ANNA MAKINDA: Waliombeba ndio watakaomwangusha


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

SPIKA mpya wa Bunge la Jamhuri, Anna Makinda anatabiliwa kuwa na wakati mgumu. Wengine wameanza kudai kuwa amekalia kutikavu. Laweza kukatika wakati wowote na kusababisha maafa kisiasa.

Akifika mwisho wa muhula wa miaka mitano, atakuwa amefanikiwa sana; bali wanaoweza kumwangusha ni walewale walioshiriki kumtwisha uspika.

Baadhi ya waliopalilia njia yake kutoka naibu spika hadi alikofikia wanasema, kwa jinsi alivyoingia madarakani, “…yawezekana asimalize hata miaka miwili katika kiti chake.” Wanaorodhesha sababu.

Kwanza, Bunge la Makinda limejaa migawanyiko. Limejaa visasi, shutuma na lawama, huku hadi kule.

Ni bunge hili lililojaa wabunge vijana, wasomi na wanasiasa wenye uwezo na ushawishi mkubwa, Bali, lina kambi mbili kuu zinazotofautiana.

Kambi moja ni ile inayoundwa na Edward Lowassa kwa kushirikiana na swahiba wake mkuu, Rostam Aziz; nyingine inaundwa na Samwel Sitta na kundi lake la zamani la wapinga ufisadi.

Ndani ya kambi hizi kuna mnyukano wa kila aina na sasa umeingiza hata wasiotarajiwa. Baadhi yao, wapo waliokuwa na wanaotarajiwa kuwa mawaziri.

Wengine ni watendaji katika taasisi za umma na serikali; viongozi kutoka chama kilichopo ikulu, wanachama wa kawaida na wafanyabiashara wa ngazi mbalimbali.

Nako bungeni makundi yanahusisha baadhi ya watendaji wa ofisi ya Bunge na spika mwenyewe. Kila mmoja anatetea anayemhusu.

Kinyang’anyiro cha “urais mwaka 2015,” kilichoanza miaka sita iliyopita, kitazidi kukiweka kiti cha Makinda shakani.

Wakati wengi wanaona Lowassa “hana sifa ya kukabidhiwa uongozi wa taifa,” wafuasi wake hasa Rostam, anaamini kuwa “hakuna wa kumzuia Lowassa kumrithi Kikwete.”

Msisitizo huo ndio uliosukuma wastaafu walioshiriki kongamano la miaka 10 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kujitokeza hadharani kukemea wanasiasa wanaotafuta madaraka kwa nguvu.

Kongamano ambalo lililofanyika, 1 Novemba 2009, lilitoa wito kwa wananchi kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kuondoka kwenye “minyororo ya utumwa wa wanaojiita wafanyabiashara.”

Mmoja wa washiriki, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema, “Mimi ni mzee, nina miaka 72… Msaidieni rais aondokane na wezi waliomzunguka.” Naye aliahidi kusaidia katika hilo.

Hakumtaja kwa jina yule aliyedai amemfunga minyororo rais. Hakusema ametoka wapi, yuko wapi na anafanya nini kwa sasa.

Hata hivyo, baadhi yao waligundua kuwa Butiku alikuwa anamzungumzia mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini – mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kampuni ya Kagoda ndiyo ilivunja rekosi ya wizi Benki Kuu (BoT) kwa kukwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni katika siku tatu na kuzitawanya katika mabenki mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Lakini hata baada ya kukwapua mabilioni hayo, hakuna yeyote aliyefikishwa mahakamani. Fedha hizo ndizo upinzani umekuwa ukidai zilitumika kumwingiza Kikwete madarakani.

Taarifa kwamba Kagoda imeshiriki katika wizi wa mabilioni ya shingi na wahusika hawajafikishwa mahakamani, zimepenya masikioni mwa wabunge wengi wa bunge la sasa.

Hivyo basi, hatua yoyote ya kutaka kuibeba Kagoda, au kuifumua, inamweka Makinda katika wakati mgumu wakati wa kutekeleza kazi zake.

Mtihani mwingine ambao Makinda anakabiliana nao, ni mgawanyiko wa wabunge kambi ya upinzani.

Kuna taarifa kwamba viongozi wakuu wa Chama cha Wananchi (CUF), wameanza ushawishi kwa uongozi wa Makinda kubadilisha kanuni za Bunge ili ziweze kukibeba chama chao.

Wanataka kuundwa kwa kanuni mpya zitakazotambua vyama ambavyo vina wabunge wachache.

Wachunguzi wanasema lengo la CUF na vyama vingine vidogo, ni kutaka kuwapo kwa kambi mbili za upinzani bungeni ili kukidhofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015.

CHADEMA ambacho ndicho kinaunda kambi rasmi ya upinzani bungeni, kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Wakati CUF ikiwa kambi rasmi bungeni, CHADEMA haikuwahi kudai kuwa kambi ya pili yenye kuhitaji huduma na uwakilishi tofauti.

Iwapo Spika Makinda ataruhusu hili kufanyika, ama kwa kutoelewa au kwa kuitika CCM na CUF katika kutaka kudhoofisha CHADEMA, mambo mawili yataweza kutokea.

Kuibuka uhasama kati ya wabunge wa CHADEMA kwa upande mmoja na uongozi wa spika kwa upande mwingine.

Na kwa vile CHADEMA ndiyo inayounda kambi rasmi ya upinzani bungeni, Spika Makinda aweza kushindwa kuendesha Bunge kama alivyoahidi.

Lakini jingine ni kwamba, uhasama kati ya uongozi wa Makinda na kambi ya upinzani bungeni, unaweza kuwaingiza nchi wahisani, wanaotoa fedha kuendesha shughuli za Bunge.

Hayo yakitokea, hadhi ya Bunge na serikali kwa jumla, itakuwa imeporomoka.

Aidha, Makinda ameingia katika kinyang’anyiro cha uspika kupitia mlango wa uwani. Ni kwa sababu, Rais Kikwete hakumueleza aliyekuwa bosi wake, miaka mitano iliyopita, Samwel Sitta kwamba hatamhitaji tena.

Wala Makinda mwenyewe hakumweleza Sitta juu ya azma yake ya kuwania nafasi ya spika. Kabla ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, Makinda hakukutana na Sitta kujadili sababu zilizomsukuma kuwania kiti hicho.

Ni mazingira haya ambayo yamefanya baadhi ya wafuasi wa Sitta kutuhumu Makinda kuwa “ametumwa na mafisadi” kummaliza mpiganaji mwenzao.

Ufa miongoni mwa viongozi hawa wawili unaongezeka hasa kutokana na kuwapo kwa Sitta na baadhi ya wafuasi wake bungeni, pamoja na Makinda na wafuasi wake.

Kuwapo kwa makundi hayo mawili, bila shaka kutazidisha ufa miongoni mwa wabunge wa pande hizo mbili.

Tatu, Makinda alikuwa msaidizi mkuu wa Sitta wakati Bunge lilipounda Kamati Teule iliyochunguza mkataba tata kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Bunge lililokuwa chini ya uongozi wa Sitta na Makinda ndilo lililojenga mazingira ya Lowassa kukimbia nafasi ya waziri mkuu.

Hapa Makinda atakuwa amejiongezea maadui wawili kwa wakati mmoja – Lowassa na Sitta.

Anajua kuwa hakuna mahali popote katika kumbukumbu za bunge panapoonyesha kuwa Makinda alipinga hatua ya bunge kumfukuza Lowassa.

Si hivyo tu: Makinda anajua kwamba ni rahisi mno Lowassa kusamehe Sitta, kuliko kumsamehe yeye.

Hii inatokana na mtandao wa Kikwete kumtambua Makinda kuwa katika kundi lililoitwa “Mwandosya Project” – mradi wa kumuingiza ikulu Profesa Mwandosya.

Lakini kwa jinsi alivyoingia madarakani, sasa anadaiwa kugeuka kuwa wa “Lowassa Project” – mradi wa kumsafisha Lowassa.

Bali, hiki kinachotendeka sasa, ni kile wengi wanachoita, “geuza adui mmoja rafiki ili kummaliza mwingine.”

Wachunguzi wanasema, kazi ya kummaliza Sitta imekamilika. Atakayefuata baada ya Sitta, bila shaka atakuwa Makinda.

Hata hivyo, akina Lowassa wanajua kuwa Makinda hawezi “kumilikiwa kisiasa” na makundi mawili kwa wakati mmoja.

Baadhi ya wanaomfahamu Makinda wanasema, kama alivyomgeuka Sitta ndiyo anavyoweza kugeuka akina Lowassa.

Jingine ambalo linamweka Makinda katika utata, ni kauli yake kwamba anataka “siasa za kitafiti na si zile za kuzua maneno.”

Kwa kawaida, kauli hii imekuwa inahubiriwa kwa nguvu na baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi.

Miaka mitatu baada ya kung’oka katika kiti chake, Lowassa bado analalamika. Anasema kilichotokea bungeni kilitokana na wivu wa kutaka uwaziri mkuu wake.

Pamoja na kuwepo uthibitisho kwamba Lowassa alitenda kosa kwa kuipa upendeleo kampuni isiyokuwa na hadhi ya Richmond, bado anaendeleza madai yake hayo.

Nne, kiti cha Makinda kinakuwa moto kwa kuwa anakuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza bunge lililojaa wanawake wengi. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 30 ya wabunge wa sasa, ni wanawake.

“Sisi wanawake tuna kasoro zetu. Hata pale ambapo mwenzetu anaonyesha ujasiri, tuko tayari kuweka nyodo; ooh anapendelea wanaume; anapuuza wanawake! Tumwache afanye kazi yake,” ameeleza mmoja wa wabunge wanawake wa muda mrefu.

Makinda anatarajiwa kuwa makini katika kushughulikia wanawake wenzake, bali kitakuwa kibarua kigumu kinachoweza kuhatarisha hata nafasi yake.

Tano, Makinda ameshika nafasi hiyo huku tayari mwenyekiti wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Kikwete akishindwa kuleta umoja ndani ya chama na serikali na kati ya wabunge wa CCM na serikali yao.

Haitarajiwi wabunge waliogawanyika tangu ndani ya chama, kuungana bungeni.

Wala chama ambacho hakina nidhamu katika kufikia maamuzi, hasa wakati wa uteuzi, hakitarajii kuheshimiwa na waliobahatika kupenya tundu la uteuzi.

Kwa mfano, karibu wabunge wengi walioshinda uchaguzi, walibahatika kupenya katika kura za maoni, kwa jitihada zao binafsi.

Mtendaji mkuu wa chama, Yusuph Makamba anadaiwa kuamuru kupindisha utaratibu ili kuangamiza asiowataka na kubeba wale anaowataka.

Hivyo basi, jitihada zozote za Makinda kutaka kuunganisha makundi haya yanayotafunana, linaweza kuwa kaburi lake kisiasa.

Lakini ukiacha hilo, kuna hili la Sitta kudhoofika kisiasa. Hili imechangiwa kwa kiwango kikubwa na wale waliokuwa wanamshabikia.

Waliokuwa wanajitambulisha kuwa waaumini wake, haraka walimgeuka na kuanza kujipendekeza kwa Kikwete.

Kwa mfano, mashabiki wa Sitta hawakufanya jitihada zozote za wazi kupeleka ujumbe kwa kamati kuu ya CCM na mwenyekiti wake, kwamba uamuzi wa kumtupa Sitta haukuwa sahihi.

Mathalani, kama wafuasi wa Sitta wangepiga kura kuwakataa wagombea watatu walioletwa na CC – Anna Abdallah, Kate Kamba na Makinda, angalau wangepoza moyo wa Sitta.

Lakini hawakufanya hivyo. Badala yake, wakapiga kura kumchagua Makinda.

Miongoni mwa waliotarajiwa kuwa mstari wa mbele kumpigania Sitta, ni mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond, Dk. Harisson Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe anajua kuwa kuondoka na kuanguka kwa Sitta hakuwezi kumuweka yeye salama. Naye aweza kuwa anatafutiwa kitanzi

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: