Aliyosema Mwalimu Nyerere sasa yametimia


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Gumzo

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kukionya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kuwa “chama legelege, huzaa serikali legelege.”

Kile ambacho Nyerere aliita legelege, kilitokana na alichoona wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi. Alikuwa akikemea serikali kwa kushindwa kukusanya kodi.

Nyerere hakukomea hapo. Alikemea pia mtindo wa “…kugeuza ikulu kuwa pango la walanguzi” na serikali kukumbatia watu wenye fedha.

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili, neno legelege lina maana: dhaifu, siyo imara, a kulegea.

Leo hii, kauli ya Mwalimu imethibitishwa kwa vitendo, kuwa CCM ni chama dhaifu, legelege na hivyo kimeunda serikali legelege.

Moja ya sifa kuu ya serikali legelege, ni kushindwa kutekeleza kile inachoahidi; kutokuwa na kauli moja kwenye jambo lilelile; kushindwa kulinda raia wake na kutaka kusafishana hata kwa yale ambayo kila mmoja anaona kuwa hayasafishiki.

Hivyo ndivyo Rais Jakaya Kikwete na chama chake wanavyofanya sasa. Wameshindwa kutekeleza ahadi ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania.”

Wameshindwa kutekeleza ahadi walizozitoa wakati wa kampeni – ujenzi wa reli ya kati, barabara zikiwamo zile za juu, ununuzi wa meli za kisasa Ziwa Viktoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika; na uboreshaji huduma za jamii.

Aidha, Kikwete aliyeasisi kauli mbiu ya kujivua gamba ili kukinusuru chama na viongozi walio mzigo kwa chama hicho, ameshindwa kusimamia kauli yake hiyo.

Siyo tu kwamba aligeuziwa kibao na kuonekana yeye pia ni “gamba la kuvuliwa,” isipokuwa vikao vya maamuzi vya chama chake vilimeguka vipande na kukifanya chama kishindwe mpaka sasa, kuchukua hatua dhidi ya wanachama wanaokichafua mbele ya jamii.

Pamoja na kelele zote zilizopigwa, hakuna hata mtuhumiwa mmoja wa ufisadi aliyefukuzwa kwenye chama mpaka sasa.

Ni Rostam Aziz pekee, miongoni mwa watuhumiwa wa wazi, ambaye amejiuzulu. Hakufukuzwa. Ulegelege wa CCM umeifanya dhana mzima ya kujivua gamba kubaki kuwa mchezo wa kuigiza.

Wilson Mukama, katibu mkuu wa chama hicho, anadai dhana ya kuvua gamba ilipotoshwa na vyombo vya habari, kwa kufanya ionekane iliwalenga baadhi ya watu tu; wakati ililenga kusafisha chama chote na kwenye ngazi zote.

Wengine wanadai hata muasisi wa dhana yenyewe, Rais Kikwete – hajui alimaanisha nini na kama anajua anaogopa kusema hasa alimaanisha nini.

Vilevile, serikali legelege, hujulikana kwa viongozi wake kutoa kauli tofauti kwa jambo moja. Serikali dhaifu huwa haina ushupavu wa kusimamia kauli moja kwa jambo moja.

Sikiliza kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyoitoa bungeni kuhusu mgomo wa madaktari nchini. Halafu soma hotuba ya Rais Kikwete juu ya somo hilihilo iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari, tarehe 1 Julai 2012. Ni vitu viwili ambavyo haviwezi kukutana – mithili ya mbigu na ardhi.

Pinda ameliambia bunge kuwa serikali imesitisha uamuzi wake wa kulizungumzia jambo hilo kwa kile alichodai, “…kuna shauri limefunguliwa mahakamani.”

Lakini Kikwete katika hotuba yake, ameibuka na kuzungumzia jambo hilohilo ambalo Pinda amesema serikali haiwezi kujadili.

Katika hotuba yake, Kikwete amesema hata yale ambayo yatakuwa msingi wa kesi na utetezi. Mathalani, Kikwete anasema, mgomo huu ni batili kwa kuwa mahakama kuu, divisheni ya kazi, imeagiza mgomo usitishwe.

Bali Kikwete anajua kuwa ni serikali iliyokwenda mahakamani kushitaki chama cha madaktari (MAT). Lakini mgomo huu siyo wa MAT. Umeitishwa na jumuiya ya madaktari.

Hivyo, kwa mtu makini aliyemsikiliza Pinda na kisha kusoma hotuba ya Kikwete, hakika anaweza kudhani viongozi hawa wawili, wanatoka katika nchi mbili tofauti.

Hakuna anayeweza kusema Kikwete ni rais na Pinda ni waziri mkuu. Hakuna anayeweza kusema, wawili hawa wanatoka katika chama kimoja. Ulegelege wa aina hii, umevuka kiwango.

Lakini ukiacha hilo, kuna hili pia: Kikwete amekana kuwa serikali yake, vyombo vyake vya dola – polisi na usalama wa taifa – hawahusiki na kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya madakatari nchini, Dk. Steven Ulimboka.

Amesema, “Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu;” kwamba hawajazoea mambo hayo. Anasema ameeleza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ufahamike.

Hata hivyo, Kikwete amekiri kuwa serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Anajitetea kwa kusema, “Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya serikali kufanya hivyo.”

Kwanza, siyo kweli kuwa serikali – kwa maana ya watumishi wake wa ngazi ya juu – haijawahi kushiriki katika vitendo kama hivi. Imeshiriki.

Mfano hai na ambao umethibitishwa mahakamani, ni mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka mkoani Morogoro na dereva teksi mmoja, mkazi wa Manzese Dar es Salaam.

Tarehe 14 Januari 2006, Sabinus Chigumbi (Jongo), Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi Juma Ndugu, waliuawa kinyama katika msitu wa Pande, wilayani Kinondoni, wakiwa mikononi mwa polisi kwa kile polisi walichodai walikuwa majambazi.

Polisi walijitahidi kupaza sauti kwa nguvu kutaka kuaminisha umma kuwa wafanyabiashara hao walikuwa majambazi sugu.

Ni tume huru ya Jaji Musa Kipenka, iliyofichua kila kitu kuhusu ujambazi wa polisi wa kushiriki katika mauaji ya wafanyabiashara hao na kisha kutaka kuficha ukweli.

Bila tume ya Jaji Kipenka, ukweli huu usingepatikana.

Kuthibitisha kuwa polisi walikuwa na nia ovu, mpaka sasa wameshindwa kumfikisha mahakamani Koplo Saad Alawi, mmoja wa watu muhimu kwenye kesi ya mauaji ya wafanyabiashara hao.

Koplo Saad aliyetoweka ghafla mara baada kutekelezwa kwa mauaji hayo, jeshi la polisi linasema “hajulikani aliko!” Kumbuka, serikali ndiyo hujigamba kuwa ni “mkono mrefu!”

Mtuhumiwa huyu, ndiye Jaji Salum Masati alisema, katika uamuzi wake, kuwa kukosekana kwake kumechangia kwa kiwango kikubwa watuhumiwa waliofikishwa mahakamani kuachiwa huru.

Hakuna anayejua kama ametoroka au polisi wamekula njama ili kuharibu ushahidi. Lakini kwa vyovyote vile; kwa intelijensia ya polisi, wanajua aliko Koplo Saad.

Hata hili la Dk. Ulimboka limeanza kuchukua sura hiyo. Baadhi ya viongozi wa serikali na jeshi la polisi wanataka kuaminisha wananchi kuwa Dk. Ulimboka ameshambuliwa kutokana na “mambo binafsi.”

Bahati njema mpaka sasa, Mungu naye ana mipango yake, Dk. Ulimboka bado yuko hai. Tayari amenukuliwa akisema baadhi ya yale yaliyomkuta. Amemtaja anayemhisi ndiye kinara wa mipango hii.

Kwa kauli yake na kwa jinsi alivyoshambuliwa, siyo watu wa mtaani waliomshambulia Dk. Ulimboka.

Siyo watu wenye ugomvi binafsi. Siyo watu waliokasirishwa na mgomo kwa madai kuwa ndugu zao wanateseka.

Waliomshambulia Dk. Ulimboka, ni watu maalum waliotumwa kwa kazi maalum.

Njia pekee ya kuondoa kiza hicho, ni Rais Kikwete kukubali na kuunda tume huru, ya watu huru; wasio na vitendo, fikra wala harufu ya minyororo ya serikali.

Vinginevyo wananchi na dunia nzima, wataamini kuwa serikali ya Rais Kikwete imeshiriki katika kile kinachoitwa “mbinu chafu za kuficha ukweli wa kilichotokea kwa Dk. Ulimboka.”

Tume iliyoundwa na kamanda wa polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemani Kova, haiwezi kufanya kazi hiyo. Hawaweza kujichunguza.

Kanuni inasema, uchunguzi wa aina ambayo Kova anataka kufanya, hufanywa kwa kutafuta kuepusha matokeo fulani yasiyohitajika.

Lakini baada ya tukio kama hili, la ushenzi katikati ya ustaarabu, tume inayoundwa huwa ya watu huru na ambao hawamo katika mkondo wa kuhisiwa wala kutuhumiwa. Tunaikataa tume ya Kova.

Kwa upande wa bunge, thamani yake ilianza kumomonyoka pale Dk. Harrison Mwakyembe aliponukuliwa na kumbukumbu za bunge akisema, “Mengine hatukuyasema ili kuokoa serikali.”

Mwakyembe alikuwa mwenyekiti wa kamati teule ya bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni tata ya kuzalisha umeme wa dharura ya kampuni ya Richmond.

Hili linabaki kuwa kitanzi shingoni mwa Mwakyembe kwa kuwa, wananchi hawajapata kujua hicho kilichofichwa ni kipi; kilimlenga nani na kilifichwa kwa maslahi ya nani.

Wananchi wanajua kuwa ripoti ya kamati ya Mwakyembe iliiangusha serikali. Iling’oa waziri mkuu na mawaziri wengine wawili – Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Kung’olewa kwa Lowassa kulimfanya Rais Kikwete kuunda upya baraza lake la mawaziri. Kama waziri mkuu ameng’oka, baraza la mawaziri limevunjika.

Rais alilazimika kuunda upya baraza lake. Sasa kipi ambacho Dk. Mwakyembe na kamati yake walificha ili kuokoa serikali waliyokuwa tayari wamevunja?

Bila shaka hicho kitakuwa kikubwa. Je, ni ushiriki wa Rais Kikwete katika mkataba wa Richmond? Je, ndiyo msingi wa kauli ya Edward Lowassa kwamba, “…nisihukumiwe peke yangu?”

Ndiyo maana baadhi yetu hadi sasa, tunaamini kuwa bado uchunguzi wa Richmond na dada yake Dowans haujakamilika.

Kunahitajika tume huru itakayochunguza mkataba huu wa kinyonyaji. Tume itakayoangalia ushiriki wa kila mmoja. Tume itakayochunguza mkataba wenyewe na kilichofichwa na Mwakyembe na wenzake.

Lakini kuna hili pia: Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuonyesha udhaifu kwa kutetea jambo, lakini baada ya muda mfupi ikabainika kuwa alichokitetea hakikuwa sahihi.

Alifanya hivi kwenye sakata la Richmond/Dowans. Tarehe 5 Februari 2011. Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Dodoma, Kikwete alisema, “Simfahamu mmiliki wa Dowans, wala sijawahi kuonana naye.”

Mahakama ya kimataifa ya migogoro ya kibiashara (ICC) ndiyo ilimuumbua Rais Kikwete.

Ilionyesha kuwa Dowans ni mali ya Rostam Aziz, swahiba mkuu wa Rais Kikwete, aliyemsaidia fedha na mbinu za kuingia madarakani.

Naye Lowassa, aliyejiuzulu kwa kashifa ya kuipa kazi Richmond amewahi kusema, kwa kuelekea Rais Kikwete, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo hukulifahamu au hukunituma.”

Katika mazingira haya, huwezi kupata kauli sahihi ya serikali juu ya jambo zito; kwani kinachosemwa leo kinaweza kukanushwa kesho na mdomo uleule.

Huo nao ni udhaifu wa kiwango chake. Kile ambacho Mwalimu Nyerere alikuwa anaonya kisitokee, ni hiki hapa.

0
No votes yet