha kimekuwa na matatizo ya kiufundi kwa muda mrefu.

Akili ya kawaida inakubali kwamba kwa kuwa Forodhamchanga ni eneo la karibu kutokea Dar es Salaam kuliko Malindi ilipo gati kuu, meli ingenusurika kufidikia. Hilo la kwanza.

Lipo tatizo jingine. Baada ya meli kufidikia na kuzama, hapakuwa na hatua za dharura kwa wakati.

Nilisema viongozi walikuwa wamelala fofo hivyo watu waliowahi eneo la tukio wakajikuta wanatumbua macho tu kwa kukosa kiongozi wa kuongoza shughuli za uokoaji.

Bado nahimiza awepo kiongozi wa serikali wa kuwajibika kwa kasoro hii kubwa.

Zaidi ya hapo, inaumiza kuarifiwa kuwa huenda wafanyakazi waliopo Control Tower hawana uwezo wa kazi wanayopaswa kuifanya.

Wale waliokuwepo wakati mv Fatih inatoka eneo la maji ya upande wa bandari ya Dar es Salaam, maeneo ya kisiwa cha Chumbe, hawakuwajibika ipasavyo baada ya kuelezwa tatizo.

Inawezekana hawakupeleka ushauri wa nahodha kwa viongozi wao wa kutaka aipeleke meli Forodhamchanga. Hii ni kasoro nyingine kubwa.

Imethibitika sasa kuwa wakati meli ilipoingia gatini Malindi, taa za usalama zililala fofo; labda zimezimwa kusudi au hazipo. Ushuhuda kwamba taa za gari ndio zilisaidia kuleta mwanga, haujafutwa na serikali.

Penye bandari inayotajwa kama ni “Bandari Huru” panahitajika vifaa na zana makini. Bandari yetu inapokea meli kubwa za mizigo kutoka ughaibuni. Kuzihudumia kunahitaji zana imara na mazingira yanayoruhusu kuwepo huduma kwa saa 24.

Kwa kuwa yetu ni “Bandari Huru” inayopokea meli kubwa za mizigo, haiwezekani pakosekane kikosi kabambe cha wazamiaji tena chenye vifaa vya kisasa. Ni aibu abiria kuokolewa na wapagazi wa Nungwi, Mkwajuni na Matemwe.

Eti wale wa serikali walifika bila ya taa za kuzamia chini ya maji. Wapagazi wa Kitumbatu waliofanikiwa kuokoa watu, ni wajuzi wa kuzamia majini bila ya taa.

Haya ni mambo ambayo si tu yanahitaji majibu, bali majibu yanayofuatana na viongozi husika kuacha kung’ang’ania ofisi. Waoneshe uwajibikaji, maana kamba imekatika.

Zipo taarifa kwamba kuna kiongozi wa juu alitoa agizo la kuzuia hatua zozote kuchukuliwa mpaka “serikali” iseme. Kwa staili ya utendaji ya viongozi wa kisiasa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hili linawezekana.

Mwaka 2003 palipotokea tatizo kwenye kituo cha kupokelea umeme wa Kidatu cha Fumba kutokea Ras Kilomoni Dar es Salaam, uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ulisema walikataliwa kuharakia eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.

Badala yake, SMZ ikaagiza wataalamu wa umeme kutoka nchini Norway. Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid alikuja kukiri hali hii kwa maelezo kuwa palitakiwa wataalamu walioshiriki kufunga mitambo kituoni Fumba.

Hii ni kasoro kubwa. Hakuna namna utaalamu waliotoa wazungu kutoka kwao, waondoke nao kama vile walikuja kufanya kazi hiyo kwa hisani. Hata kama ni kwa hisani, serikali ilipaswa kukomaza utaalamu huo kwa mafundi wazalendo.

Ndio maana wazamiaji 40 kutoka kikosi cha wanamaji cha JWTZ Kigamboni walifika Zanzibar siku tatu baada ya tukio. Hii ni fedheha.

Serikali ilianzisha kitengo cha usajili wa meli chini ya Mrajis. Huyu anatakiwa kushughulikia pia ukaguzi wa meli na vyombo vingine anavyovisajili.

Nani wa kulaumiwa iwapo mv Fatih imekuwa ikitembea baharini – kati ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam – huku ikiwa mbovu hadi inaleta maafa kwa taifa? Fedheha.

Mkurugenzi wa Bandari, Mustafa, alipata kumjibu Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, aliyefika bandarini kutathmini hali, kuwa hakuhitaji msaada maana kila kitu kipo. Aibu gani hii?

Nilidhani serikali ilipowatii wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliokataa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) itaanzisha Sumatra yake na kuipatia watendaji wajuzi na vifaa vya kufanyia kazi.

Ni fedheha nyingine serikali kufukuza SUMATRA wa Dar es Salaam kwa kuweka ‘ZUMATRA’ wasio ujuzi wala vifaa. Huko ni kuchezea maisha ya watu na mali zao.

Nilimtafuta Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Masoud ambaye siku hizi yupo chini ya Ofisi ya Rais, kupitia simu yake Na. 0777 416295 lakini iliita bila kupokelewa.

Wakati mambo yanachunguzwa; kila mtu atafakari hali hii na kujiuliza hadi lini maisha ya watu yatawekwa rehani huku viongozi wa serikali na taasisi zake wakiendelea kukataa kuwajibika?

Tumeona malalamiko ya mwenye meli, uzembe wa watendaji wa Shirika la Bandari na kushindwa kazi kwa viongozi wa kisiasa katika serikali, hivi bado tusubiri uchunguzi?

Viongozi wenye moyo hawasubiri uchunguzi bali huondoka mara tu inapotokea kasoro na ikawa imesababisha maafa kwa taifa. Mtumishi muadilifu, hutoka kabla ya kutolewa. Watoke basi!

0
No votes yet