Anguko kuu la CCM


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

USHINDI wa CHADEMA katika jimbo la Arumeru Mashariki, “ni ushahidi kwamba wananchi wakielewa watafanya mapinduzi ya kisasa.”

Hiyo ni kauli iliyorudiwa na viongozi wengi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo walipokuwa wanaulizwa “maana ya ushindi” wa chama chao katika jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.

Mmoja baada ya mwingine, walisema ushindi huo ni anguko la Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba nguvu yake ya rushwa ya kugawa vyakula na fedha taslimu, matusi na vitisho, havikufua dafu kwa maamuzi ya wananchi.

Katika uchaguzi mdogo, Joshua Nasari wa CHADEMA, ameibuka kidedea kwa kumbwaga mgombea wa CCM, Sioi Sumari. Nassari (27) alipata kura 32,972 wakati Sioi alipata kura 26,296.

Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa ameliambia gazeti hili kuwa matokeo ya uchaguzi huo ni hukumu dhidi ya CCM.

“Ni hukumu kwa waliodiriki kudanganya katika kampeni na maisha yao ya kila siku,” alisema kwa njia ya simu juzi kutoka Arumeru.

“Ni hukumu dhidi ya ufisadi. Wananchi sasa wameondoa hofu. Sauti yao imeanza kusikika kwa Mungu kwamba wanahitaji viongozi safi,” amesema.

Mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando, akihojiwa kwa njia ya simu amesema, “Kwa mtindo huu, CCM ijiandae kuwa chama cha upinzani.”

Mbali na uchaguzi wa mbunge, kulikuwa na uchaguzi wa madiwani katika kata nane ambapo CHADEMA imechukua kata tatu, CCM nne na Chama cha Wananchi (CUF) moja.

Ushindi wa CHADEMA umechukuliwa kuwa kielelezo cha kuzidi kuaminiwa na wananchi, umoja ndani ya chama, uongozi thabiti, kukubalika kwa sera hata kaulimbiu yake ya “nguvu ya umma.”

CHADEMA imefanikiwa kutwaa kiti cha ubunge jimbo la Arumeru Mashariki ambapo mgombea wake Joshua Nasari amekuwa mbunge baada ya kumbwaga mgombea wa CCM, Sioi Sumari.

Viti vya udiwani ambavyo CHADEMA wamebeba ni katika kata za Kirumba, Mwanza; Kiwira, Mbeya na Lizaboni, Songea, huku CCM ikitwaa kata za Logangabilili, Bariadi; Chang’ombe, Dodoma; Vijibweni, Dar es Salaam na Kiwanga, Bagamoyo. CUF imetwaa Msambweni, Tanga.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema ushindi wa Arumeru Mashariki unaonyesha “CCM inaweza kuondoka madarakani mwaka 2015.”

Lissu ambaye ni mwanasheria na mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni amesema, “…ushindi uliovunwa na CHADEMA juzi ni zaidi ya kuongeza mbunge mmoja. Tumepambana na mapesa mengi ya CCM, mfumo mbovu wa uchaguzi na dola.”

Hata hivyo, Lissu amesema kwa namna ushindi huo ulivyopatikana, na kama “…tukitaka kushinda katika uchaguzi mwingine mdogo pamoja na ule mkuu wa 2015, lazima tijipange.”

Mbunge mmoja wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa, amesema jijini Dar es Salaam kwamba chama chake kisingeshinda Arumeru Mashariki kutokana na migawanyiko inayokitafuna.

Ametaja makundi yaliyojitokeza tangu uchaguzi mkuu wa 2010, kwamba hayakuvunjwa; na kila moja linaendeleza mikakati ya kutafuta nguvu zaidi kwa ajili ya uchaguzi ujao 2015.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano imesaidia CHADEMA kung’amua yale ambayo yangewakwaza katika matumizi ya kompyuta.

Katika hatua nyingine, katibu mwenezi wa CCM, Nape Nnauye ameviambia vyombo vya habari kuwa CCM “imeshindwa kihalali.”

“Tumeshindwa na ushindi wa wenzetu ni ushindi halali. Hatuna cha kulalamikia pamoja na kujua yapo matatizo madogo yaliyotokea,” alisema juzi Jumatatu.

Kiti cha Arumeru Mashariki kilibaki wazi baada ya kifo cha Jeremiah Sumari. Mtoto wake, Sioi ndiye alikuwa mgombea wa CCM.

Victor Kimesera, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA amesema, “Hakuna anayeweza kusimamisha kile kilichofikia kubadilika. Wakati umefika wa watu kuchagua wanachokitaka. CCM hawawezi tena kujivuna kuwa hawataondoka madarakani.”

Ushindi wa kiti cha ubunge cha Arumeru Mashariki, unafikisha viti vya majimbo vya CHADEMA kuwa 24. Idadi ya wabunge wake wote sasa ni 49.

Alipoongea na mwandishi mwingine wa gazeti hili, Lissu amesema chama chake kina kazi kubwa ya kufundisha umma elimu ya uraia ili kupata watu watakaojiamini kuingia kwenye mchakato wa kutafuta uteuzi wa kugombea uongozi.

Lissu amesema “CCM imebakibaki tu. Ni chama cha jana na juzi. Mvuto wake kwa wananchi umetoweka. Hata ukifanya tathimini ya mikutano yake utagundua hilo; lakini CHADEMA ni chama cha leo na kesho.”

Anasema, “CHADEMA ni macho, masikio, mdomo na pua kwa wasio na nafasi. Sisi huwasikiliza watu, kuwaelewa, kutafakari na kuzungumza hoja zao.”

Ufadhili kwa CHADEMA umekuwa moja ya nguzo zake kuu. Philemon Ndesamburo, mbunge wa chama hicho jimbo la Moshi Mjini, alichangia Sh. 20 milioni wakati wa michango rasmi kwa chama chake. Vilevile alitoa helikopta.

CHADEMA iliendesha harambee iliyopewa jina la Movement for Change (M4C) katika hoteli ya Naura Springs, mjini Arusha ambako ilichangiwa mamilioni ya shilingi na watu wa rika na uwezo tofauti kiuchumi.

“Mimi najua wapo wafanyabiashara wenye uwezo wa kutoa msaada lakini tunawaambia wao kama wanaona waendelee kuchelewa kuchangia CHADEMA, wengine tunaanza; labda watakuja baadaye,” alisema Ndesamburo wakati akikabidhi mchango wake.

Hivi sasa CHADEMA imepata uzoefu wa kutosha katika kusimamia na kulinda kura zake kwa njia ya kupata mawakala wenye ujuzi na jasiri ili kudhibiti mbinu za wizi wa kura zinazotajwa kutumiwa na chama tawala.

Wachambuzi wa masuala ya siasa na viongozi wa vyama mbalimbali, kwa siku ya juzi na jana, wamesema matokeo ya chaguzi za Jumapili iliyopita, yanaonyesha “nguvu ya umma” ina uwezo wa kuondoa serikali ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

0
Your rating: None Average: 3.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: