Amesuka msuko uleule


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

BABA Mkubwa anapotaka kufanya jambo fulani mara nyingi hujifungia ndani kimya hadi tukamsahau kama yupo au amesafiri.

Humo ndani atapiga kichwa kutafuta msamiati mzito wa kutoka nao ambao anajua atawaacha watoto wake wakihangaika kupata maana katika kamusi au fasili yake. Basi watoto watabishana mwaka mzima alikuwa na maana hii au ile.

Aliposema umefika wakati sasa wa “kuhuisha katiba”, watoto walikimbilia haraka kusema anataka katiba mpya kumbe alimaanisha marekebisho tu. Ametaja maeneo ya kurekebisha na mengine amekataa.

Baadaye alikuja na msemo mwingine wa kujivua gamba. Kabla hajamaliza hotuba yake na kufafanua maana ya kujivua gamba watoto walipiga mbio kuandika kuwa “watu waliochukua chao mapema watabanduliwa kama gamba la nyoka.”

Sisi wengine tulihoji wamesalitiana? Si wote wanatoka  kundi haramu la Chukua Chako Mapema? Itawezekana kweli waachane na kauli ya “huyu mwenzetu?” Isitoshe nani kati yao hajachukua chake mapema?

Tukasubiri Aprili hola! Mei gamba halikudondoka, Juni, Julai… Tukaambiwa siyo hivyo ila ni kujenga mfumo bora wa kulindana. Kwa maana hiyo watu wasitarajie gamba kudondoka. Ni kweli 2011 ikakatika.

Baba Mkubwa ni mwanafasihi mkubwa. Ndiyo maana sikutaka kabisa kuingia kwenye mtego wa kuamini kile alichosema ni dhamira yake ya “kusuka upya” Baraza la Mawaziri.

Tuliposikia kauli hiyo tulijishika pumzi. Kusuka upya ni kufumua kilichosukwa ovyo na kurudia au kusuka tena kwa lengo la kuboresha.

Hata hivyo ni lazima anayefanya hivyo yeye mwenyewe ajue kwamba msuko wa kwanza ni ovyo au hauna mvuto. Pia ni lazima awe na ufundi wa kuboresha zaidi ya awali.

Msemo wa “kusuka au kunyoa” una lengo la kuonyesha uamuzi mgumu. Kusuka ni uamuzi mwepesi; kunyoa ni uamuzi mgumu.

Baba Mkubwa angesema “nitanyoa” Baraza la Mawaziri tungejua amedhamiria kufanya mabadiliko makubwa, lakini aliposema “nitasuka upya” alimaanisha kurudia tu kwa vile ameshurutishwa na mijadala ya wabunge na wananchi.

Matokeo ndiyo haya. Aliita wasaidizi wake wakajifungia ndani wakamchambua kila mtuhumiwa, wakitafuta jinsi ya kuwasuka kwenye “makuti mengine”.

Wakafanikiwa kwa kuwafutia tuhuma wawili halafu na wengine akasema eti wamewajibika kisiasa kutokana na makosa ya wasaidizi wao. Kama alijua wasaidizi ndio wenye makosa, kwa nini hakuwachukulia hatua?

Kama hawakuchukua hatua hadi CAG na Kamati za kudumu za Bunge zikatoa ripoti zao zikifichua uoza katika wizara wameachwa ofisini hadi lini? Nani hajui kuwa wahasibu na wakurugenzi wa halmashauri nyingi wamegeuka wezi, lakini aliyekuwa Waziri wa Tamisemi amehamishwa wakati naibu wake ametupwa?

Wizara ya Madini na Nishati, ilikuwa gumzo mwaka mzima uliopita na hasa kutokana na sakata la fedha lililomkumba katibu mkuu. Waziri ameondolewa lakini naibu wake amehamishwa kwingine. Katika Biashara na Viwanda, bosi katimuliwa ‘mdogo mtu’ kapewa ulaji kwingine.

Hii ndiyo maana ya kusuka upya yaani kurudia makosa. Baba Mkubwa hakutaka kunyoa. Huu ni ushahidi kuwa Baba Mkubwa ama hajui au haoni tatizo la utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri.

Ni rahisi kumwambia Baba Mkubwa “atazame” tatizo lakini si rahisi kumwambia “aone” tatizo. Si kila mtu anayetazama anaona.

Baba Mkubwa amelazimishwa kutazama na kuchukua hatua kinyume cha dhamiri yake ndiyo maana amesuka pamoja na wazembe na wanaolala usingizi Mjengoni.

Makuti mapya kaweka kwenye Fedha, kwingine…tehe, tehe, tehe, tehe, tehe!

0658 383 979
0
No votes yet