Aliyechukua serikali ya Kikwete airudishe


Boniphace Kamalamo's picture

Na Boniphace Kamalamo - Imechapwa 06 May 2008

Printer-friendly version
Waziri Sophia Simba

KUNA kila dalili kwamba serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeelemewa. Wananchi wanauliza, "Mbona serikali yetu inakwenda kama imechukuliwa na msukule!"

Hata Rais Jakaya Kikwete, hawezi kukana wazi jambo hili. Hawezi kusema serikali yake bado iko imara. Maana anajua kuwa tayari mawimbi yameiyumbisha na yeye amebaki mpweke.

Ndani ya jahazi la serikali ya Kikwete, kuna mawaziri wasiozidi 15 ambao ndio wanaoweza kusafiri na rais hadi mwisho. Ndiyo wenye uwezo, siha na nguvu ya kutetea serikali.

Wengine wote waliosalia, wanahesabu siku za kutokomea. Wanafahamika hata kwa majina. Baadhi yao wametajwa mara kadhaa kwamba wamechoka tangu asubuhi.

Ikiwa sasa serikali inatimiza nusu ya kipindi chake uongozi cha miaka mitano, inaonekana serikali imesahau hata ajenda yake iliyoingia nayo madarakani.

Ajenda ya kupambana na ufisadi na uharamia mwingine uliojikita nchini, haikuwa ajenda ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hiyo ilikuwa ajenda ya vyama vya upinzani.

Serikali ya CCM iliamua kuidandia hoja hiyo baada ya kushindwa kustahimili shinikizo la wananchi.

Wengi wao bado wanakumbuka jinsi serikali ya Kikwete, ilivyopindisha hoja ya mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, kuhusiana na sakata la ufisadi ndani ya Benki Kuu (BoT) mwaka jana.

Serikali ikitumia kile inachopenda kuita "rungu la wabunge wa CCM," ilifyeka hoja ya Dk. Slaa na kuitokomeza. Ndiyo chanzo, au sababisho la Slaa kupeleka hoja hiyo kwa wananchi kupitia mkutano wa hadhara.

Lakini leo, ikiwa ni takribani miezi 10 tangu hoja ya Dk. Slaa ikataliwe kwa rungu la Spika wa Bunge, Samwel Sitta, serikali imejikuta ikibeba hoja hiyo na kuifanya hoja yake.

Matokeo yake, serikali inapatwa na kigugumizi katika kushughulikia mafisadi. Baadhi yao wanasema kigugumizi cha serikali kinatokana na kubeba hoja isiyo yake.

Hali hiyo inatajwa kuwa ndiyo iliyozalisha serikali mbili, ndani ya serikali moja na ndani ya chama kimoja.

Wakati serikali moja inasema rais mstaafu Benjamin Mkapa, aachwe apumzike, nyingine inasema, "itamchunguza Mkapa."

Ukiangalia mlolongo wa mambo na jinsi yanavyoshughulikiwa na watawala, mara moja utabaini kwamba serikali imezidiwa.

Kwa mfano, serikali haijasema lolote ambalo wananchi wanataka kusikia kutoka serikali yao kutokana na tuhuma za kulimbikiza fedha nje ya nchi ambazo zinamkabili Andrew Chenge.

Tayari imefahamika kwamba baadhi ya fedha hizo amehifadhiwa katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Makao Makuu.

Ndani ya NBC pekee, Chenge amehusishwa na kusimamia au kuwa karibu na Sh.16 bilioni. Nyingi ya fedha hizo ni kupitia akaunti ya kampuni ya Tangold ambapo Chenge anatajwa kuwa mkurugenzi.

Tayari Chenge mwenyewe amethibitisha kuwa karibu na kiasi hicho cha fedha, lakini anasema "Tangold si kampuni yake, bali ni kampuni ya serikali."

Hata fedha zilizokutwa katika akaunti yake nchini Uingereza, anasema hazihusiani na mlungula wa rada kama ainavyodaiwa.

Hadi sasa, serikali haijasema chochote cha maana kuhusu utajiri wa Chenge. Badala yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sophia Simba anasema, "labda mwenzetu (Chenge) ameuza ngombe wote wa kwao."

