Amjuae msafi na mwadilifu CCM na serikalini amtaje


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 18 January 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WATANZANIA walishangaa Desemba 8 mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alipowatunuku nishani ya utumishi uliotukuka viongozi kadhaa na wastaafu walio hai na waliokwishakufa ikiwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.

Mshangao huo ulitokana na ukweli kwamba viongozi waliostahili kutunukiwa kwa macho na akili za wananchi hawakuguswa. Waliotajwa kustahili ni pamoja na Spika Mstaafu Samwel Sitta na Waziri Mkuu Mstaafu Samwel Malecela.

Kabla ya kwenda mbali niseme wazi silalamikii Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa naye kukosa. Huyu hakustahili na hastahili nishani hii. Sababu zinaeleweka, kunitarajia kuzitaja hapa ni uchochezi.

Mshangao wa Watanzania haukutokana na kitendo cha Rais kuwatunuku nishani viongozi hao walio hai na waliokwishakufa bali aina ya viongozi waliopata nishani hizo wakiwamo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Spika Mstaafu Pius Msekwa  na Spika wa sasa wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda.

Wakati akitunuku nishani hizo kwenye viwanja vya Ikulu Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema bayana kuwa nishani hizo zilikuwa zinatolewa kwa Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu wastaafu, walio hai au waliokufa, walioondoka madarakani bila kashfa na hata baada kuondoka kwao madarakani, wameendelea kuwa na maadili mema na kuishi kwa heshima na maadili ya ofisi yao.

Hapa ndipo mshangao wa Watanzania unapoanzia. Hivi Rais Mstaafu Mkapa kwa mfano aliondoka madarakani bila kashfa? Hivi kweli Rais wetu mpendwa JK hafahamu kashfa zilizomwandama mtangulizi wake alipokuwa madarakani? Kweli hajui kashfa za Mkapa? Hata moja!!!

Mshangao wa Watanzania unakuja kwamba kama kuna Watanzania 52 waliostahili kupata nishani kwa kigezo cha kutoa michango mbalimbali ya kutukuka kwa maendeleo ya nchi (Tanganyika) katika miaka 50 ya uhai wake eti ni pamoja na Benjamin William Mkapa, basi ina maana katika chama tawala na serikalini hakuna msafi wala mwadilifu.

Bila kuingiza uchochezi niseme kwamba Mkapa na Anne Makinda hawakustahili kwa kigezo chochote kile kupata nishani zile.

Hata kwa bahati mbaya tu bado Mkapa na Makinda hawakustahili kupata nishani yoyote ya utumishi uliotukuka. Hivi utumishi wa Mkapa unatukukaje ilhali bado tunamdai kodi ya pango aliyopangisha kampuni yake binafsi kwenye jengo la Ikulu?

Hivi utumishi wake unatukukaje wakati aliwagawia mali ya umma mwanawe, mkwewe, marafiki zake, vivele wenzake na maswahiba zake kwa bei sawa na bure. Hapa nazungumzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya.

Hivi utumishi wa Mkapa unatukukaje huku inafahamika leo kuwa alipewa mkopo (wewe soma hongo, mlungula au rushwa) wa mamilioni ya shilingi na kampuni ya kikaburu iliyokuwa inaitaka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na eti baada ya miezi saba deni likafutwa kwa kisingizio kuwa alikuwa amemaliza kulipa.

Kwanza huu si uchochezi na pili kiongozi wa nchi kukopeshwa na mzabuni anayewania kupewa zabuni ya ununuzi wa benki ya taifa si utumishi uliotukuka. Tatu Mkapa hapa hakulipa deni. Kama kweli alilipa, pesa hizo zilitokana na biashara gani aliyofanya pale ikulu ndani ya miezi saba?

Sitaki kusema sana bali kuongeza kwamba hata Makinda hakustahili kupata nishani kwa kuligeuza Bunge kuwa kijiwe cha CCM cha kutolea mipasho ikiwalenga wapinzani au kijiwe cha kugongea meza na kuzomea wapinzani wanaotoa hoja za kulikwamua taifa.

Makinda, kwa kuwafungia njia majirani zake jijini Dar es Salaam baada ya kupata uspika na baadae kujigeuza baunsa wa CCM wa kuwatimulia mbali wabunge wa upinzani wanaohoji mambo yanayowakwaza wananchi hakustahili, hastahili na hatastahili kupata nishani.

Sasa mimi najiuliza kama waliopata nishani hawakustahili hata kidogo kwa sababu hawakuwa na utumishi uliotukuka, nani anayestahili au aliyestahili kupata nishani hizo za utumishi uliotukuka Tanzania.

Yaelekea CCM na hasa katika serikali yake hakuna watu wasafi na kama wapo basi hawajulikani. Kama watu wasafi na waadilifu ni Anne Makinda na Benjamin Mkapa basi hakuna msafi wala mwadilifu huko CCM na serikalini. Nani kama yupo unayemfahamu?

Ijulikane wazi kuwa mtu mwadilifu na msafi hawezi kuwa Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, kwa sababu huyu katajwa na Tume ya Jairo kuwa alikuwa miongoni mwa waliopokea posho zile zisizo miguu wala kichwa zilizokuwa zinagawiwa na huyo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini.

Niambiwe nani msafi serikalini na katika CCM. Mtu huyo si Samwel Malecela kwa sababu imeelezwa kuwa huyu alipewa mapesa kwa mamilioni na Jeetu Patel na pesa zenyewe zikaporwa kwa mkewe Anne Kilango Malecela alipopata ajali mkoani Morogoro.

Msafi ndani ya CCM hawezi kuwa Frederick Sumaye kwa sababu huyu akiwa Waziri Mkuu aliwahi kuhamisha makusudi mradi wa maji mkoani Singida kwenda kwao Wilaya ya Hanan’g yenye makao makuu Katesh.

Mwadilifu ndani ya CCM hawezi kuwa Waziri Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kwa sababu rafiki yangu huyu alihusika sana na mradi wa mabasi ya wanafunzi Dar es Salaam. Mradi huu ulifilisiwa naye Lukuvi pamoja na kina John Guninita, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM mkoani Dar es Salaam.

Kuna Bwana mmoja CCM na serikalini naye hastahili kutunukiwa nishani hii. Namtaja hivi: alikiuka katiba, sheria, kanuni na taratibu kwa kukutana na mafisadi na kupatana nao warejeshe walichopora badala ya kuwakamata na kuwashitaki mahakamani na kuhukumiwa ili wakifungwa awatoe kwa kutumia mamlaka ya kikatiba.

Mwisho niwatendee haki rafiki zangu hawa. Naomba anayemjua mtu msafi ndani ya CCM na serikali amtaje. Pia nimeanzisha orodha itakayotaja kila kiongozi na kashfa yake. Nyinyi nisaidieni kuikamilisha kwa kunitumia majina ya viongozi na kashfa zao.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: