Anayedai mabilioni ya Dowans ni Rostam


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Rostam Aziz

MJUMBE wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rostam Aziz, ndiye alishitaki serikali na ndiye anaidai Sh. 94 bilioni katika kesi ya Dowans, MwanaHALISI limebaini.

Rostam anadai Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) iliyotolewa tarehe 15 Novemba mwaka jana.

Kampuni ya Dowans Holding S.A ndiyo ilipeana kienyeji mkataba wa kufua umeme na kampuni feki ya Richmond Development Company LLC na baadaye kuunganishwa na TANESCO.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limepata, Rostam ndiye mwenye nguvu ya kisheria (Power of Attorney) kushitaki na kudai fedha za kampuni inayodaiwa kuwa Marekani Kusini na isiyo na ofisi nchini.

Nyaraka hizo ambazo zina utata, zinaonyesha kuwa Rostam alipewa nguvu ya kisheria tarehe 28 Novemba 2005.

Dowans na Richmond – kampuni iliyopewa mkataba kwa upendeleo, huku ikiwa haina fedha, utaalam wala historia ya kufua umeme – zilibadilishana mkataba 23 Desemba 2006 kinyume cha sheria za nchi.

Wiki iliyopita, gazeti hili liliripoti mwanasheria maarufu, mbunge na naibu waziri wa Miundombinu, Dk. Harisson Mwakyembe akisema aliyeleta balaa la Dowans ni Rostam Aziz.

Mwakyembe alinukuliwa akisema ndani ya mkutano wa wabunge wa CCM jijini Dar es Salaam, “…mnahangaika nini? Aliyetufikisha hapa ni mtu mmoja tu; anaitwa Rostam Aziz. Serikali ifanye kila linalowezekana kuhakikisha fedha hizi hazilipwi.”

Nyaraka zinazoonyesha kuwa za bodi ya wakurugenzi wa Dowans Holdings S.A zinathibitisha kutoa mamlaka ya kisheria ya aina hiyo kwa Rostam.

“Nadhani Rostam ni kiongozi pekee duniani kwa sasa, mwenye ujasiri wa kushitaki serikali inayoundwa na chama chake na bado akaendelea kuwa katika uongozi na bila kuchukuliwa hatua yoyote hata baada ya kugundulika,” ameeleza wakili mmoja jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa mamlaka aliyonayo ni pamoja na  kuajiri mawakili, kudai, kushitaki na kupokea malipo yoyote ya fedha kwa niaba ya kampuni.

Kazi nyingine ambazo Dowans ilimpa Rostam ni kufunga na kufungua akaunti za benki za kampuni hiyo na kununua au kuuza hisa za kampuni pale atakapoona inafaa.

Wakurugenzi wa Dowans S.A waliosaini maelekezo hayo ya maandishi walikuwa ni Bernal Zamora Arce anayejitambulisha kuwa rais wa kampuni hiyo na Noemy del Carmen Cespedes Palma ambaye anaonyeshwa kuwa mwanasheria wa kampuni.

Bernal Zamora Arce ndiye mwanasheria mkuu wa serikali ya Costa Rica alieleza mwaka 2008, katika barua yake kwa bunge la Tanzania kuwa hana kampuni iliyoandikishwa na kwamba hata kama ingekuwepo haina anwani kwa maana ya ofisi, simu, sanduku la barua; wala chombo cha kusafiria – gari, pikipiki au baisikeli.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, iwapo mahakama itaamua TANESCO ilipe Sh. 94 bilioni, ni Rostam atakayechukua malipo hayo na kupanga jinsi ya kuyatumia.

Nafasi ya Rostam katika “biashara” hii inamwezesha kudai, kufungua madai, kukazia hukumu, kutumia fedha kwa biashara, kuajiri washauri na maajenti kwa shughuli za kampuni.

Mamlaka ya Rostam yanahusu pia kutetea kampuni, kujibu au kupinga hoja au hatua zozote kisheria zinazogusa kampuni katika biashara zake za sasa na hata za baadaye.

Mwanasheria mmoja jijini Dar es Salaam aliyesoma nyaraka zinazompa mamlaka Rostam, alisema haraka, “Basi huyu ndiye mwenye kampuni. Ama kweli hii ndiyo power of attorney!”

Hati ya mamlaka inampa Rostam uwezo wa kuingia katika biashara na makampuni mengine, kunua hisa na bondi na kuwa na vitegauchumi.

Maelezo kwenye hati ya mamlaka yanasema Rostam ataendelea kuwa na mamlaka hayo hadi atakapopewa taarifa ya kuyasitisha.

Pamoja na mamlaka ya Rostam kushitaki na kukazia hukumu ili kupata akitafutacho, wasuluhishi wa ICC wamekiri kuona kuwa alifanya ushawishi mkubwa katika kuhakikisha kampuni yake hiyo inapata zabuni ya kufua umeme nchini, nje ya utaratibu wa kisheria.

Kwa mfano, wakati wa kesi hiyo, ilielezwa jinsi Rostam alivyotumia mamlaka yake ndani ya serikali kushawishi TANESCO kutoa zabuni ya kufua umeme kwa kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na sifa ya kufanya kazi hiyo.

Rostam alijua, kwa sifa za kawaida za uchambuzi wa zabuni, Richmond isingeweza kupata zabuni hiyo ya kufua umeme mwaka 2006, imeeleza taarifa ya kampuni ya uwakili ya Rex Attorney iliyoitetea TANESCO.

Rex wamesema, katika taaraifa waliyopeleka TANESCO kuwa ICC iligundua kuwa kwa kutumia ushawishi wake, Rostam aliwezesha TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini kuachana na taratibu za kisheria zilizowekwa chini ya Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, na kutafuta mzabuni nje ya utaratibu wa sheria.

Chini ya utaratibu wa kisheria, zabuni hupitiwa na Bodi ya Zabuni ya TANESCO au wizara, lakini zabuni iliyoipa kazi Richmond ilipitia timu iliyondwa na wizara ambayo haikuwa na nguvu ya kisheria.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya Rex Attorney, wapatanishi wa ICC waliridhika na maelezo ya Hans Lottering, mkuu wa idara ya usambazaji umeme TANESCO, aliyedai kuwa alilazimishwa kuweka saini uhamishaji mkataba kutoka Richmond hadi Dowans.

Lottering alidai kuwa aliambiwa “kitu kitamtokea” iwapo asingesaini kuruhusu uhamishaji mkataba.

“Mahakama ilikubali kuwa Rostam alikuwa na nguvu kubwa na ushawishi kiasi kwamba alifanikiwa kuhamisha mkataba huo kwa faida yake na rafiki zake,” wameeleza Rex Attorney.

Ni Lottering huyohuyo ambaye Rex ilimnukuu akiiambia ICC kuwa kama suala la kutafuta wazabuni na kusaini mkataba wa kuzalisha umeme lingeachwa kwa TANESCO, lingechukua muda mfupi kuliko miezi 18 iliyotumiwa na timu iliyoundwa na wizara nje ya utaratibu kwa shinikizo la Rostam.

Rostam amepewa madaraka hayo makubwa na kampuni ambayo si tu uhalali wake wa kisheria unatia shaka, lakini pia bila ya yeye kuwa mmoja wa wanahisa au wakurugenzi.

Hata hivyo, katika uamuzi wake, ICC inatoa tuzo kwa Dowans Holdings S.A na Dowans Tanzania Limited.

Kampuni inayoitwa Dowans Tanzania Limited (DTL) haitajwi popote wakati wa Richmond na Dowans ya Costa Rica zikibadilishana mkataba.

Kilichoitwa Dowans Tanzania Limited kinadaiwa kuanzishwa mwaka 2006 na mmoja wa wakurugenzi wake akiwa Brigedia Jenerali Sulaiman Mohamed Yahya Al Adawi ambaye ni raia wa Oman.

Bali brigedia huyo alipoulizwa juu ya kampuni hiyo, alikana katakata kuwa mmiliki na kusena hana biashara inayohusiana na umeme.

Serikali imekuwa kimya juu ya Richmond hadi ilipoanikwa na bunge; lakini imeendelea kuwa kimya juu ya Dowans hadi juzi tu mahakama ya kimataifa ilipotoa hukumu ya kulipa Dowans.

Hatua ya serikali kujitokeza mwishoni kutaja wamiliki wa Dowans ili “wachukue tuzo,” imejenga shaka kwa nini serikali hiyohiyo haitaji wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kagoda inadaiwa kuchota zaidi ya aSh. 40 bilioni kutoka benki Kuu ya Tanzania (BoT) tangu 2005 lakini, pamoja na kuwepo taarifa za mabenki ambamo fedha zilipitia, serikali imekaa kimya.

Rostam Aziz, ambaye ni mbunge wa Igunga, rafiki wa Rais Jakaya Kikwete, amekuwa akitajwa kumiliki Kagoda, lakini mara zote amekana kuifahamnu; kama ambavyo amekuwa akikana kufahamu Richmond na Dowans.

0
Your rating: None Average: 3.8 (5 votes)
Soma zaidi kuhusu: