Anguko la CCM dhahiri


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 August 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekasirika. Sasa inashusha hasira zake kwa wabunge, Spika na Bunge lenyewe. Viongozi wanajua fika kuwa Bunge, kama Serikali na Mahakama, ni mhimili wa dola.

Mihimili hii hufanya kazi kwa niaba ya wananchi. Serikali inatawala. Bunge linatunga sheria. Mahakama inasimamia utekelezaji wa haki kisheria.

Majukumu ya bunge, pamoja na kutunga sheria, ni kuwa chombo cha uwakilishi cha wananchi na kushauri na kusimamia serikali.

Sasa CCM na serikali yake vinaona bunge linafanya zaidi ya linachopaswa kufanya. Eti bunge limeingilia utawala. Inashutumu kiongozi wa bunge, Spika, kwamba analiongoza vibaya, hivyo kutingisha mamlaka ya serikali.

Ni kweli kwamba serikali inaongozwa na sera za chama kilichochaguliwa wakati wa uchaguzi mkuu, lakini kwa bahati mbaya, chama hakipo Ikulu. Aidha, chama siyo mhimili wa dola.

Tunasikitika basi kuona chama chenye serikali kikimshambulia Spika, katika vikao vyake vya ndani, kuwa anadhoofisha serikali.

Inasikitisha zaidi pale inapofahamika chama hikihiki kinashambulia wabunge wake; kinawatisha na kutaka wasiikosoe serikali. Mbona CCM inajua kuwa yenyewe ni bomba tu la kupitishia wabunge lakini wabunge ni wa wananchi majimboni?

CCM inaweza kutamba inao wabunge wengi, lakini ukweli unabaki palepale: hawa ni wawakilishi wa wananchi, siyo chama.

Tunashangazwa na utamaduni huu wa CCM kushambulia na kutisha wabunge. Tunasikitishwa pia chama hiki kuandaa ukumbi, mazingira na hoja za kutumia ili kushambuliwa Spika.

Tunaona CCM na viongozi wake wa ngazi za juu na chini, wamepotea njia. Kama wanataka heshima ya jamii, sharti warudi kwenye mstari. Kwa nini?

Wanalifahamu tatizo la msingi linalozua yote hayo, isipokuwa wanalikwepa. Mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) alilieleza tatizo hilo kuwa ni ufisadi.

Ufisadi umefanya CCM kuwa jamvi. Umeiegemea. Kila ukitajwa unabubujikwa jasho. Ndipo unachukua CCM, kama taulo, na kujipangusia; na kujifunikia uso. Hii ni hatari kubwa.

Kinachotusumbua ni CCM kufanya ufisadi kuwa jambo la kawaida nchini. Kwa makusudi au kwa woga, kinaambukiza uovu kwa wadogo na wakubwa na hata kwa vizazi vijavyo.

Tunapinga kwa nguvu zote juhudi za kuzima uhuru wa wabunge na bunge na kufanya wananchi wakose wawakilishi thabiti na jasiri.

Tunapinga njama za kuziba midomo ya wananchi. Bali hizi ni dalili za anguko kubwa la CCM muda si mrefu ujao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: