Al-Shabaab kuichoma Kenya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version

KIKUNDI cha kigaidi cha Al-Shabaab chenye maskani yake nchini Somalia kimetoa kitisho kipya cha kuteketeza maeneo muhimu na nyeti kiuchumi nchini Kenya ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo.

Taarifa zilizopatikana jijini Nairobi juzi zimesema kuwa kituo binafsi cha kiintelijensia (Intel Centre) ndicho kilichoweka wazi kitisho hicho.

Aidha, Shirika la Habari la Associated Press (AP) la Marekani limesema kituo hicho cha uchunguzi chenye makao yake jijini Virginia kimekariri taarifa za onyo la kikundi hicho dhidi ya Wakenya kikisema, “wasubiri kulia wiki mbili kuanzia sasa.”

Habari kuhusu kikundi hicho chenye fungamano na kikundi cha kigaidi cha al-Qaeda zinasema kwamba Al-Shabaab wameonya kuwa watashusha chini majengo yote marefu nchini humo.

Kwa taarifa fupi ya onyo wamesema: “Jambo kubwa na la hatari linakuja” katika kipindi cha wiki mbili na nchi “itashuhudia maghorofa yakiporomoka."

Hii si mara ya kwanza kwa Al-Shabaab kutoa kitisho cha kuteketeza “majengo yote marefu ya vioo” kwani wamekuwa wakifanya hivyo tangu majeshi ya Kenya yalipoingia Somalia Oktoba mwaka jana kwa lengo la kuzuia mfululizo wa mashambulizi yaliyohusisha matukio ya utekaji nyaraka raia wa Kenya.

Nchi hiyo inajumuisha raia wengi wenye asili ya Somalia hasa kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi.

Majengo yaliyoko katika hatari ya kulengwa katika mashambulizi hayo ni yale ya hoteli kubwa hususan “zinazopendelewa sana na raia wa nchi za Magharibi, kwenye ofisi za serikali, vyombo vya habari vya kimataifa na mashirika mengine nyeti.”

Kikundi hicho chenye msimamo mkali kinatuhumiwa kuhusika katika shambulio la 28 Mei, 2012 katika jengo la biashara za rejareja jijini Nairobi. Mtu mmoja alikufa na wengine 35 kujeruhiwa katika tukio hilo.

Polisi wa Kenya walitangaza Alhamisi iliyopita kwamba wanamshikilia mtu mmoja wakimtuhumu kwa kuhusika na shambulio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi hao, mtu aliyekamatwa alikuwa kwenye ndege iliyokuwa inakwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), huku akiwa na hati ya kusafiria ya Ujerumani yenye jina la Lahbazi Tarek.

Siku moja baada ya tukio hilo, polisi jijini Nairobi, walisambaza picha ya mtuhumiwa mkuu Emrah Erdogan, anayeaminika kuwa ama ni raia wa Uturuki au Ujerumani.

Harakati za kutokomeza wapiganaji wa kundi la Al Shabaab nchini Somalia zinaungwa mkono na nchi kadhaa ikiwemo Ethiopia na Marekani.

Kikundi hicho kimekuwa kikisema kuwa kila anayeshirikiana na majeshi ya kigeni yaliyoko Somalia, atakabiliana na mashambulizi yao.

Mwaka 1998, jiji la Nairobi, pamoja na jiji la Dar es Salaam, Tanzania, yalikabiliwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa kwenye majengo ya ofisi za kibalozi za Marekani, katika muda unaofuatana. Zaidi ya watu 200 walifariki dunia katika mashambulizi hayo.

0
No votes yet