Amani yatoweka


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Dk. Steven Ulimboka

UHAI wa Dk. Steven Ulimboka uko mashakani. Viongozi wenzake wa Jumuia ya Madaktari Tanzania wanaishi kwa hofu. Wanachama wa Chama cha Madaktari nchini nao wanahofia kukamatwa, kuteswa na labda kuuawa.

Kwa lugha ya Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, amani imetoweka nchini.

“Hii ni hatari. Wenye kauli na misimamo tofauti na serikali sasa wataishi kwa woga. Iko wapi amani ambayo imeimbwa miaka nendarudi?” amehoji Mabere Marando, wakili wa mahakama kuu.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), Ananilea Nkya amesema ipo haja wananchi kuhakikishiwa    usalama wao.

Naye Dk. Willibrod Slaa, katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipoulizwa juu ya tukio la kutekwa na kuteswa Dk. Ulimboka, alimlaumu Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake kwa vyombo vya habari.

Alisema amemshangaa Rais Kikwete kwa kuibuka na kujitetea kuwa serikali yake haikuhusika na utekaji wa daktari, badala ya kuunda tume huru ya kuchunguza tukio hilo ambamo serikali ni mtuhumiwa Na. 1.

Amesema kwa rais kutokuwa makini katika kulinda na kuhakikisha usalama wa raia, “amedhihirisha udhaifu wake ulioelezwa ndani ya bunge.”

“Mimi siungi mkono mgomo. Sipendi kuona wananchi wanakosa huduma muhimu – iwe ya tiba, maji, elimu, chakula…lakini hapa kuna madai ya mazingira bora ya kazi na maslahi ya wafanyakazi,” ameeleza.

Amesema kwamba rais hasemi ukweli kuhusu serikali kutokuwa na fedha. “Kwa mfano, sijamaliza kupitia vitabu vyote vya bajeti inayojadiliwa sasa, lakini tayari nimeona kuna Sh. 15 bilioni kwa ajili ya chai tu.”

Amesema kuwa wala tatizo siyo kushindwa kubaini vipaumbele, “bali Rais Kikwete siyo sensitive (hana hisia); ana tatizo la kuwa insensitive (kutokuwa mwenye hisia) katika masuala ambayo yanahusu haki za watumishi wa umma wakiwemo madaktari.”

Wakati hata hali ya Dk. Ulimoka haijaelezwa kuwa nzuri, Rais Kikwete ametishia madaktari akisema wajue kuwa “…ajira zao wanaziweka hatarini.”

Amesema kuwa katika hotuba yake ya kila mwezi kwa taifa,  “Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kuwalinda. Kwa madaktari interns (wanafunzi), wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu…”

Dk. Ulimboka ambaye amekuwa kiongozi wa madaktari wa umma na binafsi katika kudai mazingira bora ya kazi, alitekwa jijini Dar es Salaam, Jumanne wiki iliyopita, na watu ambao walijitambulisha kuwa ni polisi.

Badala ya kumpeleka kwenye kituo cha polisi cha karibu, Oyster Bay, walimpeleka walikojua, kumpiga, kumtoa meno na kung’oa kucha kabla ya kumtelekeza kwenye msitu wa Mabwepande akiwa hajielewi.

Dk. Ulimboka amekaririwa akisema kwa taabu, kwamba watekaji walimfunga kitambaa cheusi usoni, wakampeleka kwenye nyumba moja na kuanza kumpiga; lakini akihisi alikuwa katika maeneo ya Mwenge.

Kati ya Leaders’ Club na Mwenge kuna maeneo mawili makubwa ya ulinzi wa dola: Polisi Oyster Bay na ofisi za usalama wa taifa Makumbusho (Kijitonyama).

Dk. Ulimboka aliokotwa asubuhi Jumatano akiwa amezinduka lakini akishindwa kusimama, kuongea na hata kunywa maji.

Jumamosi alipelekwa Afrika Kusini kwa uchunguzi zaidi na matibabu.

Madai makuu ya madaktari yamekuwa zana stahiki za kazi, mishahara inayolingana na kazi wanayofanya, posho za mazingira magumu na hatarishi.

Kutekwa kwa Dk. Ulimboka kumeresha kumbukumbu za matukio kadhaa ya raia kuvamiwa, kupigwa, kujeruhiwa, kumwagiwa tindikali na hata kuuawa (Soma makala uk.14).

Mwaka 2008, Mkurugenzi Mtendaji Saed Kubenea na mshauri wa taaluma Ndimara Tegambwage, walivamiwa ofisini, kumwagiwa tindikali na kujeruhiwa kwa mapanga.

Serikali ilishindwa kufanya upelelezi na kuwasilisha ushahidi mwanana wa kuweza kutia hatiani waliohusika, huku Tegambwage akiambiwa asitoe ushahidi kwa madai kuwa “utawavurugia kesi.”

Dk. Ulimboka aliitwa usiku na mtu aitwaye Abeid. Akafuatana na daktari mwenzake, Deo Michael kwenye eneo la mkabala na walinzi wa Ultimate Security, karibu na Leaders’ Club, Kinondoni.

Haikuchukua muda, wakaingia watu watatu wenye silaha waliojitambulisha kuwa ni polisi na kusema, “Tunamtaka huyu” (Dk. Ulimboka), ameeleza mtoa taarifa.

Wawili, kila mmoja alishika bastola; mwenzao ambaye alivaa suruali ya “kijeshi hivi, alikuwa na bunduki aina ya SMG,” ameeleza.

Walimchukua dokta, wakamburuta hadi upande wa pili wa barabara walipoegesha gari lao na kuondoka naye. Kama mzaha vile, Dk. Ulimboka akaishia.

Abeid, yule aliyekuwa mwenyeji wa madaktari hawa wawili, alibaki kujitia haelewi kilichotokea.

Asubuhi ya Jumatano ndipo madaktari walipopokea simu kutoka Bunju ikiwaita, “…njooni mchukue mzoga wenu.”

Watu wawili walioona mtu aliye taabani kuelekea msitu wa Mabwepande, wameieleza MwanaHALISI kuwa walimkuta “…amechakaa kama mtu aliyetapikiwa. Ni mfano wa majani yaliyocheuliwa na ng’ombe.

“Tulimkuta hoi, amevimba kila mahali, hajitambui kabisa. Tulipomhoji alishindwa kutoa sauti. Hakuwa na suruali. Ni shati tu huku chini kote ametapakaa kinyesi,” anasimulia mmoja wao.

Siku hiyo hawakujua kuwa huyo alikuwa Dk. Ulimboka ila “…siku tunarudi kutoka Same kuzika, ndipo tukagundua kumbe tuliyemkuta na kumsaidia ni Dk. Ulimboka. Tuliona picha magazetini.”

Habari nyingine zinasema kuna wapitanjia waliompa mwananchi mmoja Sh. 5,000 abaki pale kumlinda majeruhi hadi wafike polisi.

Sasa zimeenea taarifa kuwa Abeid, yule mwenyeji wa Dk. Ulimboka kabla ya kutekwa, amekwenda Pretoria, Afrika Kusini, nchi ileile ambako Dk. Ulimboka alipelekwa Jumamosi asubuhi, kwa msaada wa madaktari wenzake.

Gazeti hili halijapata uthibitisho wa fununu kuwa Abeid, anayetajwa kama kachero katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alikutwa ofisi za Ubalozi wa Afrika Kusini, Masaki, akishughulikia viza.

Dk. Ulimboka ameumizwa kichwani, kifuani na tumboni. Ametolewa meno mawili ya mbele na kumng’oa kucha mikononi. Pia walimkatakata mikononi.

Akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) – Idara ya MOI – baada ya kufikishwa kwa ambulance ya shirika la tiba la AAR, Dk. Ulimboka alimtambua mmoja wa aliowaita watekaji wake.

Ghafla alijiwa na nguvu, akatoa sauti akisema, “Nipe simu yangu, na waleti yangu.” Yule “mtekaji” akatimkia chooni. Mhudumu mmoja amedai kuwa alisikia mtu aliyeko chooni akisema, “Ndiye, wala hajafa.”

Ilimaanisha alikuwa akiwaambia wenzake katika “mpango wa kumwangamiza” Dk. Ulimboka, kuwa haukufanikiwa.

Huyu ndiye Kamishna wa Polisi Suleiman Kova wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, anasema “alipigwa na madaktari kwa bahati mbaya kwani alikuwa tayari katika kikosi cha kufanya uchunguzi wa tukio lililomhusu Dk. Ulimboka.”

Kova aliiambia MwanaHALISI juzi Jumatatu, kuwa hawezi kujibu maswali ya mwandishi, kwani angeharibu uchunguzi.

“Nimeunda tume ya watu watano wanaochunguza jambo hili,” amesema (Soma makala uk. 3).”

Hii ilikuwa mara ya pili kwa madaktari kugoma. Mara ya kwanza walikutana na rais aliyeahidi kutatua matatizo yao; lakini walipoona hakufanya hivyo, waliamua kugoma mara ya pili kuishinikiza serikali.

“Una mgonjwa. Unatamani kumsaidia maana unafahamu nini cha kufanya. Lakini huna zana. Mara hakuna hiki mara kile kimeharibika. Unafanyaje?

“Unashuhudia mgonjwa aliye mbele yako anakufa hivi hivi kwa kuwa huwezi kumsaidia. Sasa hii hali haiwezekani kuendelea, kama vile tuna viongozi wasiokuwa na akili timamu,” daktari mmoja amemwambia mwandishi wa habari hizi.

Viongozi wa upinzani, wabunge wa CCM ambao wana msimamo wa wastani na waandishi wa habari, wamekuwa wakieleza kuwa wanapigiwa simu za vitisho na watu wasiowafahamu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: