Amri ya mahakama ipingwe baada ya hukumu


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version

MOJA ya malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji kazi wa mahakama, ni tatizo sugu la ucheleweshaji kesi. Malalamiko hayo hutokea ama kesi inapoanza kusikilizwa, wakati inapoendelea kusikilizwa, au inapoahirishwa bila sababu za msingi.

Ucheleweshaji mwingine hutokea pale linapotokea pingamizi za kisheria wakati kesi ikiendelea, ambapo mahakama hupaswa kulisikiliza na kulitolea uamuzi.

Hali hii hujitokeza katika kesi za aina zote mbili: kesi za jinai zinazoendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai (CPA) ya Mwaka 1985 na kesi za madai zinazoendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Madai (CPC) ya Mwaka 1966.

Mashitaka yanaweza kutokana na uvunjaji wa sheria nyingine yoyote kama ya mikataba au rushwa au usalama barabarani. Lakini usimamizi wa uendeshaji wa kesi ni kwa mujibu wa CPA au CPC. Sheria hizo mbili ndio misahafu yao mikuu mahakamani. 

Majaji na mahakimu, nao katika kusikiliza mashitaka yanayoletwa mbele yao, huongozwa na sheria hizo mbili pamoja na Sheria ya Mahakimu (MCA) ya Mwaka 1984.

Majaji na Mahakimu hao wanapaswa kusimamia uendeshaji wa kesi nzima ili kuhakikisha haki sio tu inatendeka, bali inaonekana kutendeka.

Sheria zile za CPA na CPC zimekuwa zikitumika miaka mingi kiasi kwamba kuna wakati zimekuwa haziendani na wakati tulionao wa mabadiliko ya kiuchumi hapa nchini, kiasi cha kuzifanyia marekebisho ya mara kwa mara.

Moja ya marekebisho hayo ni yale yanayohakikisha kesi hazicheleweshwi kwa kisingizio cha haki ya kukata rufaa kiholela, kwa kupinga jambo lolote na wakati wowote wakati kesi inapoendelea kusikilizwa.

Mfano hai ni marekebisho ya CPA ya mwaka 2002 yanayohusu usikilizaji kesi za madai kwa Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya.

Sheria hiyo hairuhusu tena mtindo wa zamani wa kuzipinga amri za Mahakama kwa kukata rufaa au kuomba mapitio juu ya amri zinazotolewa wakati kesi ikiendelea.

Kifungu cha 79 (2) cha CPC kilichoingizwa na sheria ya marekebisho hayo kinasema, “Hakuna maombi ya mapitio ya kesi au rufaa yatakayopelekwa mahakamani dhidi ya uamuzi au amri yoyote ya mahakama ya pingamizi la awali au wakati kesi ikiendelea, isipokuwa kama uamuzi au amri hiyo inaweza kuimaliza kesi.”

Hii ina maana gani kisheria? Katika lugha rahisi ina maana kwamba upande wowote wa shauri au kesi usipinge kwa maombi ya rufaa au mapitio ya amri yoyote ya mahakama wakati kesi ikiendelea au kama kuna uamuzi kuhusu pingamizi la awali.

Kwa mfano, wakili wa upande wa utetezi anaweza kutoa hoja ya kisheria kuhusu kukiukwa kwa namna kielelezo au nyaraka fulani ya ushahidi ilivyoletwa mahakamani.

Nao upande wa mashitaka au ulalamikaji unaweza kutoa hoja kutetea kisheria utaratibu ulioutumiwa kuwasilisha ushahidi husika. Mahakama ikitoa uamuzi wa suala hilo, hakuna upande wowote utakaopinga kwa kukata rufaa au kuomba mapitio katika mahakama ya juu kama vile mahakama kuu.

Nasema hivyo kutokana na hali iliyoanza kujitokeza ya ukiukaji wa sheria hususan katika mashitaka ya jinai.

Kwa mfano, mahakama ya hakimu mkazi au mahakama ya wilaya inapomaliza kusikiliza mashahidi wa upande wa mashitaka na kwa mujibu wa taratibu za CPA, mahakama inapaswa kutoa uamuzi kama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Ikiwa uamuzi ni kwamba mshitakiwa au washitakiwa hawana kesi ya kujibu, wanaachiwa huru. Lakini kama uamuzi ukiwa ni kwamba mshitakiwa au washitakiwa wana kesi ya kujibu, hawapaswi kupinga amri hii kwa maombi ya rufaa au mapitio katika mahakama kuu. Kufanya hivyo ni kukiuka sheria iliyofanyiwa marekebisho. Na. 25 ya Mwaka 2002.

Ina maana kwamba hata jaji mhusika anapaswa kujua hilo au sivyo, ni ukiukaji wa sheria na hata mazoea ya utendaji wa mahakama. Kwani amri au uamuzi wa kwamba mshitakiwa ana kesi ya kujibu huumpa fursa ya kujitetea.

Hapaswi kupinga uamuzi huo ambao una lengo la kumpa fursa hiyo ambayo ni ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (a). Uamuzi atakaoupinga ni ule wa hukumu ya mwisho hasa kama akitiwa hatiani na kupewa adhabu.

Iwapo utaratibu huu wa kisheria utakiukwa kwa mahakama kuruhusu mawakili wapindishe sheria ambayo ina lengo la kudhibiti ujanja-ujanja wa kuchelewesha kesi na pia haki kutendeka ipasavyo na kwa wakati muafaka, itashusha hadhi ya mahakama yenyewe na mfumo mzima wa utawala wa sheria.

Hili pia litaathiri Bunge ambalo hutunga sheria ili zitafsiriwe ipasavyo kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi.

Sitakuwa tayari kusema ni kesi zipi zinaanza kuelekea katika kupotosha sheria, kwani wale mawakili wenye kutaka kufanya hivyo au kama wameshafanya wakisubiri uamuzi wa mahakama, wanajijua.

Hata hivyo, siwalaumu mawakili hao wasomi ingawa sielewi kwa nini hawampi mteja wao fursa ya kujitetea ili watu wote tuone na kusikia ushahidi wake.

Tunachoona sasa ni harakati za mawakili hao wasomi wakitaka kumnasua mteja wao kutoka katika mkono wa sheria kwa njia na gharama yoyote ile. Mahakama Kuu ambako kuna majaji tunaoamini wana upeo mkubwa wa kisheria wanapaswa kukaa chonjo.

Waendesha mashitaka nao wawe wanajiandaa ipasavyo kisheria kuhakikisha wanapinga kwa nguvu ya hoja upotoshaji wa utaratibu uliowekwa kisheria kwa mujibu CPA, ambayo inabainisha wazi kuzuia ucheleweshaji kesi kwa staili hii kama ilivyokuwa zamani.

Wakati huo (kabla ya marekebisho ya sheria), kesi zilikuwa zinapigwa danadana kati ya mahakama za chini na zile za juu, miaka nenda miaka rudi, kiasi cha kushangaza. Hatuhitaji kurudi katika hali ile ya ujima katika masuala ya utawala wa sheria nchini.

0
No votes yet