Simba wala haonyeshi mshutuko pale anaposikia kiongozi wa umma anatuhumiwa kulimbikiza mabilioni yote hayo katika mazingira ya kutatanisha.

Pamoja na kwamba Simba anajua kwamba Chenge hawezi kuthibitisha mahali popote kuwa yeye ni mfanyabiashara mkubwa mwenye uwezo wa kumiliki mabilioni yote hayo, bado inaonekana kuwa analeta mzaha katika mambo muhimu.

Hii ni kwa sababu Simba si miongoni mwa watu wanaoguswa na matatizo ya Watanzania; matatazo ambayo chimbuko lake ni taifa hili kuwa na watu wanaopora fedha za umma.

Simba anajua kuwa Chenge hawezi kuthibitisha mahali popote kuwa ni mfanyabiashara, anayeweza kumiliki kiasi hicho cha fedha.

Lakini pamoja na jambo hilo kuwa la wazi, lakini serikali haitaki kuchukua hatua dhidi ya mhusika. Badala yake, inaendelea kuhubiri kwamba inasubiri ripoti ya uchunguzi kutoka Shirika la Upelelezi la Uingereza (SFO) ili iweze kuchukua hatua.

Haya si maelezo yanayoweza kutosheleza kiu ya wananchi wanaokesha kulinda rasilimali za taifa lao. Maelezo haya yanastahili kutolewa katika vijiwe vya kahawa na bao.

Maana wakati Chenge anasema, Tangold ni mali ya serikali; kiasi cha Sh. 16 bilioni zilizorundikwa katika benki ya NBC si zake ni za serikali, taarifa zilizopo katika ofisi ya Wakala wa Msajili wa Makampuni nchini (BLERA), zinaonyesha kwamba Tangold haiwezi kuwa kampuni ya serikali.

Hii ni kwa sababu, Tangold ilisajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius na baadaye kuandikishwa nchini kama tawi la kampuni ya kigeni.

Hata katiba yenyewe ya Tangold inathibitisha hilo. Kifungu cha 7 (e) cha Katiba ya kampuni hiyo kinaruhusu wanahisa wake kumilikisha hisa zao kwa wanandoa, baba, mama, watoto na wajukuu.

Sasa kama serikali inakubaliana na uwongo wa Chenge kwamba Tangold ni mali ya serikali, yuko wapi, baba, mama na mwanandoa wa serikali, ambao wanaweza kumilikishwa hisa hizo?

Hii ina maana kwamba kama serikali haishirikiani na Chenge kuudanganya ulimwengu, basi Chenge atakuwa na ngekewa ya hali ya juu ya kumiliki mali na kudanganya kuwa ni ya serikali.

Hakuna mahali popote duniani ukiondoa Tanzania, ambako serikali inaweza kuchezewa kiasi hiki.

Ni hapa tu, ambapo waziri wa serikali anaweza kusimama bungeni na kuliambia taifa uwongo. Ni Tanzania pekee, ambapo waziri anaweza kula njama na mafisadi, na wabunge wakanyamaza kwa kisingizio cha kulinda chama kilichopo madarakani.

Hili lilifanywa na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, pale alipoliambia Bunge kwamba Tangold ni mali ya serikali wakati hisa zake zinaweza kugawiwa kwa baba, mama na mtoto.

Kutokana na hali hiyo, ukichanganya na hali inavyokwenda ndani ya serikali, mara moja utabaini kwamba wengi wa mawaziri wa Kikwete, hawawezi kumsaidia bosi wao.

Wengi wao, ama wameshiriki, au wamenyamazia ufisadi unaofumuka sasa.

Hakuna ubishi kwamba utajiri huu kwa Chenge, ni sehemu tu ya tone la maji katika bahari. Taarifa hizi, hazizungumzii hata chembe mali zake nyingine ikiwamo nyumba zinazodaiwa kutapakaa kila pembe ya jiji la Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, kimya cha serikali kinathibitisha madai ya wengi, kwamba Chenge hayupo pekee yake katika hili. Kuna msululu wa watu nyuma yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: