Amri ya hakimu Kisutu ni hatari


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version

HAKIMU mmoja jijini Dar es Salaam amepiga marufuku waandishi wa habari kuandika mwenendo wa kesi kati ya wafanyabiashara wawili – Yusuf Manji na Reginald Mengi.

Huyu ni Ilvin Mgeta wa mahakama ya hakimu mkazi, Kisutu. Magazeti yamemnukuu akiagiza vyombo vya habari kuacha kuripoti kesi hiyo kwa kuwa “vinapotosha.”

Hivi nani anapotoshwa – Hakimu? Wananchi ambao ni wasomaji wa magazeti? Mlalamikaji? Mlalamikiwa? Hakimu, anataka kumlinda nani ambaye ni mwepesi wa kupotoshwa?  

Katika hatua hii, siyo vizuri, kama ambavyo siyo salama, kwenda peke yangu. Sharti niite wenzangu – Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Sharti niite vyama vya waandishi wa habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari mmojammoja; vyama vya wapigania haki za binadamu, watetezi na wadau wote wa uhuru wa maoni, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa habari.

Hoja ni hii hapa. Hakimu anaelekea kunyonga uhuru wa vyombo vya habari; uhuru wa habari; uhuru wa wananchi kupata habari. Nani amemtuma?

Twende hivi: Ripota (au chombo cha habari) ambaye ameandika kwa makusudi, taarifa ya mwenendo wa kesi mahakamani isiyo sahihi na “kwa lengo la kupotosha kilichotendeka mahakamani,” huweza kuchukuliwa hatua: Kushitakiwa kwa kudharau mahakama.

Kama hivyo ndivyo, uamuzi wa kuzuia vyombo vyote vya habari kuandika mwenendo wa kesi, unatoka wapi? Hakimu amepata wapi ushauri, ushawishi na uwezo wa kunyamazisha vyombo vya habari na wananchi?

Manji anamlalamikia Mengi kwa kumtwisha kashfa ya kumwita “fisadi papa” na anataka kufidiwa kwa Sh. 1 tu. Uko wapi uzito wa dunia nzima kukosa taarifa za mwenendo wa kesi hii?

Amri ya hakimu inaturudisha miaka mingi nyuma; nyakati zile za “gag orders” – amri za kuzuia utoaji habari fulani iliyodhaniwa na watawala au mamlaka fulani kwamba ingeleta sokomoko kwao.

Hata kama amri hii bado imo katika sheria za sasa – Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na Sheria ya Utangazaji – hata watekelezaji wake wanaona aibu kuzitumia sheria hizi kwa kuwa zinawafanya waonekane mbilikimo katika medani ya sheria, demokrasi na haki za binadamu.

Watetezi wa hatua ya hakimu wanadai kuwa vyombo vya habari vinaweza kumbabaisha hakimu; kuathiri uelewa/ufahamu wake na hata msimamo wake katika kesi inayoendelea. Hivyo sharti vidhibitiwe.

Wanakosea. Wanasahau kuwa taarifa zozote zile zinazoandikwa juu ya kesi iliyoko mahakamani, ni moja ya misaada mikuu katika kupata mwanga juu ya kilichotendeka, kinachoendelea na kinachosubiriwa.

Wadai, wadaiwa, mahakimu na majaji hupata utajirisho wa aina yake kutokana na mlisho wa nyongeza utokao pembeni na hata katika mrejesho kwa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari.

Vipi hakimu azime mifereji ya fikra na taarifa mwanana kwa mashauri yaliyoko mbele ya mahakama? Niruhusu niseme hapa kuwa, hata amri/sheria ya kuzuia kuandika lolote juu ya kesi ambazo tayari ziko mahakamani, ni mizengwe ya kipuuzi na kinga ya kijima katika maendeleo ya sheria.

Kwa kuzingatia kauli na hatua ya hakimu inayojadiliwa, mahakimu na majaji ni “watu wepesi sana kushawishiwa kuacha sheria na kufuata fitina, ushauri na hata porojo nje ya mahakama.”

Amri ya hakimu inataka kutuelekeza kuwa mahakimu na majaji ni dhaifu sana. Nashindwa kukubaliana na msimamo huo.

Bali najikumbusha kauli ya jaji aliyewahi kusema kuwa ndani ya mahakama hakuna mwamuzi mmoja – iwe mahakama ya mwanzo, ya wilaya au mahakama kuu.

Alisema ndani ya mahakama kuna waamuzi (hakimu au jaji maalum) wengi. Hawa ni pamoja na wanaofuatilia kesi. Hivyo ndani ya mahakama kuna waamuzi wa aina nne.

Kuna hakimu au jaji mwenye madaraka ya nguzo hiyo ya dola. Kuna waamuzi wa upande wa mlalamikaji; waamuzi upande wa mlalamikiwa; na waamuzi upande wa kati –  ule wa wanaofuatilia kuona upande upi umesema nini na mahakama itasemaje.

Wakati kesi inaendelea, wote wakitoka nje, kila mmoja ana maoni yake. Wakati mwingine “mahakimu” au “majaji” wa nje waweza kuzua mjadala mkali unaoweza kuzimwa na polisi peke yake; kila mmoja akitetea upande wake.

Lakini hoja za waamuzi, ikiwa ni pamoja na taarifa za vyombo vya habari, haziendi mbali hadi kushawishi na hata kukanganya hakimu au jaji anayesikiliza kesi.

Mahakimu na majaji wanajua hili na siku zote wametakiwa kufanya maamuzi yasiyoathiriwa na ushawishi – rushwa halisi ya fedha, vitu au ahadi.

Mahakama zinazoendeshwa na mahakimu; wasomi wazuri wa sheria, hazitarajiwi kusombwa na mawimbi ya kinachotokea nje ya pembe nne za mahakama.

Badala yake, zinapaswa kuvuna yale ambayo ni elimishi na yanayosaidia kufafanua, kuboresha na kutoa nuru zaidi kwa yanayotokea mahakamani.

Hakimu ambaye mbele yake kuna kesi ya kijana anayetuhumiwa wizi kwa kuwa tu amekutwa na fedha kwenye soksi mguuni, aweza kupata maarifa akisafiri katika daladala.

Akiona msongamano na vitimbi vya daladala, atagundua kuwa mahali salama pa kuweka fedha katika mazingira hayo, ni kwenye soksi; tofauti kabisa na alivyoamini awali kuwa aliyehifadhi fedha kwenye sokosi, bila shaka “atakuwa mwizi.”

Maarifa haya hayawezi kuvuruga kesi. Yanaweza kuimarisha haki kwa yule ambaye angechukuliwa kuwa mwongo, mwizi au punguani.

Kwa msingi huu, mahakimu hawatetereki kwa taarifa zinazoandikwa magazetini au kauli za washindani nje ya mahakama.

Hivyo hatua ya hakimu wa Kisutu kupiga marufuku vyombo vya habari kuandika mwenendo wa kesi ya Manji na Mengi inaweka msingi mbaya na mchafu katika mazingira ya sasa ya kujenga demokrasi.

Hakimu amevunja haki ya kukusanya na kusambaza taarifa na habari; ameziba njia mwanana za taarifa za nyongeza muhimu kwa kunawirisha mbongo na kufanya maamuzi.

Hatua hii ya hakimu inashawishi ziwepo amri nyingine za aina hii za kutuziba akili na midomo na kufanya taifa hili kuwa la kondoo.

Tunakubaliana kuwa aliyetenda kosa afikishwe mahakamani, ikiwa ni pamoja na aliyedharau mahakama ili sheria ichukue mkondo wake.

Lakini tunakataa kwa kishindo, amri ya jumla ya kunyamazisha vyombo vya habari, tena juu ya shauri lililoko mahakamani. Hiki ndicho chanzo cha udikiteta mchafu.

Kuna nini katika kesi ya Manji na Mengi? Nani ameomba vyombo vya habari vinyamazishwe? Kwa nini sheria zisichukuliwe dhidi ya walio na kosa?

Hakimu Ilvin Mgeta ana rekodi ya utendaji haki mahakamani. Nani amemshauri achukue hatua ambayo wengi watabaki wakisema, “Mh, siyo bure?”

Kwa wenye vyombo vya habari, waandishi mmojammoja, wanaharakati wa haki za binadamu na wadau wa uhuru wa habari, tukatae amri ya hakimu kwa kishindo.

0713 614872 ndimara@yahoo.com www.ndimara.blogspot.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: