Amani halisi ni tunda la haki


Fred Mpendazoe's picture

Na Fred Mpendazoe - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

NCHI yoyote ikiishapata uhuru wake, huelekeza mikakati yake katika kuwapatia maendeleo wananchi  wake.

Serikali imara na amani ni mambo muhimu kwa uhuru na maendeleo ya wananchi. Serikali imara ni muhimu kwa ajili ya kulinda uhuru na heshima ya nchi na amani ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Amani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Lakini napenda tuelewane kabisa mwanzoni, je ni amani ipi inayoweza kuchochea maendeleo ya nchi au taifa?

Amani ya kweli na amani halisi ni tunda la haki. Amani na haki za binadamu ni vitu viwili vinavyoambatana. Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, Sehemu ya Tatu inaeleza juu ya Haki za Binadamu.

Kuna haki ya usawa. Mfano, binadamu wote ni sawa; watu wote ni sawa mbele ya sheria.  Kuna haki ya uhuru wa mawazo, mfano kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kueleza fikra zake; na kuna haki ya kufanya kazi mfano kila raia anastahili fursa na haki sawa ya kushinda nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi.

Amani na haki za binadamu ni vitu ambavyo vinaambatana. Kwa hiyo, katika jitihada za serikali makini za kuimarisha amani ili maendeleo kwa nchi yapatikane, ni lazima serikali hiyo iweke jitihada za makusudi za kuisimamia haki kwa raia wake. Bila haki hakuna amani na bila amani maendeleo hayawezi kupatikana.

Ni jambo lisilopingika kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake, kwa muda mrefu, imekuwa ikihubiri amani na utulivu bila kusimamia haki za msingi katika jamii.

  • Mkulima ana amani gani wakati hana haki ya kupanga bei ya mazao yake?
  • Mfanyakazi ana amani gani bila ya kuwa na haki ya kujadiliana na mwajiri wake juu ya mafao na mshahara wake?

  • Wanafunzi wa vyuo wana amani gani wakati hawana usawa kwenye mikopo?
  • Polisi wana amani gani wakati wanaishi kwenye makazi duni na mishahara duni?
  • Mwananchi ambaye hana uhakika wa mlo mmoja kwa siku ana amani gani?

Chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, CCM ilisimamia misingi ya haki, usawa na kujitegemea. CCM ni chama kilichopigania maskini na wanyonge. Kilitambulika kama chama cha wakulima na wafanyakazi.

Kutokana na uongozi mahiri wa Mwalimu Nyerere Watanzania walikuwa wazalendo kwenye nchi yao, na waliheshimika duniani kote kwa umoja na mshikamano waliokuwa nao katika masuala ya kitaifa. Na pia Tanzania ilishangaza dunia kutokana na amani iliyokuwepo pamoja na kuwa Tanzania ilikuwa nchi changa na maskini.

Uongozi wa Mwalimu Nyerere ulizingatia haki, usawa na kujitegemea, kutokana na msimamo huo Tanzania ilikuwa nchi ya amani kweli.

Lakini amani inayohubiriwa na CCM na Serikali yake haina maana katika maisha ya Mtanzania kama amani yenyewe maana yake ni kutokuweko mapigano na maandamano. Amani ya namna hii, inayohubiriwa na CCM bila ya kusimamia haki za msingi za binadamu ni kisingizio kingine cha kudumisha dhuluma ambayo inawanyang’anya Watanzania wengi haki ya utu wao. Amani na utulivu unaohubiriwa, kwa muda mrefu, ni usanii mwingine na ni upuuzi.

Amani ni tunda la haki, usawa, na uhuru. CCM na Serikali yake imeanza kuwatisha raia na kuwataka wasiandamane kwa kisingizio kwamba hali ya amani ni tete. Naomba Watanzania waelewe, utii bila uhuru na haki ni utumwa.

Serikali isimamie haki na uhuru kwa raia wake na amani halisi na amani ya kudumu itashamiri. Polisi wavitendee haki vyama vyote vya siasa kwa sababu nchi yetu ni ya mfumo wa vyama vingi kikatiba.

Nakubaliana na maneno ya aliyekuwa kiongozi wa China, Mao Tze Tung aliposema, “Siasa ni vita isiyomwaga damu na vita ni siasa inayoendana na kumwaga damu.” Hivyo, kwa kuzingatia maneno ya Mao, vyama vyote vya siasa vinapaswa kulindwa vifanye siasa kwani siasa ni vita isiyomwaga damu. Kuvinyima haki vyama vya siasa ni kusababisha vita, kwani vita ni siasa inayoendana na umwagaji damu.

Polisi wanapowapiga mabomu waandamanaji ni siasa inayoendana na umwagaji damu. Polisi wanapowapiga mabomu wanachuo ni siasa inayoendana na umwagaji damu.

Polisi waviache vyama vya siasa na wanasiasa wafanye siasa, kwani siasa ni vita isiyomwaga damu. Vyama vya upinzani vikisema Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kuliongoza taifa hili, hiyo ni vita isiyomwaga damu.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) au chama kingine cha siasa kikisema CCM haifai kuendelea kuongoza nchi, hiyo ni vita isiyomwaga damu.

Naomba kusisitiza, amani ambayo inahubiriwa na CCM na Serikali yake wakati Watanzania wana hali mbaya ya maisha; hawana umeme, umaskini ukizidi kuongezeka, na haki za binadamu hazizingatiwi si amani ya kudumu wala si amani inayostahili.

Amani ni jambo muhimu na vyama vya siasa vinajua hivyo na mabadiliko tunayotafuta tunataka yapatikane kwa njia ya amani.

Lakini Serikali ielewe pia, inapotokea kwamba kila juhudi ya kuleta mabadiliko kwa njia za amani imefungwa, kama wananchi wananyanyaswa katika nchi yao wenyewe, na kunyimwa kabisa nafasi yoyote ya kushiriki katika kuleta mabadiliko yao wenyewe, bado kweli tunayo haki ya kudai iwepo amani, hali wananchi wakiteseka na kutotendewa haki, wakiwa watumwa kwenye nchi yao?

Kwa kweli, amani katika hali hiyo haiwezi kutarajiwa na amani ya namna hii haiwezi kuchochea maendeleo.

Amani ni tunda la haki. Serikali iweke jitihada zaidi katika kusimamia haki kwenye jamii, na amani itakuwepo, na amani inayotokana na  haki na usawa ni amani inayodumu na ni amani halisi.

Nahitimisha kwa kuikumbusha serikali kwa maneno ya Shaaban Robert kwamba, “unaweza kuichovya hatia yako kwenye dhahabu kama upendavyo, lakini mkuki imara wa haki hauvunjiki.”

Kwa hiyo, kuhubiri amani bila kusimamia haki ni hatia, na serikali kudai maandamano ni chanzo cha amani kuwa tete ni kuichovya hatia yake kwenye dhahabu lakini msingi wa haki ni imara na haki itashinda.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: