Anna hataki kuelezwa, anakula bila kunawa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

HII inaweza kuwa nchi ya wendawazimu. Kama siyo, basi sote tumelogwa. Jaribu kufikiria hili, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Anna Abdallah, ambaye pia ni mbunge wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), analipuliwa bungeni kwamba wanajilipa fedha kwa mamilioni kwenye vikao vya bodi tena wengine wakilipwa mara mbili, naye anakiri, lakini anageuka hapo hapo na kuuliza, “Kwa nini iwe nongwa kujilipa hivyo?”

Anna ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe kabisa nchini, tena akiwa mwanamke wa kwanza kuweka historia nchini kuwa mkuu wa wilaya na  mkuu wa mkoa wa kwanza mzalendo, anakwenda mbali zaidi na kuhoji “kwa nini iwe nongwa kwa mjumbe wa bodi kulipwa posho yeye na msaidizi wake ambaye ni mkewe?”

Anasema mjumbe huyo, Mudhihir Mudhihir, aliamua kumfanya mkewe kuwa msaidizi wake kutokana na ulemavu wa mkono, na kudai kwamba hata bungeni kuna wabunge walemavu na wana wasaidizi ambao hulipwa. Anna huyo!

Naomba kuwakumbusha wasomaji juu ya kauli za watu wenye shibe ambazo zilipata kutolewa nchini.

Basil Pesambili Mramba, akiwa waziri wa fedha, alikuwa na jeuri na kiburi cha madaraka. Jeuri ya shibe alionyesha alipowaambia wananchi kuwa ikibidi watakula nyasi lakini lazima ndege ya rais inunuliwe kwa kuwa rais hawezi kupanda punda. Mramba!

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andew Chenge wakati huo akiwa waziri wa miundombinu, aliweka wazi kuwa fedha zinazolalamikiwa dola milioni moja (Sh. 1.2 bilioni) kuwa amejiwekea akiba ughaibuni zikituhumiwa kuwa zilitokana na rushwa ya rada ni vijisenti tu.

Kwa viwango vya Chenge, fedha hizo ni vijsenti. Chenge!

Yupo Tingatinga; huyu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu, John Malecela, ambaye pia alipata kuwa waziri mkuu, waziri, mkuu wa mkoa na balozi wa Tanzania Uingereza. Wakati akiwa Waziri wa Uchukuzi aliwaambia wananchi waliokuwa wanalalamika kuhusu huduma mbovu ya usafiri wa treni, kwamba wanaweza kwenda kuzimu. Alitumia kimombo they can go to hell.  Malecela!

Kauli ya Anna aliyotoa wiki iliyopita akijitetea dhidi ya tuhuma alizobebeshwa na msemaji wa kambi ya upinzani katika Wizara ya Kilimo na Chakula imenikumbusha kauli hizo za watangulizi wake.

Kauli hizo ni kielelezo cha kukataa kuwajibika juu ya makosa yaliyotendwa na wenye dhamana katika kusimamia maeneo mbalimbali katika utumishi wa umma.

Ni kauli za kibabe na kujivimbisha, ni kielelezo cha wazi kwamba taifa hili limeshindwa kabisa kujenga uwajibikaji kwa wanaokabidhiwa ofisi za umma.

Ni kauli zinazotufundisha kwamba kama taifa tumejenga utamaduni wa kukataa kuulizwa juu ya maovu yanaotendeka chini yetu na hata yale ambayo tunayafanya wenyewe kwa mikono yetu wenyewe au hata kwa baraka zetu kama wasimamizi wa maeneo hayo.

Hali hii ndiyo ilijitokeza wakati wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walipoanzisha kampeni ya kupiga vita utamaduni wa wabunge kujirundikia posho za vikao vya wabunge.

Kwa kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda alionyesha udhaifu na woga kupambana katika vita vya posho, akaungana na wabunge wa CCM kupeleka kwa rais mapendekezo ya nyongeza ya posho za wabunge.

Alipigwa butwaa baada ya kujikuta kuwa ametangaza nyongeza ya posho wakati rais alikuwa amesema hapana.

Inawezekana, kulikuwa na kupishana maneno kati ya Spika Makinda na Rais Jakaya Kikwete kwa sababu tu mmoja kati yao alisoma upepo na kuamua kugeukia kwa wengi – umma, akaziruka posho na mwingine akabaki na aibu hadi kesho.

Tabia hii ya kukataa kuwajibishwa ndiyo ilimponza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati, David Jairo, alipobainika kuchangisha fedha kinyume cha taratibu kutoka kwa taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo ili eti ‘kusaidia’ kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo.

Wale wafanyakazi wa wizara hiyo waliomlaki Jairo kwa nderemo na vigelegele pale wizarani wakiimba ‘baabaa baba, baba huyo…’ akiwemo aliyekuwa waziri, William Ngeleja, nao hawakuwa wanafanya kitu kipya, ila kuwasilisha ujumbe mmoja kwamba hakuna kuwajibishana katika uendeshaji wa ofisi za umma.

Nimechukua sehemu kubwa ya makala kuzungumzia vituko vinavyofanywa ndani ya ofisi za umma kwa nia moja tu, kuonyesha kwamba kila wananchi wanapolalamika kuwa huduma hii au ile iliyopaswa kutolewa na serikali kama vile ujenzi wa barabara, madaraja, huduma bora za afya, maji safi, elimu na nyinginezo nyingi, maelezo yamekuwa hakuna fedha.

Kimsingi siyo kwamba hakuna fedha, ila hakuna utayari wa kuwa makini na kusimamia rasilimali zilizoko, kila mmoja anajitafunia kwa wakati wake. Maamuzi mengi ni ya ovyo katika kutumia rasilimali za umma.

Kwa bahati mbaya sana, wanaofanya maamuzi ya matumizi ya rasilimali hizo hawawajibiki kwa maamuzi hayo, hata pale wanapoulizwa wanabaki wakishangaa kuhojiwa na kuona wanaohoji hawajui wasemalo, wana nongwa. Ndiyo maana ya ‘kwenda kuzimu’ au ‘kula nyasi’ au ‘vijisenti’.

Mwaka huu eneo la kusini mwa Tanzania, mkoani Mtwara kulikuwa na machafuko makubwa, wakulima wa korosho walicharuka kutokana na kudai malipo yao ya pili ya korosho.

Wakulima hao katika wilaya ya Tandahimba, walifanya vurugu kisha wakavamia kituo cha polisi, vibanda vya biashara na kuchoma moto baadhi ya mabanda huku wakiishinikiza serikali iwalipe malipo ya pili ya mauzo ya mazao yao.

Kuchelewa kwa malipo hayo kulileta madhila makubwa kwa wakulima wa korosho, kiasi cha kuibua hoja ya  kukataa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Bungala, ni miongoni mwa viongozi wa wananchi aliyeweka wazi suala hilo bungeni kwa kulieleza kuwa mfumo huo kwa wakulima wa Kilwa hauwafai kutokana na kutaabika kwa kutolipwa fedha zao kwa wakati.

Alisema wakati mwingine kulipwa fedha kidogo tofauti na matayarisho ya zao hilo, kauli yake iliungwa mkono na takriban wabunge wote wa kusini.

Wakati wakulima wa korosho wakiugulia njaa na mateso ya kutolipwa fedha zao, bodi yao inayoongozwa na Anna, siyo tu ilikuwa inaendelea kutumbua fedha za walipa kodi, bali pia utumbuaji wenyewe umejaa ujanja ujanja kama ambavyo ilionyeshwa bungeni wiki iliyopita na msemaji wa kambi ya upinzani, Rose Kamili.

Anna anasema madai hayo ni nongwa, kwamba waliopeleka nyaraka kwa kambi ya upinzani juu ya utafunaji wa fedha za umma, akiwamo yeye mwenyewe na wenzake wanne kulipwa jumla ya Sh. 7,325,000 katika kikao kimoja tu cha Bodi ya Korosho kilichokaa Novemba 29, 2011 ni nongwa.

Hivi ipi nongwa, kula bila kunawa au kuhojiwa kwa nini unakula bila kunawa?

Kwa nini Anna anapata ujasiri wa kusema haya? Ni kwa sababu anaendeleza utamaduni ule ule wa kina Malecela, Mramba, Chenge na wengine wengi. Hakuna wa kuwauliza hata kama wakila bila kunawa, kufanya hivyo ni nongwa. Kweli Anna anajua kuupepeta!

0
Your rating: None Average: 4.4 (7 votes)