Ajali ya Mwakyembe yatatanisha zaidi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Yasheheni madai mazito
Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe

AJALI ya gari iliyomhusisha Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe imeanza kuibua mengi, MwanaHALISI limegundua.

Joseph Msuya, dereva wa Mwakyembe, amenukuliwa akisema askari wa Usalama Barabarani (trafiki) hakuwa wa msaada wowote kwake na Mwakyembe ambaye alikuwa bado hajajitambua.

Gazeti hili limeelezwa kwamba trafiki huyo alikuwa akisimamisha magari, akionyesha kuwa anataka yasaidie majeruhi kwenda Iringa, lakini alikuwa akiyaruhusu yaondoke bila kutoa huduma hiyo kwa sababu ambazo hazijafahamika hadi sasa.
 
Gari ambalo hatimaye lilitoa msaada kwa Mwakyembe lilisimamishwa na dereva wa mbunge hyo baada ya kuona “kulikwa na mchezo wa kuigiza.”

Taarifa zilizozagaa kwenye eneo la ajali, kabla na baada ya Mwakyembe kujitambua, zinasema trafiki huyo alikuwa amemwambia dereva Msuya kuwa yeye aende kupata matibabu hospitalini Iringa mjini “kwa vile Mwakyembe alikuwa tayari amefariki.”

Hata hivyo, Msuya alipoulizwa juu ya kauli hiyo alisema, “Sina la kuwaambia sasa hivi. Sina la kusema… Kama lolote basi tusubiri kutoka vyombo vya sheria.” Hakukanusha kusikia au kuambiwa hayo.

Taarifa hizo ambazo hazikuweza kuthibitishwa zinasema ushauri wa trafiki ulifanywa wakati Mwakyembe alikuwa hana fahamu na alionekana kama aliyekufa.

“Lakini kwa bahati nzuri, Dk. Mwakyembe alipata fahamu na kuanza kukohoa na ndipo hata trafiki huyo aliposhindwa kuendeleza ushawishi wake wa kutaka mbunge huyo atelekezwe," zimeeleza taarifa.

Trafiki alikuwa mmoja wa trafiki wawili waliokuwa wakisafiri kwa gari aina ya Coaster lililokuwa likitoka Iringa, na lilipishana na gari la akina Mwakyembe lililokuwa linaelekea Dar es Salaam.

Mwakyembe, akiwa katika gari lake aina ya Toyota Lancruiser, Na. T 362 ACH, Alhamisi iliyopita, alipata ajali eneo la Ihemi, mkoani Iringa na kupata mstuko wa shingo wakati dereva wake, Msuya alipata michubuko mwilini.

Taarifa za mwishoni mwa wiki iliyopita zinasema polisi kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam walikwenda nyumbani kwa Mwakyembe wakitaka kumchukua dereva Msuya kwa madai kwamba “wanataka kwenda naye kwenbye eneo la tukio, lakini ndugu zake waliwakatalia.

“Hatuwezi kumruhusu atoke hapa. Wanamtaka aende kufanya nini? Kama ni suala la vipimo, basi polisi wa iringa tayari waliishapima. Hatoki hapa,” ameeleza mmoja wa wanafamilia akinukuu mjadala uliojitokeza kati ya polisi wa ndugu zake nyumbani kwa Mwakyembe.

Msimamo wa familia unafuatia kutofautiana kwa maelezo ya polisi na maelezo yale ya mwakyembe na dereva wake.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi, amenukuliwa katika vyombo vya habari nchini akisema gari la Mwakyembe lilianguka kutokana na kile alichoita “uzembe wa dereva.”
 
Nyombi amekaririwa akidai kuwa uzembe huo wa dereva ulitokana na mwendo wa kasi ambao unadaiwa kumfanya ashindwe kumudu gari hilo.
 
Hata hivyo, maelezo ya Nyombi yanatiliwa mashaka kwa vile taarifa zinasema gari la Dk. Mwakyembe liliangukia upande wa kushoto; kwa maana kuwa lilikuwa limefanikiwa kulipita lori lililokuwa mbele yake.
 
Zaidi ya hayo, polisi wa usalama barabarani hawakuweza kusimamisha na kutambua lori hilo, ambalo Dk. Mwakyembe na dereva wake wanasema ndilo lilisababisha ajali. Ni hali hii inayozidi kujenga mashaka juu ya taarifa ya Kamanda Nyombi.
 
Hadi gazeti linakwenda mtamboni, hakukuwa na taarifa zozote juu ya lori hilo, dereva wake wala mmiliki wake kukamatwa na kuhojiwa na polisi.
 
Vilevile, hatua ya polisi kutoa taarifa ya ajali hiyo hata kabla uchunguzi kamili haujafanyika, imejenga mashaka na kufanya wengi wahoji kama hakuna kinachozibwazibwa.
 
Polisi walitoa taarifa Alhamisi jioni, siku ambayo ajali ilitokea, wakisema hakukuwa na mchezo wowote mchafu katika tukio hilo.
  
Hata hivyo, maelezo ya Dk. Mwakyembe, dereva wake na taarifa kwamba trafiki hawakutoa msaada zinazidi kuweka giza katika tukio zima la ajali hiyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: