Anenayo leo Profesa Abdallah Safari


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

PROFESA Abdallah Jumbe Safari ni mtu wa vipaji vingi. Ni mwanasheria aliyebobea. Ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na mtunzi wa vitabu vya riwaya na vya taaluma yake.

Hata hivyo, wiki iliyopita, jina lake lilitawala katika vyombo vya habari kwa jambo jingine tofauti ambalo analipenda sana – siasa.

Profesa Safari alitangaza rasmi kwamba ameamua kuacha kuwa mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF). Amekuwa mwanachama wa chama hicho tangu mwaka 1995.

Alijiunga na CUF kipindi kifupi baada ya kurejea nchini kutoka nchini Uingereza alikokuwa kwa ajili ya masomo ya shahada ya juu ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Sussex.

“Nimeamua kutoka CUF lakini sijapanga kujiunga na chama chochote kwa sasa. Nilijiunga na CUF kwa sababu niliamini katika itikadi yake ya ‘haki sawa kwa wote’ ambayo naona sasa wameachana nayo.”

Hadi Jumatatu, profesa Safari alikuwa hajatangaza uamuzi wa kuhamia chama chochote kingine. Bali alisema kwamba atafanya hivyo akishafanya utafiti wa kujua chama kinachomridhisha kwa sera na malengo yake.

Anasema, “Nitajiunga na chama ambacho kitafuata haki. Katika vyama vilivyopo sasa, sijaona chama chenye itikadi hiyo. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kuwa nitaacha siasa. Mimi ni muislamu na siasa ni sehemu ya imani yangu.”

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Profesa Safari  anasema itafika wakati atataja chama kinachomfaa kushiriki siasa.

Mwanasheria huyo alijiunga na CUF kama mshauri wa sheria wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, na alikitetea chama hicho katika kesi mbalimbali.

Akiwa mwajiriwa wa Chuo cha Diplomasia (CFR) kinachomilikiwa na serikali, Safari alimtetea Lipumba katika kesi ya uchochezi ya mwaka 2001 ambayo ilitokana na mauaji ya Zanzibar ya Januari 2001. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kufukuzwa kazi kwake serikalini.

“Nakumbuka siku hiyo (Februari, 2001) nilikwenda mahakamani kumtetea Lipumba kwa vile mimi ndiye niliyekuwa mwanasheria wake. Mara baada ya taratibu za mahakamani, Lipumba alipewa dhamana na kuruhusiwa kuondoka mahakamani.

“Sasa mimi nilikuwa na gari yangu binafsi aina ya Mercedes Benz yenye namba T 246 CD 23. Lipumba hakuwa na gari na nje kulikuwa na mkusanyiko wa wapenzi na wanachama wa CUF.

“Kwa vile yeye hakuwa na gari, nikaona ni vema nimpe lifti. Tulipoingia kwenye gari watu wakataka waisukume hadi tutakapoishia. Hata hivyo, nikaendesha na nikampeleka Lipumba ofisini kwake Buguruni na mimi nikaenda ofisini kwangu CFR kule Kurasini.
 
“Siku chache baadaye, nikaanza kusikia maneno kuwa nimetumia gari ya ofisi kumbeba Lipumba. Lakini ile haikuwa gari ya serikali, ile ilikuwa gari yangu binafsi.

“Hayakuisha. Nikaambiwa niache gari yangu ofisini na nisitembee nayo. Nikasema hilo haliwezekani, gari yangu itabaki vipi ofisini. Lakini ofisini nilikuwa na gari ya ofisi, nayo ni Mercedes Benz yenye namba T 246 CD 26. Kama unavyoona, gari zote hizo zina namba za kibalozi.

“Mkuu wa chuo, Profesa Abilahi Omar, akaniambia kama sitaki kuacha gari ofisini, basi nibandue namba zile za kibalozi. Hilo nikakubali. Gari ya ofisi ikaachwa iozee palepale nilipoiegesha mara ya mwisho hadi ikaota majani.

Akizungumza kwa uchungu, Profesa Safari alisema ilipofika tarehe 2 Novemba, 2001, CFR wakamkabidhi rasmi barua ya kumfukuza kazi ingawa anasema dalili za kufukuzwa alikuwa ameanza kuziona mapema.

“Tayari nilikuwa nimepanga kwenda katika Chuo Kikuu cha Aberdeen nchini Scotland kwa ajili ya likizo ya utafiti mwaka huo. Tayari nilikuwa nimeshafunga mizigo yangu nikijiandaa kwa safari.

“Kufukuzwa kwangu maana yake ni kuwa nilikosa likizo hiyo. Baba yangu mzazi, Kapteni Jumbe Safari, alikuwa Dar es Salaam wakati huo na aliposikia nimefukuzwa kazi alipata ugonjwa wa kiharusi na ndiyo tatizo lililokuja kumuua miaka minne baadaye.

“Nimefukuzwa kazi, hakuna hata kiongozi mmoja wa CUF aliyekuja kunifariji. Nakumbuka nilikwenda kumpa taarifa Lipumba nikamkuta anafanya shughuli zake kwenye laptop na alichofanya ni kutoa jibu la ‘sawa’ na kisha kuendelea na shughuli zake.

“Kuna fedha za kuwatetea kwenye kesi nilizokuwa nawadai nikamkumbusha kuwa sasa sina kazi na wanisaidie kwa kunilipa, akasema chama hakina hela.

“Matokeo yake mimi nikaanza kuuza mali zangu ili nisomeshe watoto wangu na wengine ninaowalea. Na baba yangu alipofariki dunia, sikusikia chochote kutoka CUF.

“Leo hii, mtu anasimama na kuhoji eti Safari ameifanyia nini CUF? Yaani yote yale niliyoyafanya zawadi yake ndiyo ile ya kuzomewa na wanachama kwa sababu ya kutaka kuwania uongozi. Ngoja nipumzike,” alisema.

Profesa Safari anasema juhudi zake za kutaka alipwe haki zake kwa sababu alifukuzwa kazi bila ya makosa zimegonga mwamba kwa sababu CFR anayotaka kuishitaki ina kinga ya diplomasia.

“Ili mtu uishitaki CFR ni lazima serikali ikubali kuondoa kinga hiyo ya kidiplomasia. Wakati Kikwete (Rais Jakaya), alipokuwa waziri wa mambo ya nje nilijaribu kuonana naye ili anisaidie kwenye hilo lakini alikataa kuzungumza na mimi.

“Ndiyo maana mimi nasema Kikwete si mtu anayejali utawala wa sheria. Kama angekuwa anajali hilo, angeondoa ile kinga ya kidiplomasia ili mimi na Watanzania wenzangu wenye madai yao dhidi ya CFR tupate haki zetu mahakamani,” alisema.

Katika sakata lake hilo, Safari anasema watu maarufu kama Samuel Sitta, Patrick Chokala, Jenerali Davis Mwamunyange, Profesa Hassa Mlawa waliokuwa wajumbe wa bodi ya CFR walibariki maamuzi ya kufukuzwa kwake.

Hata hivyo, anasema hataweza kusahau mchango wa wasomi maarufu nchini akiwataja kuwa ni Profesa Issa Shivji na Profesa Jwan Mwaikusa aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliotumwa nyumbani kwake wakati akirejea kazini.

Anasema wasomi hao walisimama kidete kumsaidia ili kuhakikisha anapata haki zake kwenye suala hilo.

Profesa huyo aliyezaliwa tarehe 3 Juni, 1951, anasema kwa sasa anataka kujikita zaidi kwenye uandishi wa vitabu vya taaluma na riwaya ili kuwanufaisha wananchi na vipaji vyake.

“Sina kesi nyingi za kutetea watu mahakamani na nimeondoka CUF jambo linalomaanisha nitakuwa na muda mrefu zaidi wa kufanya mambo yangu binafsi kama vile uandishi wa vitabu.
 
“Mimi huamka mapema alfajiri ili niswali swala ya asubuhi. Baada ya hapo, kichwa changu huwa freshi na hapo ndipo ninapoweza kuandika vizuri zaidi. Masaa matatu au manne ya asubuhi baada ya swala ndiyo ninayoyatumia kuandika,” anasema.

Baadhi ya vitabu ambavyo Safari tayari ameandika ni Mashitaka ya Jinai na Utetezi; Kabwela; Harusi; Joka la Mdimu; Msomi; Examination of Witness in Trials, Uandishi wa Manufaa na Ndani ya Treni.

Tofauti na wanasheria wengi ambao hujisikia fahari kwa kuzungumza kiingereza, Safari anasikia fahari zaidi kwenye Kiswahili.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, profesa Safari anasema baba yake ndiye mtu aliyemsababishia mahaba makubwa na lugha hiyo.

“Baba yangu alikuwa akipenda sana kusoma mashairi ya watu kama vile Abushiri Mbwana na Shaaban Robert. Kwa ujumla alipenda sana lugha hiyo na mimi nimerithi kwake.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: